Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Halmashauri ya Jiji la Dodoma itaendelea kuyafanyia usafi kwa kuondoa taka ngumu makorongo yote ili yaweze kupitisha maji vizuri na kuondoa kero ya mafuriko wakati mvua zinaponyesha.

Kauli hiyo ilitolewa na Mkuu wa Kitengo cha usafi na uthibiti wa kata ngumu, Dickson Kimaro alipokuwa akiongelea mipango ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma katika kuhakikisha wananchi hawaathiriki na mafuriko yatokanayo ma maji ya mvua kushindwa kupita kwenye makorongo.

Kimaro amesema “Halmashauri ya Jiji la Dodoma itaendelea kuyafanyia kazi kwa lengo la kuhakikisha wananchi hawapati kero kama hizi zinazoonekana. Kama mnavyoona kule mbele kuna eneo ambalo maji yakifika darajani yanagota na kurudi kuingia katika makazi ya watu. Hapa Mtaa wa Kishoka tunasafisha korongo hili kwa kuondoa taka ngumu na kuliongezea kina ili maji yaweze kupita vizuri ndiyo sababu mnaona mtambo (JCB Backhoer) ukifanya kazi yake. Tukitoka hapa tutaenda maeneo mengine mfano Kata ya Ipagala na Kizota ili kuhakikisha usalama wa wananchi unazingatiwa katika maeneo yao kipindi mvua zinaponyesha”.

Amesema kuwa kazi hiyo ilitanguliwa na kusafisha mitaro ya maji ya mvua katika halmashauri na mitaro ya katikati ya mji na barabara kuu zinazoingia na kutoka katika Jiji la Dodoma. “Kazi hii tulianza tukishirikiana na wenzetu wa Tanroads na Tarura. Lakini kuna haya makorongo makubwa ambayo mchanga umejaa na taka ngumu. Tutayapitia yote na kuhakikisha yanakuwa safi na kupitisha maji ya mvua vizuri” alisema Kimaro.

Kwa upande wake Afisa Mazingira katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Ally Mfinanga amewataka wakazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma kuacha tabia ta kutupa taka ngumu katika makorongo ili kuyaruhusu maji ya mvua kupita kwa urahisi. 

“Wito kwa wakazi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, wakati halmashauri inachukua hatua ya kusafisha eneo hili kwa kuondoa mchanga, tope na taka ngumu wananchi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma hususani wa Mtaa wa Kishoka hakikisheni hamtumii makorongo kama sehemu ya kutupia taka ngumu. Leo hii wote ni mashuhuda tunaona hapa korongo limeziba kwa sababu tunatupa taka ngumu. Halmashauri imeweka utaratibu wa makampuni na vikundi kwa ajili ya kubeba taka ngumu. Shime kwa wakazi wa Jiji la Dodoma kuhakikisha makampuni na vikundi vinatumiwa ipasavyo” amesema Mfinanga.

Nae mkazi wa Kisima cha Nyoka, Mtaa wa Kishoka, Zawadi Juma amesema kuwa mvua zikinyesha wanahangaika sana. 

“Huku wakati wa mvua tunahangaika sana. Hata ukitaka kwenda kwenye genge huwezi kupita lazina uzunguke, hatuwezi kwenda kununua vitu dukani kwa sababu maduka yapo upande wa pili. Watoto wanaoenda shule au kutoka shule hawawezi sababu maji yanakuwa yamejaa hapa.

Mvua inaweza kuanza kunyesha saa 1 asubuhi hadi ikikata saa 4 kuvuka hamuwezi mpaka kesho yake saa 1 ndio maji yanakuwa yamepungua. Kiukweli nawashukluru sana kwa sababu serikali imeleta hii mitambo kutengeneza njia ya maji” alisema Juma.

By Jamhuri