Na Dotto Kwilasa,JamhuriMedia,Dodoma

Mtendaji Mkuu wa Mahakama Tanzania ,Prof.Elisante Ole Gabriel ameeleza kuwa kwa kipindi cha miaka 60 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ongezeko la Majaji wa Rufani limeongezeka kutoka Majaji 16 hadi kufikia 35 ikiwa ni zaidi asilimia 100.

Ameeleza hayo jijini hapa Aprili 5,2024 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika miaka 60 ya Muungano na kueleza kuwa ongezeko hilo limeenda sambamba na uanzishwaji wa Masjala ndogo ya Mahakama ya Rufani nchini.

Amesema wakati Dkt. Samia Suluhu Hassan akiingia madarakani Machi 2021 kulikuwa na Majaji wa Rufani 16 na katika uongozi wake hadi kufikia 03 Septemba 2023 idadi ya Majaji wa Rufani imeongezeka na kufikia 35 ikiwa ni zaidi ya asilimia 100.

Amefafanua kuwa,”ongezeko la Majaji wa Mahakama ya Rufani kwa sasa linawezesha majopo 11 ya majaji watatu, majopo saba ya Majaji watano na majopo Matano ya Majaji saba kuendesha vikao vya Mahakama ya Rufani kwa wakati mmoja huku idadi ya Vituo vya kusikilizia mashauri ya Mahakama ya Rufani imeongezeka na kutoka 16 wakati wa Mhe. Dkt. Samia akiingia madarakani na kufikia vituo 18 mpaka sasa, “amesema

Kuhusu Vituo vya usikilizaji wa Mashauri ya Mahakama ya Rufani Prof. Elisante amesema viko katika Masjala za Mahakama Kuu za Arusha, Dar es Salaam, Bukoba, Dodoma, Iringa, Kigoma, Mbeya, Morogoro, Moshi, Musoma, Mtwara, Mwanza, Shinyanga, Songea, Sumbawanga, Tabora, Tanga na Zanzibar.

“Faida zilizotokana na kuongezeka kwa Majaji wa Mahakama ya Rufani ikiwa ni pamoja na kupunguza mrundikano wa mashauri, kusogeza huduma karibu zaidi na Wananchi katika Masjala zote za Mahakama Kuu, Mashauri kusajiliwa na kuamuriwa kwa wakati na kupungua mzigo kwa majopo yaliyokuwepo, “amesema.

Akieleza historia ya Mahakama ya Rufani amesema mwaka 1963 mfumo mpya ulianzishwa ambao uliunganisha Mahakama za wenyeji na Mahakama Kuu na kuondoa ubaguzi wa rangi na ukatenganisha Mahakama (judiciary) na Utawala (Executive) ambapo Sheria za kimila zilitambuliwa na kuunganishwa ili kuondoa migongano ya sheria (Conflict of laws).

“Mabadiliko ya mwaka 1963 yaliweka msingi wa mfumo wa Mahakama zilizo chini ya Mahakama Kuu ambao upo hadi sasa,katika kipindi hicho rufaa kutoa Mahakama Kuu zilipekwa Mahakama ya Rufani ya Afrika Mashariki (E.A.C.A) na Jaji Mkuu wa kwanza Mtanzania aliyeongoza Mahakama Kuu ya Tanzania alikuwa Mhe. Augustino Saidi ambaye alihudumu kuanzia mwaka 1971 mpaka mwaka 1977,”amesema.

By Jamhuri