JK aonesha picha za wazai wake

Na Issa Michuzi,JamhuriMedia

Akiwa katika mahojiano katika kipindi maalumu cha kuadhimisha miaka 72 ya kuzaliwa cha JK72 na watangazaji wa Clouds FM na Clouds TV, Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt Jakaya Mrisho Kikwete akiwa na mkewe mbunge wa mchinga Mama Salma Kikwete alitumia wasaa huo kuonesha picha za wazazi wake, ikiwa ni pamoja na za babu yake mzaa baba, baba mzazi na mama mzazi.

Katika mahojiano hayo yaliyofanyika kijijini Msoga jana Dkt. Kikwete amesimulia kwamba babu yake mzee Mrisho Kikwete alikuwa Chifu wa Wakwere na kwamba baba yake mzazi mzee Kikwete Mrisho Kikwete au kwa jina lingine Khalfani Mrisho Kikwete alikuwa Mkuu wa Wilaya Pangani,Same na Tanga katika vipindi tofauti tofauti.

Amesimulia kwamba wakati mama yake alipokuwa mjamzito naye, babu alitamka kuwa ikiwa mtoto atakuwa wa kiume atampatia urithi wa cheo chake, cha uchifu.

Historia fupi ya Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ni kwamba alizaliwa Oktoba 7,mwaka 1950 katika kijiji cha Msoga, Mkoa wa Pwani, akiwa mtoto wa sita katika familia ya watoto tisa. Alimuoa mama Salma Kikwete mwaka 1989 na wamebarikiwa watoto nane.

Amepata elimu ya msingi na ya kati katika shule za Msoga na St. John Bosco Lugoba kati ya mwaka 1958 na 1965. Aidha, alipata elimu ya sekondari katika shule za sekondari za Kibaha (1966 – 1969) na Tanga (1970 – 1971). Alihitimu Chuo Kikuu cha Dar es Salaam mwaka 1975 na kupata Shahada ya Uchumi,

Mwaka 1976 alijiunga na Chuo Kikuu cha Maofisa wa Jeshi Monduli na kutunukiwa Cheo cha Luteni Kanali na baadaye kuwa Mkufunzi Mkuu na Kamisaa wa Siasa katika chuo hicho. Kikwete amefanya kazi katika Chama cha Mapinduzi kwa nyadhifa mbalimbali kwenye mikoa ya Singida na Tabora na wilaya za Nachingwea na Masasi.

Mwaka 1988 aliteuliwa kuwa Mbunge na Naibu Waziri wa Nishati na Madini. Mwaka 1990 alichaguliwa kuwa mbunge wa Jimbo la Bagamoyo na akateuliwa kuwa Waziri wa Wizara ya Maji, Nishati na Madini. Nyadhifa nyingine alizoshika ni Waziri wa Fedha mwaka 1994 na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kuanzia mwaka 1995 hadi 2005.

Alishika rasmi wadhifa wa urais mwaka 2005 na kuchaguliwa tena 2010 kwa muhula mwingine wa miaka mitano.Mengine, kama wanavyosema, ni historia.

Katika kumalizia mahojiano hayo Dkt. Kikwete amebainisha kwamba yuko katika hatua za mwisho mwisho kukamilisha kuandika kitabu cha maisha yake ambacho amesema kitakuwa na kila kitu kinachomhusu.