Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Bagamoyo

KAMATI ya Siasa ya CCM wilayani Bagamoyo, Mkoani Pwani, imeridhishwa na maendeleo ya ujenzi wa mradi wa soko kuu Bwilingu lililopo Chalinze ambalo limefikia hatua ya umaliziaji na kugharimu kiasi cha sh.bil 1.4 mara litakapokamilika ikiwa ni sehemu ya fedha za mapato ya ndani ya Halmashauri ya Chalinze.

Aidha imekoshwa na mradi wa duka la dawa la jamii (DRF) katika kituo cha afya Chalinze ,ambao inasaidia upatikanaji wa bidhaa ya dawa kirahisi na kwa bei nafuu.

Akitoa rai mara baada ya kamati ya siasa hiyo, kutembelea miradi mbalimbali, Mwenyekiti wa CCM Bagamoyo Alhaj Abdul Sharif Zahoro alieleza ,miradi inayotekelezwa Halmashauri ya Chalinze ni ya mfano wa kuigwa .

Alieleza, miradi hairidhishi tuu bali pia imejengwa kwa ubora kwa kuzingatia thamani ya fedha ukizingatia fedha ni za mapato ya ndani.

“Tunaipongeza Halmashauri ya Chalinze, Mkurugenzi Ramadhan Possi, mbunge wa jimbo Ridhiwani Kikwete, Mkuu wa wilaya ,watendaji na wataalamu kwa usimamizi mzuri wa miradi hii ,tuendelee na msukumo wa kuisimamia ili ambayo haijakamilika ikamilike ilihali ilete matokeo chanya kwa wananchi “

“Tunamshukuru na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha nyingi za kutekeleza miradi kwenye sekta mbalimbali” alieleza Sharif.

Vilevile akiongelea miradi ya halmashauri ya Bagamoyo aliishukuru Serikali kwa kutengwa kiasi cha fedha zaidi ya sh .bil.40 ikiwa ni sehemu ya kuanza kwa ujenzi wa Bandari ambayo itasaidia kuifungua wilaya ya Bagamoyo na kuinua uchumi.

“Niwaombe wahusika , watendaji na wataalamu na mkuu wa wilaya msaidie msukumo wa kuanza kwa Bandari hii ili kuleta kuleta matokeo na imani kwa wananchi kuinua uchumi wa wanaBagamoyo” alisisitiza Sharif.

Awali Mkurugenzi wa Halmashauri ya Chalinze Ramadhan Possi alieleza mradi wa soko kuu Bwilingu ulianza sept 2020,kwa kujenga maduka 37 ,ujenzi uliendelea kwa kujenga fremu 46 ,vizimba 230 kwa kutumia Mkandarasi Mzawa MO Building and Civil Engineering Ltd.

Possi alifafanua tayari ,wameshalipa fidia milioni 100 kwa wananchi waliopisha mradi.

Vilevile kamati hiyo ya siasa,ilitembelea ujenzi wa duka la dawa la jamii Chalinze na wodi ya wazazi kituo cha afya Miono ,mradi ambao unalenga kutoa huduma ya mama na mtoto.

Mganga mkuu halmashauri Chalinze, Dkt Allen Mlekwa alieleza,duka hilo la dawa linatoa fursa ya kupata dawa kwa bei nafuu kwani dawa zinazouzwa nje 5,000 utapata katika duka hilo k sh.1,500.

Pamoja na hayo, kamati ya siasa CCM Bagamoyo, ilipitia mradi wa shule ya awali na msingi Ridhiwani J.K ,shule ambayo ina madarasa 16, wanafunzi 760 na itapunguza mrundikano wa wanafunzi.

Kwa Upande wake, Mkuu wa wilaya ya Bagamoyo,Halima Okash aliwataka wananchi,kutunza ,kulinda na kuienzi miundombinu ya miradi ya maendeleo inayojengwa kwenye maeneo yao ili iweze kudumu.

Okash alieleza, Serikali inapeleka fedha nyingi kutekeleza miradi na ikikamilika inakabidhiwa kwa wananchi ambao wanapaswa kuilinda na kuitunza .