Kamati ya Jumuiya ya Madaktari Tanzania yapinga Tume

Lifuatalo ni tamko la Jumuiya ya Madaktari Tanzania kwa waandishi wa habari walilolitoa Juni 28, mwaka huu juu ya Tume iliyoundwa na Polisi kuchunguza kutekwa na kupigwa kwa Dk. Stephen Ulimboka.

 

Madaktari wote hatuna imani na Tume iliyoundwa na Jeshi la Polisi nchini yenye lengo la kuendesha uchunguzi juu ya kutekwa, kunyanyaswa na kupigwa vibaya kwa Dk. Stephen Ulimboka na tunataka chombo huru kiundwe ili kupata ukweli wa tukio hilo.

 

Pia tunakemea na kuonya juu ya vitisho vyote vinavyotolewa na baadhi ya watawala katika taasisi mbalimbali dhidi ya madaktari, mfano Hospitali ya Rufaa ya Dodoma, Bugando, Mbeya na kwingineko ambako wametishwa na kufukuzwa kwa kutumia mabavu. Madaktari tunazidi kusisitiza kuwa hakuna njia nyingine yoyote ya kusuluhisha mgogoro huu isipokuwa ni kwa kutekeleza madai na hoja za msingi za madaktari kwa njia ya mazungumzo ya dhati.

 

Madaktari tumechoka kuona huduma za afya nchini zikizidi kudorora mwaka hadi mwaka. Tumechoka kuona wagonjwa wakilala chini na watoto wakilala wanne katika kitanda kimoja. Tumechoka kuona msongamano mkubwa kwa wagonjwa katika hospitali zetu huku kukiwa hakuna mpango wowote wa uboreshaji.

 

Tumechoka kuona wagonjwa wakikosa dawa, vipimo sahihi na watumishi wa afya wakifanya kazi katika mazingira magumu yanayoviza ubora wa huduma na misingi ya taaluma. Kwa hiyo, kwa moyo wetu leo tumejitolea kutetea uboreshaji wa sekta ya afya licha ya vitisho tunavyoendelea kuvipata.

 

Rai kwa madaktari: Madaktari wote kuwa watulivu katika kipindi hiki kigumu, tunashukuru madaktari wote kwa ushirikiano na kuendelea na mshikamano.

 

MUNGU IBARIKI TANZANIA

MUNGU IBARIKI AFRIKA!


Imetolewa na

Kamati ya Jumuiya ya Madaktari