Unapoamka asubuhi kutoka kitandani unajiuliza swali gani? 

Unapomsikia jogoo akiwika alfajiri unajiuliza nini? Je, kila asubuhi unajiuliza kuhusu hatima ya maisha yako?  

Kila asubuhi imebeba  ujumbe wa maisha yako.  Kila asubuhi Mungu anakuambia: “Nimekuamsha  salama mwanangu mpendwa. Ninakupenda  sana.  Fanya kazi kwa bidii.”

Kila asubuhi imebeba mafanikio yako. Mwandishi  wa kale aitwaye Anon anasema: “Kila  asubuhi  unakabidhiwa saa 24 za dhahabu.”  Kila  kunapokucha  kila mtu  anapokea bure zawadi  ya  siku mpya.  

Hatupokei zawadi  hiyo kwa sababu sisi ni watu  wema kuliko wengine ambao hawajafanikiwa  kuiona asubuhi tuliyoiona sisi.  HAPANA. 

Kila asubuhi tunayoipokea ina malengo na  makusudio maalumu katika  maisha yetu.  Tuitumie kila asubuhi tunayokutana nayo kama  fursa ya kubadilika kimaono, kiupendo,  kiuchumi, kiimani na kiafya.

Aliyekuwa mkurugenzi wa Apple, Steve  Jobs,  wakati akizungumza na wahitimu  wa Chuo  Kikuu cha Stanford mwaka 2005 alisema: “Kila  nikiamka  asubuhi  huwa ninajiuliza: Kama leo  ingekuwa siku yangu ya mwisho kuishi duniani,  je,  ningefanya ambacho ninataka kukifanya leo?  Je, ningeishi kama ambavyo  ninataka kuishi leo?  Na kama jibu langu lingekuwa HAPANA, basi  hapo ningejua kuwa kuna kitu ninatakiwa  kukibadilisha.”

Martin Luther, kwa upande wake alisema: “Hata kama leo ingekuwa siku yangu ya mwisho bado  ningefanya kazi ambayo ingezaa matunda kwa ajili yangu au kwa anayekuja nyuma yangu.”

Je, kwa upande wako kama leo ndiyo ingekuwa  asubuhi yako ya mwisho ya kuishi hapa duniani  ungefanya nini?

Kila asubuhi kimbia. Kila asubuhi ni lazima uwe na mbio za kuyatafuta mafanikio yako  yalikojificha. 

Mtu mmoja alisema: “Kila asubuhi swala  huamka akijua wazi kuwa lazima awe na kasi  zaidi kuliko simba ili asiliwe.  Lakini pia kila  asubuhi, simba huamka akijua wazi kwamba  lazima awe na kasi kuliko swala ili asilale njaa.”  Kimbia kwa kasi kama swala ili usiliwe na simba.  Kimbia kwa kasi kama simba ili usishinde njaa.  

Bila kujali kama wewe ni simba au swala, ni  lazima kila asubuhi uwe na kasi ya kuyatafuta  mafanikio unayoyataka.

Kila asubuhi unatakiwa kuamka na moyo uliojaa  roho  ya  ushindi.  Kila asubuhi ni lazima ujione  kama mshindi. Kila asubuhi ni lazima upige hatua  99 za kuyasogelea mafanikio yako. Asubuhi ya  leo ndiyo itakayoibadilisha asubuhi ya kesho  yako. 

Je, unafahamu siri ya asubuhi? Asubuhi ni siku nyingine. Kila asubuhi unakabidhiwa kalenda ya maisha yako.  Kila asubuhi umri wako  unaongezeka.  Kila  asubuhi  unakumbushwa  kuzitubu dhambi zako.  Kila asubuhi  unakumbushwa kuiombea kazi yako. Kila  asubuhi unakumbushwa kumwombea mke/mume  wako, watoto, marafiki na majirani zako.

Yule mwandishi wa kale aitwaye Tecumseh (1768-1813) anasema: “Unapoamka asubuhi toa  shukrani kwa ajili ya uhai wako na nguvu. Toa shukrani kwa ajili ya chakula chako na furaha yako ya kuishi. Kama huoni sababu ya kushukuru, kosa liko kwako.”

Kila asubuhi, kila mwenye pumzi hupokea muda wa saa 24 bure.  Hakuna anayepokea zaidi.  Kila  mtu hupokea kwa haki kabisa.  Kila mtu hupokea kwa kiwango sawa na hukitumia kadiri anavyotaka.  Mwandishi  H. Jackson  Brown Jr  katika makala yake  ya  ‘Time  Management’, anasema:  “Usiseme hauna muda  wa kutosha. Unayo idadi sawa kabisa ya saa kwa  siku ambazo zilitolewa kwa Hellen Keller,  Pasteur, Michelangelo, Mama Tereza, Leonardo da Vinci,  Thomas Jefferson na Albert Einstein.”

Je,  unamfahamu mnyama duma (Cheetah)? Wengi  wanajua tu kwamba ni kati ya wanyama  wenye kasi sana. 

Duma anakimbia zaidi ya maili 60 kwa saa, lakini wengi wasichokijua kuhusu mnyama huyu ni uwezo wake mkubwa wa kubadili uelekeo  kinyume na alikokuwa anakimbilia kwa kasi ile ile aliyokuwa nayo. Hapa amewashinda wanyama  wengine wote.

Wengi wetu tuna kasi sana ya maisha, kasi ya  kutafuta ajira, kasi ya mahusiano, kasi ya kutafuta  elimu nzuri, kasi ya kuzisaka fursa na kwingineko kwingi. Swali ni: Je, endapo kunatokea  mabadiliko ya ghafla kwenye eneo fulani maishani mwako, una uwezo kiasi gani wa kubadili kasi yako ili uendelee kukimbia kwenye uelekeo mwingine? 

Au ndiyo uelekeo ukibadilika na wewe unalala chali na kuanza kulalamika? Amua kubadilika.  Kila asubuhi jiambie: “Nataka kuwa kama duma.”

By Jamhuri