Uongo wa Katibu Mkuu TALGWU

Asema ununuzi wa gari lake ulifuata taratibu wakati haukufuata

DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Katibu Mkuu wa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) Taifa, Rashid Mtima, ametoa taarifa zisizo sahihi baada ya kukanusha kuhusu Sh bilioni 1.1 za zabuni ya uchapaji wa sare ambazo ni fulana na kofia za sherehe za Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) za mwaka 2022 na mchakato wa ununuzi wa gari lake kwa matumizi ya ofisi lenye thamani ya Sh milioni 180.

Katika taarifa yake aliyoitoa Mei 26, 2022 amenukuliwa akikanusha habari iliyoandikwa na Gazeti la JAMHURI kwamba Sh bilioni 1.1 za kuchapa sare 80,000 za Mei Mosi za mwaka 2022 ‘hazijapigwa’ licha ya kuwa na dosari na kukataliwa huku mzabuni ambaye ni Kampuni ya Savana General Merchandise akiwa ametafutwa na mjumbe mmoja wa bodi ya zabuni pia akidaiwa kuwa uwezo wake wa mtaji kifedha ni mdogo na alilipwa kabla sare hizo hazijafanyiwa uhakiki.

Hata hivyo, amesahau kwamba Mei 6, 2022 alizungumza na JAMHURI kwa njia ya simu na akakiri kwamba wamezikataa sare hizo kwa kuwa zina dosari na ataanza kuzungumza jinsi gani mzabuni huyo aliidanganya kamati yake ya ukaguzi.

Pia amesahau kwamba alisema zilivyopelekwa mikoani wenyeviti wakabaini zina kasoro na kama wangefuata kifungu namba sita cha kanuni mbalimbali za Talgwu toleo la mwaka 2018 jambo hilo lisingetokea kwa sababu inataka kuwe na cheti cha ukaguzi kutoka kwa wakala anayetambulika kisheria na ripoti ya ukaguzi kutoka katika kiwanda kilichochapisha sare hizo.

“Yeye alizipeleka fulana mikoani na zikakataliwa na huko si makao makuu na kama ulitudanganya wakati wa kukagua ukatuonyesha nzuri ila tulipofika mikoani,” amesema na kuongeza: “Zikagundulika ni feki na zina kasoro, tuna uwezo

wa kuzikataa zote au baadhi hata zile 80,000 zote na kumi zilikuwa mbovu tuna nafasi ya kuzikataa kwa sababu mkataba unaturuhusu.

“Ila nisingependa tufike huko, kwa sababu kulingana na taratibu zetu za ununuzi tunatakiwa kufuata taratibu zetu, yeye ameshindwa kazi na tutamwambia ameshindwa kazi,” amesema.

Kuhusu malipo ya mzabuni yaliyobaki amesema chama hicho ni taasisi na ina taratibu zake na wameingia naye mikataba lakini hawawezi kumlipa mtu ambaye amekiuka taratibu za mkataba.

Amesema mkataba wao unawaruhusu kufanya hivyo na kwa bahati mbaya zabuni hiyo imepitia katika mazingira magumu.

Pia amesema kwa mara ya kwanza mzabuni huyo walimlipa Sh milioni 300 kisha wakamlipa Sh milioni 400 hasa baada ya kuleta kisingizio cha usafiri wa ndege kutoka India hadi hapa nchini na kiasi hicho cha fedha alicholipwa ni kikubwa kabla hajaanza kazi na hatua hiyo ni kinyume cha kanuni mbalimbali za ununuzi za Talgwu toleo la mwaka 2018 zinazomtaka alipwe asilimia 30 ya malipo kwa ajili ya kusafirisha sare hizo kutoka nje ya nchi na Mtima anatakiwa kuwathibitishia wanachama wa Talgwu kwa ujumla wake wanaokatwa asilimia mbili ya mishahara yao kila mwezi kama michango ya kuchangia chama hicho kwa kuonyesha nyaraka zilizotumika kusafirisha sare hizo.

“Tulimlipa hizo fedha, wala haina shida na kwa kuwa kitu ulichokitengeneza kina dosari, hiyo fedha itarudi tu hata kama ni shilingi ngapi itarudi hata kama tutalipa zote, kwa sababu amekiuka mkataba na hata kama amepigwa kapigwa yeye mzabuni na si sisi wateja wake,” amesema.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Savana General Merchandise, Crispin Sanga, amezungumza na JAMHURI Mei 5, 2022 na kusema wamefanyiwa hujuma na mshindani wao (Mhindi) katika zabuni hiyo na akahoji kama sare zina dosari kwa nini Talgwu walizipokea na wao kwa sasa wanasubiri kulipwa fedha zao zilizobaki.

“Sisi kazi yetu tumemaliza na tunachofanya kwa sasa hivi ni kuandika invoice ili tulipwe fedha zetu zilizobaki,” amesema.

Mbali na hayo, mzabuni huyo ndiye ameliambia JAMHURI kwamba aliposhinda zabuni aliambiwa kuwa uwezo wake ni mdogo na akatakiwa athibitishe ndipo wakaziomba benki za DTB na CRDB ziwaandikie barua Talgwu kuthibitisha

kwamba wana mtaji wa fedha.

Pia JAMHURI hatukusema kwamba mchakato wa zabuni hiyo haukuzingatia taratibu ila ni yeye Mtima aliyesema ulikuwa mgumu kwa sababu ndiyo sehemu pekee wanatumia kiasi kikubwa cha fedha kufanya ununuzi huku mzabuni wao akisema ndani ya Talgwu kuna vitendo vya rushwa hadi akahujumiwa na mshindani wake.

“Tunatumia fedha nyingi kununua sare za Mei Mosi na unavyotuona tuko imara, ni kwamba tumezingatia taratibu na kuna hatua zilichukuliwa kwa wafanyakazi mwaka juzi na lazima nisimame imara kusimamia taratibu kama kiongozi,”

amesema na kuongeza:

“Huwezi kujua kwa sababu hao wanaokuwapo katika zabuni na mimi kama kiongozi lazima nisimamie taratibu ziende, kelele za watu ni lazima, kwa sababu hii ni zabuni kubwa kuliko zote ndani ya chama. Hata wazabuni kuwatipu ni kitu cha kawaida lakini baada ya hapo tunatokaje? Taratibu zinafuatwa na mwisho mnatoka na kitu kizuri?”

Kuhusu mchakato wa zabuni hiyo, Sanga, amesema watu wa Talgwu wamegubikwa na rushwa wenyewe kwa wenyewe ndani na walimtaka mzabuni wao Mhindi wampe hiyo kazi.

“Sasa hao ngazi za juu huko wajumbe wa Bodi ya Zabuni ya Talgwu inasemekana waligombana wakitaka kumchukua huyo Mhindi na inasemekana huyo ni mtu wao wa zamani na inaonekana wananufaika naye kwa namna moja ama nyingine,” amesema na kuongeza:

“Hao ngazi za juu huko naona interest zao zikavurugika kwa sababu huyo Mhindi wao hakupata na ilivyo ni kwamba muda waliotupatia hiyo zabuni ulikuwa umekwisha na tulipata habari kwamba walikuwa Arusha huko wakatupitisha

kabla ya Januari mapema tu Desemba.

“Lakini baadaye tukaja kusikia kwamba tumeshindwa, tukasema kama ni hivyo basi haina shida, tuache na watu wa bodi ya zabuni ndio waliokuwa na ugomvi wao na dakika za mwisho Januari ndiyo tumepewa mkataba na tulitaka

kuchapisha hizo fulana hapa Tanzania tukaona viwanda vingi viko bize, vina kazi nyingine.”

Pia amesema wenyewe kwa wenyewe huko ndani ya Talgwu wana ugomvi wao na ndio waliosababisha mambo yote hayo kutokea.

Amesema wao wenyewe Talgwu wana vita yao humo ndani kwa ndani kuhusu zabuni hiyo na watajua baadaye ni nini kimetokea. 

Ununuzi wa gari la Talgwu

Kuhusu ununuzi wa gari, Mtima, amenukuliwa akikanusha taarifa iliyoandikwa na JAMHURI kwamba mchakato wake haukufuata taratibu.

“Madai ya gazeti hilo kwamba fedha za ununuzi wa gari zilitosha kununua gari jipya lakini likanunuliwa la mtumba, napenda ieleweke kwamba mchakato wa ununuzi wa gari hili ulizingatia taratibu zote za kanuni za ununuzi za chama toleo la mwaka 2018 la Talgwu,” amenukuliwa Mtima.

Licha ya kukanusha hivyo lakini Mtima si mkweli kwa sababu anajua mchakato wa ununuzi wa gari lake umegubikwa na utata.

Gari hilo la Mtima ambalo ni mtumba (used) limenunuliwa na Talgwu kwa Sh milioni 180 kutoka kwa muuzaji, Dar es Salaam Motors and Commission Agent Ltd, aliyepo makutano ya Mtaa wa Swahili na Barabara ya Morogoro eneo la

Fire bila kufuata taratibu za zabuni.

Kwa mujibu wa kanuni mbalimbali za Talgwu toleo la mwaka 2018 kifungu cha nne, ni kwamba huduma au kitu chochote kitakachonunuliwa na gharama yake ikazidi Sh milioni 80 inatakiwa itangazwe zabuni ya wazi kwa umma ili kila mtu aweze kuomba.

Licha ya kanuni hizo kusema hivyo, lakini ununuzi wa gari hilo haukutangazwa kwa umma kama inavyotakiwa na muuzaji akawauzia Talgwu bila kupitia mchakato wa ushindani wa zabuni.

Gari hilo lilinunuliwa kati ya mwaka 2017 na 2018, baada ya Mtima kupeleka maombi kwa Baraza Kuu la Talgwu ya kununua gari jipya (bila kutaja aina ya gari) lililoanza kutengenezwa kuanzia mwaka 2015 kwa ajili ya matumizi ya ofisi

yake na akaidhinishiwa Sh milioni 100.

Taarifa za uhakika ambazo JAMHURI inazo ni kwamba baada ya kutafuta gari na kulikosa kutokana na cheo chake, Mtima, akaliomba baraza hilo limuongezee Sh milioni 80 zaidi ili anunue gari lenye thamani ya Sh milioni 180 na  akapewa kibali cha kufanya hivyo.

Baada ya kupata kibali hicho, ndipo Ofisa Ugavi na Ununuzi wa Talgwu, Brigither Emmanuel, akamshauri Mtima kuhusu ununuzi wa gari lenye thamani hiyo kupitia barua yake aliyomwandikia Desemba 17, 2019.

“Kwa mujibu wa taratibu na miiko ya taaluma ya ununuzi wa vyombo vya moto kama magari kwa matumizi ya taasisi na viongozi inashauriwa kununua vipya kabisa isipokuwa ununuzi wa ndege, meli na treni yanaruhusiwa kununuliwa

mtumba kwa kibali maalumu cha wizara husika,” amesema Brigither kupitia barua hiyo na kuongeza:

“Hata hivyo, kanuni za ununuzi za chama zipo kimya juu ya utaratibu wa ununuzi wa vyombo vya moto kwa viongozi wa taasisi. Nashauri kuwa gari la katibu mkuu likanunuliwe jipya katika Kampuni ya Toyota Tanzania Ltd kwa kuwa

ndio waagizaji wa magari hayo yakiwa mapya.

“Kwa kuwa fedha hizo ni za umma na zinatokana na makato ya mishahara ya wafanyakazi wa serikali za mitaa hapa nchini ni wazi kwamba Sh milioni 180 zinatosha kupata gari jipya kwa ajili ya kiongozi wa taasisi.”

Aidha, taarifa nyingine za uhakika ni kwamba ofisa ununuzi na maofisa wengine wa Talgwu walikwenda ofisi za Kampuni ya Toyota Tanzania Ltd na kukuta gari aina ya Land Cruiser linalouzwa Sh milioni 180 linapatikana kama bajeti yao walivyotengewa.

Katika hatua nyingine, licha ya Mtima kupewa ushauri huo wa kitaalamu lakini hakuufuata na inadaiwa mwaka 2018 akaamuru gari hilo linunuliwe kwa kuwa limeshapatikana kutoka kwa muuzaji huyo ambaye hakupatikana kutokana na

zabuni kutangazwa kama kanuni zao zinavyotaka.

Bali amepatikana kienyeji kwa kuwa baada ya fedha hizo kuidhinishwa kilipita kipindi cha muda mrefu bila mchakato huo kuendelea ndipo kwa wakati huo muuzaji huyo akiwa ndiye aliyewapangisha Talgwu jengo la ofisi zao zilizokuwapo Mtaa wa Tanga na Utete, Ilala jijini Dar es Salaam kwa zaidi ya miaka 10 kabla hawajahamia Temeke karibu na Uwanja wa Benjamin Mkapa akawauzia gari hilo.

Baada ya makubaliano hayo kufanyika, taarifa za uhakika zinasema Talgwu wakafanya malipo ya gari hilo kwa awamu tano (JAMHURI lina kivuli cha nakala za mkataba wa malipo); Desemba 24, 2018 wamelipa Sh milioni 40, Januari 30, 2019 wamelipa Sh milioni 35, Februari 28, 2019 wamelipa Sh milioni 35, Machi 29, 2019 wamelipa Sh milioni 35 na Aprili 30, 2019 wamelipa Sh milioni 35.

Kasoro za gari zabainika

Baada ya malipo hayo kuanza ndipo utata na kasoro zikaibuka kutokana na gari hilo kuwa na kadi mbili (JAMHURI lina nakala za vivuli vya kadi) kutoka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) zilizotolewa na ofisa wake mmoja mwenye namba 20000269 ya kitambulisho chake wakati wa mchakato wa usajili wake.

Kadi ya kwanza ya gari hilo iliyotolewa na TRA katika ofisi zake zilizopo Mtaa wa Samora, Dar es Salaam na kuthibitishwa Januari 3, 2019 na Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive inaonyesha gari hilo lenye namba za usajili T 327 DPP aina ya Toyota Land Cruiser V8 lilitengenezwa mwaka 2015, ikiwa na maana kwamba limeingizwa hapa nchini miaka minne kabla hawajalinunua rasmi mwaka 2018 huku mmiliki wake akiwa ni Talgwu.

Vilevile, gari hilo likasajiliwa hapa nchini kwa mara ya kwanza Oktoba 6, 2014, ikiwa na maana kwamba lilisajiliwa kabla halijaanza kutengenezwa.

Januari 23, 2019, Ofisa Utumishi wa Talgwu, Cassian Mbunda, akamwandikia barua muuzaji baada ya kubaini kasoro za gari hilo.

Kupitia barua hiyo (JAMHURI lina kivuli chake) ambayo nakala yake Mtima alipelekewa, Mbunda, amesema baada ya kupokea gari hilo Januari 2, 2019 na kukaguliwa, wamebaini kuna kasoro katika kadi ya usajili iliyotoka TRA.

“Kadi inaonyesha gari limetengenezwa mwaka 2015 na limesajiliwa kwa mara ya kwanza Oktoba 6, 2014 hapa Tanzania, hivyo limekwisha kutumika kwa miaka mitano hapa nchini Tanzania na haionyeshi ni Land Cruiser la aina gani.

“Mikanda ya viti vya gari haionyeshi tarehe ya lini gari limetengenezwa kama ilivyo kawaida, pia tunaomba kupatiwa nyaraka zilizotumika katika uagizwaji, upokeaji na usajili wa gari husika,” amesema Mbunda kupitia barua hiyo.

Pia JAMHURI lina taarifa za uhakika kwamba baada ya muuzaji huyo kuipokea barua hiyo Machi 8, 2019 akapeleka kadi nyingine ya pili ya gari hilo lenye rangi ya fedha iliyotolewa na ofisa huyo wa TRA katika ofisi zake zilizopo Mtaa wa Samora mwenye namba 20000269 ya kitambulisho.

Januari 23, 2019, Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive iliithibitisha kadi ya gari hilo ikiwa inaonyesha lilitengenezwa mwaka 2013 na kusajiliwa kwa mara ya kwanza hapa nchini Oktoba 6, 2014 huku mmiliki wake ni Talgwu.

Pia baada ya muuzaji kupeleka kadi ya pili ya usajili ikabainika lilibadilishwa muundo (upgrade) wa gari hilo kutoka kutengenezwa mwaka 2013 na kuonekana kuwa limetengenezwa mwaka 2015 kisha likang’olewa mikanda ya viti na kuwekwa mipya, isiyoonyesha mwaka wa matengenezo kama inavyokuwa kwa magari mengine.