Watuhumiwa wa kesi ya dawa za kulevya aina ya heroin, wanalalamikia kucheleweshwa kwa shauri dhidi yao wakidai linachukua muda mrefu tangu lilipoanza mwaka 2013.

Watuhumiwa hao wanamlalamikia Jaji wa Mahakama Kuu, Upendo Msuya wakihoji; “Sijui Mheshimiwa Jaji ana malengo gani na kesi hii. Maana ameirusha tena hadi mwakani, wakati ilibidi iendelee mwezi huu,” alisema mmoja wa watuhumiwa baada ya kesi hiyo kuahirishwa.

Watuhumiwa kwenye kesi hiyo waliokutwa na dawa za kulevya kilo 50 za heroin ni Ismail Shebe mwenye hati ya kusafiria ‘Passport’ Na. AB293433 na Rashid Said Salum mwenye hati ya kusafiria Na. AB012971. Wote ni wakazi wa Dar es Salaam.

Mbali ya watuhumiwa hao, yumo pia raia wa Iran, Majed Armand –mwenye hati ya kusafiria ‘Passport’ Na. 214488959 aliyezaliwa mjini Chabahar Agosti 25, 1973.

Kesi hiyo ilianza kusikilizwa hatua za awali, mwaka 2013, lakini Jaji Msuya aliiahirisha Novemba 30, 2015 lakini akairusha tena hadi Desemba 7, mwaka huu.

Desemba 7, 2015, Jaji Msuya aliahirisha tena kesi hiyo akijenga hoja ya kuiahirisha kwa kukataa hati ya upekuzi iliyofanywa na Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP), Lubbe aliyewakamata watuhumiwa hao.

Desemba 19, 2010 ASP Lubbe – Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi cha Kabuku mkoani Tanga, alikamata gari lenye namba za usajili za Kenya KAW276G aina ya Mitsubishi Pajero likiwa na watu wawili.

Watu hao, Shebe na Salum ambao ni mtuhumiwa wa kwanza na wa pili katika kesi hiyo, walikutwa na dawa za kulevya kilo 50. Zilifahamika kuwa ni dawa za kulevya aina ya heroin baada ya kupimwa na Mkemia Mkuu wa Serikali.

Katika mahojiano na polisi, watuhumiwa walimtaja Armand- Mkazi wa Mikocheni B, Dar es Salaam aliyeunganishwa kwenye kesi hiyo. Nyumbani kwake alipekuliwa na kugundulika kuwa na dawa nyingine za kulevya gramu 953.

Mbali na watuhumiwa, mashahidi nao wanalalamikia usumbufu wa kuitwa mara kwa mara bila kesi hiyo kuendelea na malipo yao kucheleweshwa.

“Tunapata malipo yetu kwa shida. Tunaitwa hapa Tanga, halafu unaambiwa kesi inaahirishwa. Tumekuja katika kesi ya tarehe 30, 2015 tukarudi makwetu na tumekuja tena Desemba 7, ambako pia kesi imeahirishwa,” anasema mmoja wa shahidi.

“Malipo yanachelewa. Tunakuja na kurudi. Hivi unavyoona Jaji tena ameahirisha mpaka mwakani. Sijui msajili atapanga tarehe gani. Maana tunaona usumbufu tu  na Jaji anakuja na jambo jipya kwamba haitambui hati ya upekuzi, maana yake nini?” anahoji.

Hii si kesi ya kwanza ya ‘unga’ kuendeshwa na Jaji Msuya kwani kumbukumbu zinaonesha kwamba alipata kutoa dhamana kwa watuhumiwa wanne wakiwamo raia wawili wa nje, waliotoroka baadaye.

Februari 21, 2011 polisi walikamata watuhumiw awengine katika eneo la Jogoo, Mbezi Beach jijini Dar es Salaam wakiwa na kilogramu 179 za heroin.

Waliokamatwa ni Watanzania Fred Chande na Zuberi Mbwana na raia wa nje ni Shabaz Malik Muhammad, raia wa Iran akiwa na hati mbili za kusafiria.

Hati hizo ni PQ 5144792 ya Iran na nyingine KE611868 ya kutoka Pakistan. Mwingine aliyekamatwa ni Adbulghai Pirbaksh – raia wa Pakistan ambaye hati yake ya kusafiria ni ZF410415.

Wakati kesi hiyo ikiendelea, Jaji Msuya aliruhusu watuhumiwa hao wadhaminiwe Julai 05, 2011 kwa dhamana ya Sh milioni 10 dhidi ya dawa zenye thamani ya Sh bilioni tatu.

Sheria ya Kuzuia Dawa za Kulevya ya Mwaka 1995 Kifungu cha 27 (1) (b) kinasema mtu yeyote atakayekutwa na dawa zenye thamani zaidi ya Sh milioni 10 ikiwa imethibitishwa na Kamshina wa Tume ya Dawa za Kulevya hatapewa dhamana.

Taarifa zinasema watuhumiwa baada ya dhamana walitoroka kwani hawakutokea mahakamani Julai 23, 2011 ilivyopangwa, kisha

Jaji Msuya akafuta kesi hiyo akisema ilikuwa na kasoro upande wa mashtaka.

Serikali ilikata rufaa kesi hiyo ikarudi tena mahakamani mwaka huu na kusikilizwa kati ya Agosti 4 hadi 8.

Mahakama ilimtia hatiani Fred Chande na kumhukumu kifungo cha miaka 20 jela na kulipa faini ya Sh bilioni 15.6 huku ikimwachia huru Zuberi Mbwana aliyejitetea akisema kwamba alikwenda kwa Chande kumsabahi hivyo hahusiki.

Pamoja na utetezi huo, ulioacha wengi midomo wazi kwani kwenye maelezo ya awali ya mashtaka ilielezwa mahakamani kwamba watuhumiwa walikutwa na mifuko ya kilo moja katika mfumo wa pipi zenye uzito gramu 10 kila mmoja.

Watuhumiwa hao walikamatwa kwenye nyumba ya Diana Jacob Namfua.

“Hivi kilo 179 zingeharibu vijana wangapi wa Tanzania kiasi kwamba kuna adhabu zinatolewa na kutiwa shaka. Wageni wanakuja kuharibu Watanzania. Sijui kama Rais John Magufuli analijua hili,” anasema mmoja wa mashahidi.

By Jamhuri