Katiba mpya itakimudu kizazi cha ‘FACEBOOK?’

Suala la maisha na siasa ni kama lile fumbo la yai na kuku. Kipi kinaanza kati ya siasa na maisha. Ni siasa ndiyo inayozaa maisha ama ni maisha ndiyo yanayozaa siasa? Kipi ni mzazi wa kingine?

Katika maswali kadhaa hapo juu nimetoa swali kuhusu mtu kushindwa kudumisha upendo katika ndoa yake. Ukiamua ‘kuli-politicalize’ suala hilo utasema uchumi mbaya na ugumu wa maisha unaleta kutoelewana ndani ya ndoa. Lakini inakuwaje kwa wale walio na maisha mazuri na bado ndoa zinawasumbua? Je, nao watasema ni kushindwa kwa siasa? Tuache hilo, tumuangalie huyu kiongozi wa dini anayeiba wake za waumini wake. Huyu naye atatuambia ni kutokana na sababu za kisiasa ndiyo maana anafanya hivyo? Ninachokiona mimi ni kuwa jamii ya Kitanzania imepotoshwa mno na inaendelea kupotoshwa na hili dude liitwalo siasa. Siasa zimechukua nafasi ya uwajibikaji na sasa wengi wanaona ukombozi upo katika siasa. Unapomuuliza mtu kwa nini anafanya uzembe kazini halafu anakujibu (kwa sababu ya katiba mbovu), basi bila shaka unatambua moja kwa moja kuwa tupo katika hali mbaya ya kifikra na kimtazamo. Wanasiasa wametudanyanya na kutupoteza kwa ajili ya maslahi yao na wafuasi wao.

Kwa ushirikiano na baadhi ya vyombo ‘uchwara’ vyahabari, wanaelekea kushinda makakati wao wa kugeuza akili za Watanzania kuwa za kiutumwa. Kama alivyoniambia rafiki yangu mmoja, “sasa wanatu-localize bila falsafa na tunaendelea kuamini kuwa ukombozi wetu umo mikononi mwao.” Tunapotea! Propaganda na blaa blaa zitapita lakini uhalisia utadumu daima. Chama tawala wakati mwingi hakiweki peupe ukweli wote na wakati huo huo vyama vya upinzani vinawaghilibu wananchi. Wakati chama tawala kupitia viongozi wake na watendaji serikalini wanawaambia wananchi kuwa wanafanya kila juhudi kuwaokoa kimaisha, vyama vya upinzani vinahubiri kuwa wokovu unaonenwa na CCM umeshahamia kwao, hivyo wapewe nafasi. Hakuna anayewapa ukweli wananchi kuwa ‘wawajibike!’ Kwa mfano, katika sayansi ya uchumi wa mataifa wapo wadau watatu wanaotajwa kuratibu ukuaji ama udororaji wa uchumi (major economic players). Hawa ni mtu mmoja mmoja (households), biashara, taasisi na kampuni (firms) na mwisho ni serikali (government).

Katika mfumo wa kijamaa serikali inakuwa ndiyo mhimili wa uchumi kwa maana kuwa ukuaji na mdororo wa uchumi unaweza kukamilishwa kwa sehemu kubwa na serikali pekee. Katika mfumo wa kibepari (ambao Tanzania tunaogelea kwa kasi), serikali inabaki kama msimamizi wa sheria zinazotawala mchezo wa uchumi (regulating and monitoring). Mtu yeyote anayefahamu uchumi vizuri atakubaliana nami kuwa hali mbaya ya uchumi wa Tanzania (chini ya ule wastani ulioletwa na mabadiliko ya kidunia), imechangiwa kwa sehemu kubwa na kushindwa kwa mtu mmoja mmoja. Nashangaa kuwa wanasiasa wanajifanya kuwa hawalioni hili, wanaingiza siasa kwa mambo hata yanayoweza kumalizwa kitaalamu. Ni kweli kuwa siasa ina nafasi katika kuandaa mazingira ya uchumi wa kitaifa, lakini kukwamuka kiuchumi katika ngazi ya mtu mmoja mmoja kunategemea juhudi za mtu binafsi. Wanasiasa hawataki kuwaeleza ukweli mchungu Watanzania ya kwamba wafanye kazi kwa bidii.

Sijawahi hata siku moja kuwasikia viongozi wa vyama vya upinzani wakisema angalau sentensi ifuatayo; “Watanzania wengi mna maisha magumu lakini sehemu ya ugumu huo wa maisha yenu umetokana na kasumba ya kutofanya kazi kwa bidii”. Pamoja na kuwa wanasiasa wanafahamu kuwa umasikini wa Watanzania unatokana na uvivu wetu wa kuwajibika na kukosa ubunifu hata kwa rasilimali tulizojaliwa, lakini hawasemi hili. Wanaona kuwa wakisema hili watu watafumbuka na kubaini kuwa kumbe siasa ni msaidizi tu na si ‘mungu pekee’ wa maendeleo. Huenda ni hofu ya kukosa watu kwenye maandamano ama katika foleni za kuwapigia kura ili wapate ‘kula’ (wao wanajua!) Kuna mtu anakumbwa na baa la njaa kwa sababu alilima na mvua hazikunyesha, lakini kuna ambaye anakumbwa na baa la njaa kwa sababu hakulima licha ya kuwa na ardhi na mvua za kutosha. Kuna tatizo la askari wa barabarani kupokea rushwa kwa sababu magari ni mabovu, lakini kuna watu wanaagiza ama kununua magari mabovu bila hofu kwa sababu wamekusudia kuendelea kutoa rushwa.

Ni watu hawa hawa wavivu wa kulima wanataka katiba mpya ili kuwe na neema ya chakula! Ni hawa hawa watoa rushwa wakubwa barabarani ambao nao wamo katika kulilia katiba mpya! Tumekuwa watu wa ajabu na hatujielewi kuwa tunapotea. Katiba mpya inahitajika sana sana, lakini katiba mpya haitaingia majumbani kuwasaidia watu waivishe vyakula, katiba mpya haitawafulia watu nguo. Katiba mpya haitazuia mtu kuwa na vimada nje ya ndoa. Nimetoa mifano midogo lakini katika ngazi mbalimbali kuna mambo yanayotokana na watu kutowajibika, halafu lawama zinahamia kwa siasa. Zinyoosheni vidole siasa lakini tusisahau kuhimizama kuwajibika. Mimi ni mwanamapinduzi halisi na ninatamani kuona taifa hili likipata mabadiliko makubwa ya kisiasa – ikibidi hata kuking’oa chama tawala madarakani. Na tulipofikia ninaona kuwa ni pazuri kwa sababu miaka ya CCM kukaa madarakani inaelekea mwishoni. Lakini ninawatahadharisha wote wanaojiandaa kuiondoa CCM wawe makini.

Mbinu wanazotumia kuandaa fikra za Watanzania ili wawachague (ama wawasaidie kuendesha mapinduzi kwa maandamano) zitakuja kuwagharimu. Ukweli ni kwamba hakuna serikali yoyote duniani inayomfanyia mwananchi kila kitu, lakini fikra za Watanzania kwa sasa zinaamini kuwa CCM ikiondoka madarakani wanaokuja watawaingiza katika nchi ya ahadi. Katiba inaweza kubadilika lakini tutafanyaje kuwabadilisha wale waliozoea kushinda vijiweni wakicheza bao na huku wanalalamika kuwa maisha ni magumu? CCM itaondoka madarakani lakini utamaduni wa watu kukosa maadili tutauondoaje? Kwa vyovyote vile mimi si mwanaharakati wa kisiasa (nina falsafa ya kutoruhusu siasa kuamua hatima ya maisha yangu) lakini ninawashauri wanasiasa na Watanzania wote kuacha kuwa kama makinda ya ndege, kwa hulka ya kupanua midomo na kusubiri siasa iwaletee kila kitu. Ninaona kiini cha kukwama kwa taifa hili tunakipita pembeni; hili linanipa shaka kuhusu jeuri’ ya Katiba mpya kukimudu kizazi cha ‘Facebook’.

[email protected] 0719 127 901