Kairuki awajia juu walimu wanaotoa adhabu ya viboko kwa wanafunzi

Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Angellah Kairuki,amewaonya walimu wanaokiuka Kanuni za Elimu za mwaka 2002 na kutoa adhabu kali kwa wanafunzi Serikali haitosita kuchukua hatua kali dhidi yao.

Waziri Kairuki ameyasema hayo leo Januari 25,2023 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na Maafisa Elimu Kata, Wakuu wa Shule za Sekondari, Walimu Wakuu wa Shule za Msingi na Viongozi wa Elimu ngazi ya Halmashauri kwenye kikao kazi cha uboreshaji wa Usimamizi wa Elimu Msingi na Sekondari Jiji la Dar es Salaam.

Waziri ametoa rai kwa walimu kwa kukumbuka kuwa wamekasimiwa ya kuwa walinzi wa watoto wanapokuwa shuleni kwa hiyo wasiwe sehemu ya kuwafanya watoto kuwa watoro kupitia adhabu wanazozitoa zinazokiuka taratibu, miongozo na kanuni mbalimbali.

“Suala zima la adhabu ya Viboko shuleni linaongozwa na Waraka wa Elimu namba 24 wa mwaka 2002 na umeeleza bayana kabisa hivyo ni vyema walimu wakafuata taratibu zilizoanishwa kwenye Waraka namba 24 wa mwaka 2002 ambao umeeleza wazi ni nani mwenye Mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko na viboko vingapi vinaruhusiwa na kwa utaratibu upi vinatolewa kwa wanafunzi.

“Hatusemi watoto wasichapwe lakini wachapwe kwa kufuata taratibu na vigezo na kwa mujibu wa miongozo iliyowekwa.” amesisitiza Waziri Kairuki.

Waziri Kairuki amesema kuwa mwongozo huo unaeleza wazi ni nani mwenye mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko na viboko vingapi vinaruhusiwa na kwa utaratibu upi vinatolewa kwa wanafunzi.

Ameendelea kufafanua kuwa waraka huo na Kanuni za Elimu za mwaka 2002 lazima zifuatwe katika utolewaji wa adhabu ya viboko shuleni.

“Kwa Mujibu wa mwongozo huo umeelekeza adhabu hiyo ya viboko inaweza kutolewa pale ambapo umetokea utovu wa nidhamu uliokithiri au makosa ya jinai yaliyotendeka ndani au nje ya shule yenye muelekeo wa kuishushia heshima shule.

“Kwa mujibu wa waraka huo adhabu hiyo inavyotolewa lazima izingatie vigezo ikiwemo ukubwa wa kosa, umri, jinsi na afya ya mtoto na haipaswi kuzidi viboko vinne kwa wakati mmoja.

“Waraka huo umeeleza jinsi adhabu hiyo inapaswa kutolewa kwa mtoto wa jinsia ya kike na kiume. Kwa Mtoto jinsia ya kike adhabu inapaswa kutolewa mikononi, na kwa mtoto jinsia ya kiume ni kwenye makalio.

“Pia Waraka huo umeeleza kuwa mwenye mamlaka ya kutoa adhabu ya viboko ni Mwalimu Mkuu au Mkuu wa shule husika au Mwalimu mwingine atakayekuwa ameteuliwa tena kwa maandishi,” amesema.

Pia ametanabaisha kuwa kwa mtoto wa kike imeelekezwa aadhibiwe na mwalimu wa kike au labda tu kama shule hiyo haina mwalimu wa kike ndipo anaweza kuadhibiwa na mwalimu wa kiume.

Hata hivyo kumekuwa na video inayosambaa kwenye mitandao ya kijamii kuhusiana na mwanafunzi kufanyiwa ukatili na mwalimu kwa kupewa adhabu isiyo na staa na kuibua hisia kwa wazazi.