Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar e Salaam

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Albert Chalamila leo April 05,2024 ameongoza Baraza la Biashara Mkoa wa Dar es Salaam katika Jljijini Dar es Salaam.

Akiongea na waandishi wa Hlhabari RC Chalamila amesema baraza hilo pamoja na mambo mengine limejadili uendelevu wa biashara za wazawa, sera za wawekezaji wa nje na wa ndani ya nchi ambapo katika eneo hilo malalamiko makubwa yamekuwa wageni kutoka mataifa ya nje kujihusisha na biashara za kichuhuzi katika eneo la karikoo ambazo zingeweza kufanywa na wazawa hivyo Serikali ya mkoa inalifahamu hilo na kinachotarajiwa kufanyika ni msako wa kawaida na kutoa elimu kuhusiana na jambo hilo.

Vilevile baraza limejadili mfumo mzima wa biashara na mazingira yake, katika eneo hilo mjadala ulikuwa juu ya kufanya biashara saa 24 kwa kuwa tayari vyombo vya usafiri hususani mabasi ya mikoani yameshaanza kufanya kazi saa 24 hivyo iko haja ya biashara zingine katika mkoa kufanyika saa 24 ili kukuza uchumi wa nchi na Mkoa.

Ambapo RC Chalamila amesema ili kufanya kazi saa 24 lazima kuwepo na ulinzi madhubuti, taa, pamoja na taasisi za fedha, hivyo mara Soko la karikoo likifunguliwa biashara katika eneo hilo zitafanyika saa 24 na maeneo mengine yatajifunza kutoka karikoo.

Aidha RC Chalamila amesema vilevile baraza limejadili uchumi wa blue ambao unajikita katika uvuvi, usafirishaji, utalii, uzalishaji wa umeme, viwanda vinavyotumia malighafi za majini pamoja na mfumo mzima wa ajira.

Sambamba na hilo baraza limekubaliana kuweka nguvu sasa katika maeneo hayo ili kukuza uchumi wa Mkoa na Tanzania kwa ujumla pia baraza limejadili faida za mkoa ulipo na mataifa mengine kwa maana ya Bandari hivyo ni vizuri kuwa na mikakati ya kutumia vizuri fursa zilizoko kwa masilahi mapana ya Taifa na Mkoa.

Mwisho RC Chalamila amelihakikishia baraza kuendelea kuboresha mazingira ya kufanyia biashara, kuondoa urasimu kwa wakezaji kutoa ushirikiano wakati wote kwa sekta binafsi ili kwenda sambamba na maono ya Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan.

By Jamhuri