Kwa masikitiko makubwa na tumaini kubwa kwa Mungu, napenda kuwataarifu kwamba, huduma zote za ki-ibada na ki-Sakramenti katika Kanisa Kuu la Kiaskofu la Jimbo Katoliki la Geita zamesitishwa kuanzia leo tarehe 27 ya Mwezi Februari ya Mwaka wa Bwana 2023.

Uamuzi huu unafuatia tukio la KUFURU NA UNAJISI lililofanyika ndani ya Kanisa hili, ikiwa imafanyika pia Kufuru kubwa kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu, na unajisi kwa utakatifu wa jengo hili la Kanisa na vifaa mbalimbali vya Ibada Takatifu.

Kwa Dikrii hii, Mimi Flavian Matindi Kassala, ambaye kwa Neema ya Mungu na Mamlaka ya Kiti cha Kitume ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Geita, na ambaye Sahihi yangu nimeiweka hapo chini, na kwa mamlaka ninayopewa na Sheria Kanuni ya Kanisa (Rejea Na 1211-1213), na kwa maelekezo ya Mamlaka ya Kiaskofu, (Rejea Ceremonial of Bishop namba 1070-1072) napenda kutamka kwamba:

  1. Uharifu uliotokea katika Kanisa Kuu la Jimbo la Geita usiku wa kuamkia tarehe 26 Februari 2023 NI KUFURU KUBWA kwa Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na umeivunjia Sakramenti ya Ekaristi Takatifu Heshima yake kwa kiasi kikubwa sana na hivyo umeathiri.
  2. Uharifu uliotokea katika Kanisa Kuu la Jimbo la Geita usiku wa kuamkia tarehe 26 Februari 2023 UMELINAJISI Kanisa hili katika utakatifu wake uliowekwa wakati wa Kutabarukiwa kwake.
  3. Uharifu uliotokea katika Kanisa Kuu la Jimbo la Geita usiku wa kuamkia tarehe 26 Februari 2023 ni UHARIFU MKUBWA SANA ambao umeiathiri kwa kiasi kikubwa sana hadhi na Muumini Mkatoliki na Jamii yetu kwa ujumla.

Kutokana na matukio hayo, Kanisa hili limepoteza kwa kiasi kikubwa Baraka yake na jamii ya Waamini imeumizwa sana kutokana na Kashfa, Kufuru, na Unajisi uliofanyika kwa Imani yetu. Na hivyo ninaagiza kwamba:

  1. Kanisa Kuu la Kiaskofu la Jimbo Katoliki la Geita halistahili kwa maadhimisho ya Sakramenti ya Ekaristi, wala ya Sakramenti yoyote, wala kwa ibada yoyote.
  2. Kufuatia hali hii, Kanisa Kuu la Kiaskofu la Geita litabaki limefungwa kwa huduma zote za Ki-Ibada kuanzia tarehe 27 Februari 2023 hadi tarehe 18 Machi 2023, ili kusubiri Utakaso wake.
  3. Kwa kipindi hicho cha kufungwa kwa Kanisa, Familia nzima ya Mungu Jimboni Geita inaingia katika kipindi cha siku 20 za kuelekea adhimisho la TOBA YA MALIPIZI (Penitential Reparation) kuanzia tarehe 27 Februari 2023 hadi tarehe 18 Machi 2023.
  4. Kwa kipindi chote cha kuelekea Toba ya Malipizi Mapadre waandae na kuwaandaa Waamini katika Jimbo zika kwa Ibada za Upatanisho, mahubiri ya Toba, na Mafundisho juu ya Utakatifu wa Kanisa na kuyatoa daima kwa waamini wao ndani ya maadhimisho mbali mbali.
  5. Kwa kipindi chote cha kuelekea Toba ya Malipizi waamini wote Wakatoliki wanaalikwa kusali, kufunga, kutubu, kupokea Sakramenti ya Upatanisho na kuomba huruma ya Mungu. Katika Matendo yote haya tuombe Mungu atujalie wongofu wa ndani.
  6. Kanisa Kuu la Jimbo litafunguliwa tarehe 18 Machi 2023 kwa adhimisho ibada ya MISA TAKATIFU itakayoanza saa Nne asubuhi, na itakayohusisha pia maadhimisho ya: TOBA YA MALIPIZI; BARAKA KUTAKATIFUZA KANISA KUU; NA KURUDISHA EKARISTI TAKATIFU NDANI YA KANISA KUU.
  7. Adhimisho la tarehe 18 Machi 2023, litakuwa ni la Kijimbo, na hivyo Mapadre, Watawa, na Waamini wanawajibu wa kuhudhuria. Watu wote wenye mapenzi mema wanakaribishwa pia kushiriki katika maadhimisho yote haya.

Hali tukiyaweka haya yote mikononi kwa Huruma ya Mungu,
SERVUS MISERICORDIAE VULTUS

FLAVIAN MATINDI KASSALA
ASKOFU WA JIMBO KATOLIKI GEITA

By Jamhuri