Na Allan Vicent,JamhuriMedia,Tabora

Walinzi 5 wa jadi maarufu kwa jina la Sungusungu wilayani Sikonge mkoani hapa wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi mjini Tabora kwa tuhuma za mauaji ya mwananchi wakiwa kwenye doria.

Walinzi hao ambao ni wakazi wa Kijiji cha Ibumba, Wilayani humo wamesomewa shitaka la mauaji ya kukusudia katika Mahakama hiyo wakituhumiwa kumpa adhabu kali ya mateso na kipigo Abdallah Idd.

Imeelezwa kuwa kipigo hicho kilitokana na kijana huyo kupigiwa kura za ndiyo na wananchi kuwa anahusika kwenye tukio la kuvunja na kuiba kwenye vibanda vya maduka kijijini hapo.

Waliopandishwa kizimbani na kusomewa shitaka hilo mbele ya Hakimu Mkazi John Mdoe ni Kamanda wa kikundi hicho cha Sungusungu Bakari Kiyola, Mrisho Maulid, Mashaka Christopher, Kassim Christopher na dada Jamila Ibrahim.

Akiwasomea shitaka hilo, Wakili upande wa Jamhuri Joseph Makene amesema watuhumiwa wote 5 wanakabiliwa na shitaka la mauaji ya kusudia katika Kijiji hicho Aprili 14 mwaka jana.

Ameiambia mahakama kuwa ushahidi wa shauri hilo umekamilika na upande wa Jamhuri utaleta mashahidi 10 na vielelezo 2 ambavyo ni taarifa ya Daktari na ramani ya eneo ulipotupwa mwili wa marehemu baada ya kuteswa walipokuwa wakimhoji kuhusiana na tukio la kuvunjwa vibanda vya maduka.

Hakimu Mdoe alipowahoji washtakiwa kama watakuwa na mashahidi, mshtakiwa namba 1 Bakari Kiyola yeye alisema hana shahidi yoyote huku wenzake wanne wakisema kuwa watakuja na mashahidi wawili wawili kila mmoja.

Washitakiwa wote 5 walirejeshwa mahabusu kwa kuwa Mahakama hiyo haina uwezo kisheria kusikiliza shauri hilo la mauaji.

Ameeleza kuwa watasubiri hadi Msajili wa Mahakama
atakapopanga tarehe ya kuanza kusikilizwa shauri lao katika Mahakama Kuu Kanda ya Tabora na kutolewa uamuzi.

By Jamhuri