Na Tatu Mohamed, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amezisisitiza Mamlaka za Maji nchini kuhakikisha zinatekeleza agizo la Rais Dkt Samia Suluhu Hassan la kufunga mita za malipo ya kabla kwa wateja kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma ya maji kwa wananchi wote.

Ametoa wito huo jana wakati wa hafla ya futari iliyoandaliwa na Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kwa wadau mbalimbali wakiwemo viongozi wa Serikali, Viongozi wa Mkoa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) na wadau wengine wa Sekta ya Maji iliyoenda sambamba na dua maalum ya kumuombea Rais Samia.

Amesema kuwa ili kufanikisha utekelezaji wa agizo hilo, Wizara itashirikiana na Mamlaka za Maji nchini kuhakikisha utekelezaji wa agizo hili unafanyika vizuri.

Aidha Aweso ameitaka DAWASA kuongeza nguvu katika kukabiliana na upotevu wa maji kwenye maeneo yote ya huduma ili kuimarisha usambazaji wa maji kwa wateja wake.

Ameipongeza Mamlaka hiyo kwa kuendelea na utekelezaji mzuri wa majukumu yake ya kutoa huduma bora kwa wananchi na kuahidi Wizara kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa ili huduma ya majisafi iweze kuwafikia wote sambamba na malengo ya Serikali ya kusambaza maji mijini kwa asilimia 95 na vijijini kwa asilimia 85 kufikia mwaka 2025.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo ameipongeza Serikali kwa jitihada kubwa zinazofanyika za kuhakikisha huduma ya maji inafika kwa kila mwananchi.

“Kazi kubwa imefanyika na Serikali kwa kupitia DAWASA ya kuboresha upatikanaji wa huduma kwa wananchi wote hususani wa Mkoa wa Dar es Salaam,” ameeleza Ndugu Mpogolo.

Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Bodi ya DAWAS, Laston Msongole ameishukuru Wizara kwa kuendelea kutoa ushirikiano mkubwa kwa DAWASA na kuwezesha utekelezaji mzuri wa majukumu ya kutoa huduma ya maji kwa wote.

Amesema DAWASA imejipanga kikamilifu kuhakikisha utekelezaji wa agizo la Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu Hassan la ufungaji wa mita za malipo kabla linatekelezwa na tayari zoezi limeanza kwa majaribio kwenye baadhi ya maeneo.

By Jamhuri