Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dodoma

Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) limewataka wahitimu wa kidato cha sita waliohitimu elimu ya Sekondari kwa mwaka 2023 kutoka shule zote za Tanzania Bara kuhudhuria mafunzo ya JKT kwa Mujibu wa Sheria kwa mwaka 2023.

Akizungumza na waandishi wa habari wa leo Mei 25,2023 Makao Makuu ya JKT Chamwino Dodoma, Mkuu wa Tawi la Utawala JKT Brigedia Jenerali Hassan Mabena ,amesema vijana hao wanatakiwa kuanza kuripoti katika makambi waliyopangiwa kuanzia Juni Mosi hadi Juni 11, 2023.

” JKT imewapangia makambi watakayokwenda kupatiwa mafunzo na wanatakiwa kuripoti kambini kuanzia Juni Mosi hadi 11 Juni, 2023 katika kambi za JKT Rwamkoma Mara, JKT Msange Tabora, JKT Ruvu Pwani, JKT Mpwapwa na Makutopora Dodoma, JKT Mafinga Iringa, JKT Mlale Ruvuma, JKT Mgambo na JKT Maramba Tanga, JKT Makuyuni Arusha, JKT Bulombora, JKT Kanembwa na JKT Mtabila Kigoma.

“Mengine ni JKT Itaka Songwe, JKT Luwa na JKT Milundikwa Rukwa, JKT Nachingwea Lindi, JKT Kibiti Pwani na JKT Oljoro Arusha na kuongeza kuwa kwa wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho waripoti katika kambi ya JKT Ruvu iliyopo Mlandizi Pwani ambayo ina miundombinu ya kuwahudumia watu hao.

Amesema kuwa wahitimu wenye ulemavu wa kuonekana kwa macho wametakiwa kuripoti katika kambi ya Ruvu JKT iliyopo Mlandizi mkoani Pwani ambayo ina miundombinu ya kuhudumia watu wa jamii hiyo.

Pia JKT limewataka vijana hao kuja na bukta ya rangi ya Dark blue yenye kiuno iliyo na mfuko mmoja nyuma, urefu unaoishia magotini isiyo na zipu na vingine ambavyo vimeanishwa.

Vingine ni track suit ya rangi ya kijana au bluu, nyaraka zote zinazohitajika katika usajili wa kujiunga na elimu ya juu, zikiwemo vyeti vya kuzaliwa na vyeti vya kuhitimu kidato cha nne.