Jamii yatakiwa kuondokana na imani potofu juu ya kifua kikuu

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Katavi

Manispaa ya Mpanda mkoani Katavi imeendelea na zoezi la uhamasishaji wananchi juu ya upimaji wa kifua kikuu ili kudhibiti maambukizi ya ugonjwa huo hasa kwa watoto wadogo walio na umri chini ya miaka mitano.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kijiji cha Kakese katika Manispaa hiyo Mratibu wa Kifua Kikuu Manispaa ya Mpanda Dk Corinely Bruno amesema kwa kipindi cha mwaka mmoja uliopita watoto wawili waliugua kifua kikuu na walipoteza maisha.

‘Ni wazi kwamba kinga ya mtoto ni ndogo kwahiyo akipata maambukizi ya ugonjwa wa kifua kikuu hawezi kuhimili na hivyo hupoteza maisha’ alisema.

Dk. Corinely ameeleza kuwa dalili za kifua kikuu kwa watoto wakati mwingine hazijionyeshi waziwazi kama ilivyo kwa watu wazima ambapo mtoto anaweza kupoteza hamu ya kula na wakati mwingine hataki kucheza kabisa.

Aliendelea kueleza kuwa ni vizuri kuwafikisha watoto katika vituo vya afya kwa ajili ya ukaguzi wa mara kwa mara ili kubaini tatizo mapema kwani wakati mwingine mtoto haonyeshi dalili za kukohoa lakini anakuwa tayari ameambukizwa kifua kikuu.

Aliongeza kuwa katika wagonjwa wa kifua kikuu duniani kote watoto wanaougua ni asilimia 12, na kusema kuwa licha ya serikali kutoa bure dawa za ugonjwa huo bado wanakutana na changamoto ya ugonjwa huo kupuuzwa na jamii hali inayopelekea maambukizi kuongezeka.

Pia ameeleza kuwa endapo ugonjwa huo utaenea hadi katika ubongo wa mtoto na hivyo kusababisha ulumavu wa akili na mwili wa mtoto.

Kufuatia hali hiyo amewataka wazazi kuondokana na Imani za kishirikina kwa kudhani watoto wamerogwa na badala yake wajenge utaratibu wa kuwapeleka watoto katika vituo vya afya kwa ushauri zaidi ili kuokoa maisha ya watoto.

Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Mpanda Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa bwana Fred Kimeme alisema serikali inaendelea kupambana na ugonjwa wa kifua kikuu ili kuweza kuutokomeza kabisa.

‘Serikali inaendelea kupambana ili kuutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu na kutoa matibabu bure ili kufikia mwaka 2035 tunatamani tuwe tumeutokomeza kabisa’ alisema.

Aidha ameitaka jamiikuacha unyanyapaa kwa wagonjwa waliobainika kuwa na TB na badala yake wawasisitize umuhimu wa kukamilisha dozi zao.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi wamesema serikali inapaswa kuendelea na mapambano ya kutokomeza ugonjwa wa kifua kikuu kwa kutoa elimu ili wananchi waweze kujua dalili zake ipasavyo na kuwawezesha kuondokana na imani potofu.

Shija Muhoja ni mmoja wa wakazi wa kijiji cha Kakese, amekiri kupoteza watu wawili katika familia yake mwaka jana kutokana na ugonjwa wa kifua kikuu.

Shija amesema shemeji yake aliyekuwa na umri wa miaka 36 aliugua kifua kikuu lakini hawakubaini kwa muda mrefu kwa ajili ya kutumia mitishamba na bila kufahamu mtoto wake wa miaka miwili naye aliugua na kufariki.

“Mwishoni kabisa kabla hawajafariki Mjumbe wa mtaa alifika na kutueleza kuwa pengine ni dalili za kifua kikuu twende hospitali, na tulipoenda tukakutwa tumechelewa sasa japo walianzishiwa dawa lakini alianza kufariki mtoto wangu na baada ya wiki shemeji nae alikufa” amesema Shija.