Na. WAF – Dodoma

Takwimu zinaonesha kuwa kila wagonjwa watatu wanaolazwa mmoja ana magonjwa yasiyoabukiza ambapo inapelekea kuchangia asilimia 34 ya vifo Tanzania.

Hayo ameyasema leo Mkurugenzi wa Tiba Prof. Paschal Ruggajo kwenye mkutano wa mafunzo kwa Mama na Baba lishe, bodaboda pamoja na Waheshimiwa Madiwani juu ya uelimishaji na uhamasishaji jamii katika kudhibiti na kuzuia magonjwa yasiyoambukiza uliofanyika Jijini Dodoma.

“Kwa kushirikiana na wadau tumekusanyika hapa tukiwa na makundi maalumu kwa lengo la kupeana elimu kwa pamoja namna ya kupunguza magonjwa yasiyoambukiza” amesema Prof. Ruggajo.

Aidha, Prof.Ruggajo amebainisha kuwa magonjwa haya yana gharama kubwa kimatibabu hivyo wameweka msisitizo kwenye kinga kwa kuepuka ulaji usiofaa, kufanya mazoezi ili kuepuka tabia bwete na kuzingatia sheria za uendeshaji wa vyombo vya moto hususan bodaboda kwa kufuata sheria.

“Tuna imani kubwa kuwa tukimuelimisha mama na baba lishe juu ya kupunguza kiwango cha chumvi na sukari pamoja na mafuta katika mapishi yao akifanya hivyo nae atakua amesaidia katika kupunguza magonjwa haya yasiyoambukiza” amesema Prof. Ruggajo.

Pia, kwa upande wa bodaboda amesema wakiendesha vyombo vyao kwa kufuata sheria za barabarani nao watakua wamesaidia katika kupunguza magonjwa haya yasiyoambukiza.

Naye, dereva wa bodaboda Abdallah Kagoma amesema katika mkutano huo amejifunza mambo mengi hivyo ataenda kuwaelimisha wengine nao wapate uelewa ili kwa pamoja waweze kupunga ajali na kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza.

“Miongoni mwa mambo mengine niliyojifunza ni pamoja na kujua kumbe ajali nazo ni miongoni mwa magonjwa yasiyoambukiza, lakini pia tutakua walinzi kwa wenzetu na kuwashauri ili tupunguze ajali” amesema Bw. Kagoma

Kwa upande wake Mama lishe kutoka Sabasaba Bi. Diana Karua amesema baada ya kupata mafunzo hayo wataenda kupika vyakula ambavyo vitasaidia katika afya za wananchi.

“Japo unaweza ukaamua kupika chakula kwa kufuata msingi mzuri lakini baadhi ya walaji wenyewe wanataka uongeze mafuta au chumvi nyingi hii ni miongoni mwa changamoto tunazokutana nazo ambayo kimsingi vinahatarisha afya zao kwa kupata magonjwa yasiyoambukiza,” amesema Karua.