Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma

Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania zimeshauri swala la sheria ya ndoa lisifikishwe bungeni na badala yake libaki kwenye majadiliano ngazi ya jamii kwa kuwa linagusa Imani za dini na sio la kisiasa.

Katibu wa Jumuiya hiyo Sheikhe Ponda Issa Ponda amesema hayo kwenye mazungumzo maalum na Jamhuri mara baada ya kufanya mazungumzo na Waziri wa Katiba na Sheria Dk.Damas Ndumbaro leo Mei 25,2023 Jijini hapa.

Amesema moja ya ajenda kwenye kikao hicho ni mapendekezo ya jumuiya hiyo kuhusu sheria ya ndoa ambayo kwa muda mrefu imekuwa na mvutano kwenye jamii

Amefafanua kuwa utata wa jambo hilo usipotafutiwa ufumbuzi unasababisha ushoga kwa kuwa kwa umri wa miaka 15 tayari Binti au kijana wa kiume anakuwa na hisia za kuwa na mwenza hivyo si sahihi kuzuia hisia zao.

Amesema ,”pendekezo tulilopeleka kwa waziri ni Sheria ya ndoa inayopendekezwa haizingatii maoni ya wadau kwani inazuia haki za msingi kwa dini ya Kiislamu na vilevile ni kichocheo kikubwa cha ushoga na usagaji jambo ambalo ni kinyume na maagizo ya mwenyezi Mungu,”amesema na kuongeza,

Mapendekezo yetu ni kwamba Sheria ibaki kama ilivyo, tunakumbuka huko nyuma swala hili lilizungumzwa sana na halikuleta majibu ya moja kwa moja kwa kuwa limekaa kiiimani zaidi hivyo tunashauri lizingatie maoni ya wadau,” amesema.

Shekhe Ponda amesema mjadala wa muswada wa sheria ya ndoa ni mpana na mzito hivyo unahitaji subira na umakini kutokana na unyeti wa kitamaduni na wa kidini juu ya jambo hilo.

Kwa mujibu wa Sheria ya Ndoa mtoto mwenye umri wa miaka 15 anaruhusiwa kuolewa kwa ruhusa ya wazazi huku tafsiri ya mtoto chini ya Sheria ya Mtoto haijabatilisha kifungu cha 13 ya Sheria ya Ndoa ambacho kinaweka umri wa chini wa ndoa kuwa miaka 15 kwa wasichana na 18 kwa wavulana.

Aidha mwaka 2019, Mahakama ya Rufaa ya Tanzania ilithibitisha uamuzi wa Mahakama Kuu katika kesi ya Rebeca Gyumi dhidi ya MwanaSheria mkuu wa Serikali, kuwa vifungu vya 13 na 17 vya Sheria ya Ndoa ambavyo vinaruhusu mtoto kuolewa na umri wa miaka 15 kwa idhini ya wazazi na 14 kwa ruhusa ya mahakama ni vya kibaguzi dhidi ya mtoto wa kike na ni kinyume na Katiba ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

By Jamhuri