Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia, Kibaha

MTOTO Angel Mseven (8) mwanafunzi wa darasa la pili shule ya msingi Carisa Mwendapole, Kibaha mkoani Pwani amekutwa amefariki dunia ndani ya shimo la maji taka.

Alithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kamanda wa Polisi Mkoani Pwani, Pius Lutumo alisema, mnamo Mei 7, saa 3:15 asubuhi huko katika kituo cha Polisi Kibaha, ilipokelewa taarifa ya mtoto kuzama maji kwenye shimo na kusababisha kifo chake.

Alieleza, mtoto huyo ilisemekana alikuwa anacheza na watoto wenzake eneo hilo na baadae kukutwa tayari amefariki.

Lutumo alifafanua, uchunguzi wa awali wa Jeshi la Polisi mkoa kwa kushirikiana na vyombo vingine vya kiuchunguzi umebaini kwamba mtoto huyo aliuawawa kisha kisha kutumbukizwa katika shimo hilo tofauti na taarifa iliyopokelewa awali.

Lutumo alieleza, Jeshi la Polisi mkoa limeshaanza msako mkali wa kuwatafuta watu ama mtu aliyehusika na tukio hilo.

Jeshi hilo limetoa wito kwa raia wema wenye taarifa sahihi ya tukio hilo kujitokeza kutoa ushirikiano wa kufanikisha kuwakamata wahusika haraka iwezekanavyo ili haki iweze kutendeka.

Mnamo tarehe 6 Mei, Mwalimu Mseven wa shule ya sekondari Tumbi ilisambaa taarifa kwenye makundi mbalimbali ya watsapp kuwa amepotelewa na mtoto akiwa amevaa nguo ya kitenge ambapo baadae taarifa zilitolewa kwamba amepatikana lakini akiwa amefariki dunia.

By Jamhuri