Magreth Kinabo na Mary Gwera

Jaji Mkuu wa Tanzania,Prof. Ibrahim Hamis Juma amefungua Kongamano maalum la kusherehekea Siku ya Majaji na Mahakimu Wanawake Duniani lililoandaliwa na Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ambapo amebainisha kuwa, uwepo wa Majaji na Mahakimu Wanawake una faida nyingi ikiwemo kuongeza kuaminika kwa Mahakama na kuongeza imani ya wananchi kwa Mhimili huo na mfumo mzima wa utoaji haki.

Akizungumza jana tarehe 10 Machi, 2023 katika ufunguzi wa Kongamano hilo la siku moja (1) lililofanyika kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (JNICC), Mhe. Prof. Juma amesema kuwa, siku hiyo ni muhimu maalum kwa kusherehekea mchango mkubwa wa Majaji na Mahakimu Wanawake nchini Tanzania na Dunia nzima, ambao mchango wao ni muhimu katika utoaji haki, na hususani katika kupigania usawa katika jamii na usawa wa kijinsia.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa hotuba yake wakati wa ufunguzi wa Kongamano la siku moja (1) la Siku ya Majaji na Mahakimu Wanawake Duniani lililoandaliwa na  Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAJWA). Kongamano hilo limefanyika  leo tarehe 10 Machi, 2023 kwenye ukumbi wa  Mikutano wa Kimataifa  wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (JNICC).

“Uwepo wa Majaji na Mahakimu wanawake katika nafasi za uamuzi na nafasi za uongozi ndani ya Mhimili wa Mahakama una faida kubwa ya imani ya wananchi kwa mfumo wa utoaji haki, vilevile umesaidia Mahakama kufaidika na mitazamo tofauti huleta uboreshaji wa huduma mbalimbali,” amesema Prof. Juma.

Jaji Mkuu ameongeza kuwa, uwepo wa Majaji hao vilevile unasaidia kuifanya Mahakama kuwa na nguvu zaidi na kuwa na taswira inayozingatia usawa wa kijinsia na haki ya kijinsia.

Kadhalika,Prof. Juma ameeleza kuwa, kwa sasa hakuna Mradi wa Uboreshaji wa Huduma za Mahakama ambao unaweza kufanikiwa, bila kujielekeza katika haki za kijinsia na kuboresha mifumo inayobeba haki sawa kwa wanawake na wasichana. Hivyo Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa 2021-2025 unatambua usawa wa kijinsia kama sehemu muhimu ya mfumo wa Utawala bora wa Mahakama, akisisitiza kwamba, huwezi kuzungumzia utawala bora pale ambapo haki za kijinsia na usawa wa kijinsia hauheshimiwi.

Anasema kwa mujibu wa Matokeo ya Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2022, idadi ya watu ilikuwa milioni 61.7. Huku akisema kwamba, zaidi kidogo ya nusu ya idadi ya watu Tanzania (31.7 milioni) walikuwa ni wanawake, na wanaume milioni 30. Mahakama ya Tanzania bado ina umbali wa kutosha kufikia asilimia ya nusu kwa nusu ya idadi ya wanawake na wanaume katika Mahakama.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Divisheni ya Ardhi, Mhe. Agness Mgeyekwa aliyekuwa Mshereheshaji wa Kongamano la Siku ya Majaji na Mahakimu Wanawake Duniani akizungumza jambo katika hafla hiyo.

“Kwa sasa, ni asilimia 38 tu ya watumishi wanawake. Kazi iliyo mbele yetu ni kuziba pengo hilo ili kufikia usawa wa angalau nusu. Wajibu wa kuhakikisha tunafikia usawa ni jukumu letu la pamoja. Majaji na Mahakimu Wanawake mjitambue kuwa ninyi ni viongozi waandamizi katika utumishi wa Mahakama. Kazi zenu za kusikiliza mashauri na kuyatolea maamuzi ni nafasi za kiuongozi,” amesisitiza.

“Binafsi, mbali na kudhihirisha uongozi mahiri wa Majaji na Mahakimu Wanawake katika kutoa haki, Viongozi hao wa Mahakama wamenisaidia katika nafasi ya uendeshaji na usimamizi wa shughuli za Mahakama,” ameeleza.

Amesema kwamba, baadhi ya Kamati za Jaji Mkuu zinaongozwa na Majaji Wanawake, amezitaja Kamati hizo ambazo ni Kamati ya Maboresho (Reforms Committee), Kamati ya Kanuni (Judiciary Rules Committee), Kamati ya Ufuatiliaji na Tathmini ya Shughuli za Mahakama. Ameongeza kuwa, wapo Majaji Wanawake katika nafasi ya Majaji Wafawidhi wakiwemo wa Kituo Jumuishi cha Utoaji na Masuala ya Familia na Mirathi-Temeke, Mahakama Kuu-Kanda ya Mtwara; Mahakama Kuu-Divisheni ya Ardhi; Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Mahakama Kuu Kanda ya Moshi na Mahakama Kuu-Kituo cha Usuluhishi-Dar es Salaam.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA), Mhe. Sehel Barke amesema mafanikio mengi ya TAWJA yametokana na ushirikiano wanaoupata kutoka Mahakama ya Tanzania chini ya Uongozi wa Jaji Mkuu, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Masuala ya wanawake Tanzania (UN Women) ambapo Mwakilishi wake Bi. Rachel Boma ameshiriki katika Kongamano hilo.

Akizungumzia nafasi ya mwanamke ndani ya Mahakama, Mhe. Sehel amesema kuwa, upande wa Tanzania Bara Majaji Wanawake katika ngazi ya Mahakama ya Rufani ni taribani asilimia 38, wanawake 10 na wanaume 16, Mahakama Kuu asilimia 36, wanawake 25 na wanaume 62, Majaji Wafawidhi asilimia 33, wanawake 8 na wanaume 16, Wasajili asimilia 33, mwanamke mmoja (1) na wanaume wawili (2), Naibu Wasajili asilimia 38, wanawake 20 na wanaume 33.

Mwenyekiti wa Chama Cha Majaji na Mahakimu Tanzania, (TAWJA) na Jaji wa Mahakama ya Rufani (T), Mhe. Sehel Barke akitoa hotuba  yake kwenye kongamano la  Siku ya Majaji na Mahakimu Wanawake Duniani lililoandaliwa na  Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania(TAJWA) lililofanyika  leo tarehe 10 Machi, mwaka 2023 kwenye ukumbi wa  Mikutano wa Kimataifa  wa Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam (JNICC).

Ameongeza kuwa, kwenye ngazi za Mahakama za Mkoa, asilimia 45, Wanawake 31 na Wanaume 38 na Wafawidhi ni asilimia 50 ambapo wanawake 14 na wanaume 14, ngazi ya Mahakama za Wilaya, asilimia 50 wanawake 143 na wanaume 141, Wafawidhi asilimia 44, wanawake 59 na wanaume 76, kadhalika kwa upande wa Mahakama za Mwanzo ni asilimia 53, wanawake 467 na wanaume 408 na upande wa Wafawidhi katika ngazi hiyo ya Mahakama ni asilimia 43, wanawake 248 na wanaume 329. Kwa upande wa Zanzibar, Majaji wa Mahakama Kuu jumla ni 11 ambapo kati yao wanawake ni wanne (4) na wanaume saba (7), Mahakimu 69 kati yao wanawake 22 na wanaume 47.

Hata hivyo, Jaji Sehel ameeleza kwamba, bado kuna changamoto mbalimbali ambazo Jaji au Hakimu mwanamke anakumbana nazo katika kutekeleza majukumu yake, “Ni ukweli usiopingika kuwa Jaji au Hakimu awe mwanamke au mwanaume anatakiwa kuzingatia weledi na maadili ya kazi yake, hata hivyo kwa upande wa Jaji au Hakimu mwanamke ambaye pia ni Mama, Dada na Shangazi ana wajibu wa ziada, mtu kama huyu ana kazi ya ziada ya kuweka mizania ya kutosha kwa kazi zake za ofisi, nje ya ofisi na hata kujali afya yake kwa ujumla kwani utakuta ana majukumu mengi zaidi ya mwanaume.”

Amebainisha kuwa, kwa kutambua hilo, TAWJA imekuja na kauli mbiu ya kuadhimisha ya Siku ya Majaji na Mahakimu Wanawake Duniani, isemayo: “Majaji na Mahakimu Wanawake: Mafanikio na Changamoto”.

Jaji Barke ameeleza kuwa, kauli mbiu hiyo, inalenga kuwakumbusha Majaji na Mahakimu Wanawake kuhusu nafasi walizonazo kazini, nyumbani na kwa jamii kwa ujumla na kuwakumbusha pia kuwa wao ni wakala wa mabadiliko katika kuleta usawa wa kijinsia kutokana na nyadhifa walizonazo kwenye jamii.

Aidha, Jaji Sehel amesema kwamba, Kongamano hilo linatoa fursa kwa wanachama wake kujadili na kuzungumza ni kwa namna gani wanaweza kuendeleza ajenda ya usawa wa kijinsia na uwezeshwaji wa wanawake na ni hatua zipi kwa nafasi walizokuwa nazo wanaweza kuchukua ili kuleta usawa, kufanya tathmini ya safari ya walipotoka na walipofika mpaka sasa na pia watachambua changamoto walizokutana nazo ndani ya safari zao.

Jaji Barke anaeleza kuwa, watajadili pia kuhusu namna bora ya kukabiliana na changamoto ili kufikia lengo la kukuza na kuleta usawa wa kijinsia mahakamani, watakuja na maazimio yenye lengo la kukuza usawa wa kijinsia na kuboresha utendaji wao wa kazi. “Malengo hayo tutayapitia mwakani kuona kama tumeweza kufikia au la. Hata hivyo iafahamike kuwa ili kuwa na usawa kamili inabidi Taasisi zote za Umma na Binafsi zishirkiane na ziweke mikakati mahususi yenye lengo moja la kuhakikisha usawa kwenye sehemu zetu za kazi hapo ndipo tutaweza,” amesisitiza.

Akizungumzia chimbuko la Siku ya Majaji na Mahakimu Wanawake Duniani, Mwenyekiti huyo wa TAWJA amesema, Siku hiyo inatokana na makubaliano yaliyofikiwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa tarehe 28 Aprili 2021, kupitia Makubaliano Na. A/Res/75/274. Katika makubaliano hayo, Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilikubali kuwa kila tarehe 10 Machi ya kila mwaka iwe siku ya Majaji na Mahakimu Wanawake Duniani. Chimbuko la makubaliano hayo ni Mkutano uliofanyika Nchini Qatar.

Amebainisha kuwa, kwa upande wa Tanzania, mwaka huu ndio mara ya kwanza kuadhimisha Siku hiyo wakati kwa nchi nyingine wameiadhimisha kwa mara ya pili.

Kongamano hilo limewakilishwa na wanachama takribani 50 kutoka ngazi mbalimbali za Mahakama kwa upande wa Tanzania Bara na Visiwani na wengine wamefuatilia kwa njia ya mtandao kupitia ‘Zoom’.

By Jamhuri