*Mwanafunzi wa Chuo Kikuu nusura afie kituoni

*Adaiwa kupigwa na askari kwa zaidi ya saa nne

*Ni baada ya mjomba wake kumtuhumu kumwibia zawadi ya ‘birthday’

Mwanza

Na Mwandishi Wetu

Miezi michache baada ya kuandikwa kwa taarifa za kifo cha mfanyabiashara wa madini mikononi mwa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (SAUT) kilichopo Nyegezi, jijini Mwanza, Warren Lyimo, anadaiwa kupigwa na polisi na kunusurika kifo.

Tofauti na sakata la Mtwara ambapo polisi wanadaiwa kumkamata Mussa Hamis (25) kwa tuhuma za wizi na kisha kudaiwa kutaka kumpora fedha zake, tukio la Mwanza limegubikwa na utata.

Warren (22), amelazwa katika wodi ya wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalumu (ICU), Hospitali ya Rufaa ya Bugando kwa zaidi ya wiki mbili sasa, baada ya kupigwa na watu wanaodaiwa kuwa ni askari polisi wa Kituo cha Buhongwa, wakimtuhumu kuiba kompyuta mpakato (laptop) ya mjomba wake.

JAMHURI limeelezwa kwamba kipigo alichopewa, hata akipona kuna hatari ya kupata ulemavu wa kudumu.

Chanzo cha zahama

Taarifa za awali ambazo Gazeti la JAMHURI linazo zinadai kuwa askari polisi wanne ndio waliohusika kumpiga Warren akiwa Kituo cha Polisi Buhongwa alikofikishwa Mei 16, mwaka huu.

Mmoja wa ndugu zake Warren, Rashid Mtavila, ameliambia JAMHURI kuwa alipata taarifa za kushikiliwa polisi kwake Mei 17, mwaka huu kutoka kwa baba mkubwa wa Warren, Lusamo Lyimo, anayeishi Dar es Salaam.

“Akaniomba niende Kituo cha Polisi Buhongwa kumwekea dhamana. Nilipofika sikuamini nilichokiona. Nilikuta Warren ameumizwa vibaya sana. Wala hakuwa na uwezo wa kusimama kabisa. “Mahabusu wenzake walipomshikilia na kumsimamisha, nilibaini kuwa hali yake ni mbaya. Mmojawao akaniambia; ‘huyu dogo anaumwa sana, anahitaji msaada wa haraka’,” amesema Mtavila.

Amesema alishauri Warren apelekwe hospitalini kupata matibabu, lakini Mkuu wa Kituo akagoma akidai hilo lingewezekana iwapo waliomfikisha kituoni wangekuwapo.

Warren alipelekwa kituoni hapo na mjomba wake Rodrick Ringia (anayedai kuibiwa kompyuta) kwa kushirikiana na mkewe pamoja na askari wawili wa mgambo.

“Tulimtafuta Ringia lakini hakupatikana, hivyo polisi wakaendelea kumshikilia Warren hadi saa sita usiku. Alipozidiwa, wakalazimika kumpeleka hospitali iliyo jirani. Pale wahusika wakashindwa kumtibu, ikaamuliwa apelekwe Bugando,” amesema Mtavila.

Maelezo ya polisi yaliyoandikishwa Hospitali ya Bugando yanamtaja Warren kwa jina la David Lyimo na kwamba walimuokota mtaani akiwa amepigwa (na wananchi wenye hasira).

Kisha wakaweka namba ya simu ya mjomba wake, Ringia, ili kama kuna dharura yeye ndiye atafutwe na kushirikiana na madaktari kumpatia matibabu.

Taarifa zaidi

Inadaiwa kuwa Mei 14, mwaka huu, kulikuwa na sherehe nyumbani kwa mjomba wake Warren, Ringia, anayeishi Buhongwa. Warren alikuwa mmoja wa wageni waliohudhuria tukio hilo na kushiriki kwa furaha.

Katika sherehe hizo, mke wa Ringia alimzawadia mumewe kompyuta mpakato kwa ajili ya kumbukumbu ya siku yake ya kuzaliwa.

JAMHURI limeelezwa na ndugu wa Ringia kuwa kompyuta hiyo ilihifadhiwa chumbani kwa Ringia, lakini siku mbili baadaye haikuonekana, hivyo kudhaniwa kuwa imechukuliwa na Warren aliyelala hapo siku ya sherehe na kuondoka siku iliyofuata.

“Ringia akaanza kuwahoji majirani ambao walimweleza kuwa walimuona Warren akipita akiwa amebeba begi mgongoni. Hapo ndipo Ringia akaamua kumfuata chuoni kumuuliza kuhusu kompyuta yake,” amesema mmoja wa majirani.

Taarifa zinasema Ringia na askari mgambo aliokuwa nao hawakwenda moja kwa moja chuoni, bali walimpigia simu Warren na kumwelekeza sehemu walipokuwa.

Warren, bila kujua kuwa kuna mtego ameandaliwa kwa kutuhumiwa kuiba kompyuta, akawafuata na alipofika ndipo mahojiano yakaanza kufanyika.

Warren alimsihi mjomba wake aitafute kwa makini kompyuta, akimwambia kuwa yeye hakuichukua. Ringia na askari mgambo wakamtaka awapeleke chumbani kwake wakafanye upekuzi.

Mmoja wa wanafunzi anayesoma na Warren SAUT mwaka wa watatu Kitivo cha Sosholoji, John Francis, anamtaja kuwa ni rafiki yake na kwamba wamepanga pamoja nyumba nje ya kampasi, maeneo ya Nyegezi, Nyamazoge.

“Tunalipa kodi ya Sh 50,000 kwa mwezi, sijawahi kusikia kama anajihusisha na vitendo viovu. Ni kijana mpole anayependa kukaa chuoni muda mwingi akiwa na rafiki zake. Lakini huwa hapendi kuyaweka wazi mambo yake binafsi,” amesema.

Amesema siku mbili kabla taarifa za Warren kulazwa ICU Bugando kuzagaa, alielezwa kuwa ndugu zake walifika katika nyumba waliyopanga, mmoja akijitambulisha kuwa ni mjomba wake.

Amesema walifika na gari lenye rangi ya shaba (silver) na kuwauliza wapangaji waliokuwapo iwapo wamewahi kumuona Warren akiwa na kompyuta mpakato mpya, huku wakiwaonyesha picha.

Mweye nyumba alikopanga Warren, Magai Magai, anasema: “Tangu ameanza kupanga kwangu sijawahi kusikia taarifa mbaya zinazomhusu kijana huyu.”

Mmoja wa majirani waliokuwapo wakati Ringia na askari mgambo walipokwenda kupekua chumba cha Warren (jina tunalihifadhi), ameliambia JAMHURI kuwa Warren hakutaka kupekuliwa kwa kuwa watu hao hawakuwa na kibali na kwamba hakuiba kompyuta.

“Waliingia ndani kwa nguvu. Wakampekua. Baadaye wakaondoka naye. Sikujua wanampeleka wapi, wala hatukufuatilia kwa sababu waliomchukua walituambia kuwa ni ndugu zake,” amesema.

Taarifa zinasema kuwa alipofikishwa kituoni, Warren alipigwa kwa takriban saa nne na askari polisi wanne wakitaka akubali kuwa ameiba kompyuta ya mjomba wake.

“Alipigwa mfululizo kuanzia saa tatu usiku alipofikishwa kituoni hadi saa saba usiku huku wakimwambia kuwa wanafunzi wa SAUT wanajidai sana, kwa hiyo lazima wamuadabishe,” amesema mtoa taarifa wetu naye akiomba hifadhi ya jina lake.

Hali ya Warren Bugando

JAMHURI limeelezwa kwamba kwa zaidi ya siku 10 tangu alipofikishwa Bugando Mei 19, mwaka huu, Warren hakuwa na fahamu na wauguzi walilazimika kumpa uangalizi maalumu.

Chanzo kingine kinaeleza kuwapo kwa hofu ya watu waliokuwa na nia ya kumdhuru Warren akiwa kwenye wodi za kawaida.

Inadaiwa kuwa watu hao walianza kufuatilia kutaka kujua alipolazwa, madaktari wakawashtukia na kumhamishia sehemu salama zaidi.

Kumekuwa na ukimya usio wa kawaida katika kuzungumzia ugonjwa na mazingira ya tukio zima linalozunguka sakata la Warren. Hata hivyo, wiki iliyopita alipata fahamu na kuanza kuzungumza japo kwa shida. 

Baba mkubwa wa Warren, Lusamo Lyimo, anasema: “Tunamshukuru Mungu kijana bado anapumua. Bado yuko ICU. Hawezi kukaa. Analala tu muda wote. Kuna vipimo wameshindwa kumfanyia Bugando kutokana na hali aliyonayo.

“Wameshindwa kumuingiza kwenye MRI afanyiwe vipimo vikubwa kuona maeneo ambayo ameumizwa.”

JAMHURI limemtafuta Ringia, mjomba wa Warren, ambaye ndiye aliyemfikisha kituo cha Polisi na kumsababishia zahama.

Ringia hakuwa tayari kuzungumza kwa kina na JAMHURI, akidai kuwa amebanwa na shughuli nyingi na kuomba aachwe kwanza.

Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) wa Mwanza, Ramadhan Ganzi, amekiri kufahamu kuwapo kwa tukio hilo.

“Taarifa za kijana huyo tunazo, na kwa sasa tukio linachunguzwa. Uchunguzi utakapokamilika, basi tutatoa taarifa,” amesema RPC.

Alipoulizwa kwa nini uchunguzi unachukua muda mrefu kwa kuwa ni zaidi ya wiki mbili tangu Warren kupata madhara, RPC Ganzi anasema:

“Ni kwa sababu kwa sasa kijana hajitambui. Amelazwa, hivyo inakuwa vigumu kupata maelezo yake. Huyo kwetu ndiye dira ya kila kitu.”

Kwa upande wa SAUT, taarifa za ndani za uongozi wa chuo zinaeleza kuwa umejiweka pembeni hautaki kuingilia suala hilo ukidai hakuumia akiwa eneo la chuo.

Kwa upande mwingine, JAMHURI linafahamu kwamba uongozi wa SAUT unafuatilia kwa makini yanayoendelea katika sakata la Warren ingawa linahusisha zaidi mambo ya kifamilia.

Askari polisi ashikiliwa

Kutokana na tukio hilo, JAMHURI limeelezwa kwamba Jeshi la Polisi mkoani Mwanza linamshikilia askari polisi mmoja wa Buhongwa, akituhumiwa kumpiga na kumtesa Warren.

Kuhusu sababu za kushikiliwa kwake, RPC Ganzi, anasema ni kutokana na kuzingirwa kwake na tuhuma katika sakata hilo ndiyo maana jeshi limelazimika kuchukua hatua za awali dhidi yake wakati uchunguzi ukiendelea.

By Jamhuri