Na Magrethy Katengu,JamuhuriMedia, Dar es Salaam

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linachunguza tukio la mauaji ya watu wawili, Japhari Mwinyimvua (40) mlinzi na Richard Nonyo (65) baba mzazi wa mtu anayedaiwa ni mganga wa kienyeji wa eneo hilo.

Akizungumza leo Aprili 21,2024 Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Dar es salaam SACP Jumanne Muliro amesema tukio hilo limetokea Aprili 21, 2024 majira ya saa 3 asubuhi maeneo ya Kigogo fresh, Pugu, Ilala ambapo mlinzi huyo alikutwa ameshambuliwa na baadae kupoteza maisha.

Hata hivyo katika mtiririko huo kundi la watu lilimshambulia baba mzazi wa mganga huyo na baadae akapoteza maisha wakimtuhumu mtoto wake kuhusika na kifo cha mlinzi huyo.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam wanachunguza kwa kasi tukio hilo na wahusika wote wa tukio hilo watakamatwa haraka iwezekanavyo na kufikishwa mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria .

Katika hatua nyingne, Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemkamata Furaha Dominick Jacobo (32) mkazi wa Masaki na Mustafa Kihenga (28) mkazi wa Mwenge TRA kwa tuhuma za uhalifu wa kimtandao kwa kusambaza picha chafu za video za watu zisizo na maadili kwa lengo la kujipatia fedha kwa vitisho.

Watuhumiwa hawa wanatarajiwa kufikishwa Mahakamani leo kujibu tuhuma zanazowakabili.

By Jamhuri