Timu ya Taifa ya Tanzania Bara ‘Kilimanjaro Stars’ kesho Alhamis Desemba 7, 2017 inatupa karata yake ya pili kwenye michuano ya CECAFA dhidi ya Zanzibar Heroes ya Zanzibar kwenye mchezo wa kwanza utakaoanza saa 8.00 mchana kwenye Uwanja wa Kenyatta, Machakos.

Mchezo huo unatarajiwa kushuhudiwa na Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk. Pindi Hazara Chana ambaye anaiwakilisha nchi katika Kenya. Kuelekea mchezo huo, Kilimanjaro Stars imefanya mazoezi yake ya mwisho leo Desemba 6, mwaka huu asubuhi kwenye Uwanja wa Machakos Academy chini ya Kocha mkuu Ammy Ninje.

Kocha Ninje amesema maandalizi ya mchezo huo dhidi ya Zanzibar yamekamilika na kufanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza kwenye mchezo wa kwanza dhidi ya Libya.

Mbarak Yusuph ndio mchezaji pekee atakayekosekana kutokana na kusumbuliwa na mejeraha ya misuli lakini Kocha Ninje amesema ana washambuliaji wanne ambao atawatumia kuziba nafasi hiyo ya Mbarak.

Nahodha Himid Mao amesema mechi hiyo itakuwa ngumu lakini wako tayari kupambana kupata matokeo ya ushindi kwakuwa kila mmoja wao ana morali kubwa na nia ya kupata ushindi.

Amesema kikubwa watatakiwa kutulia na akili zao kuzielekeza uwanjani kuhakikisha Kilimanajro Stars inabeba pointi zote 3.
Kilimanjaro Stars inashuka kwenye mchezo wa kesho ikiwa na pointi moja katika Kundi hilo la A ambalo linaongoza na Kenya wenye pointi 4 wakifuatiwa na Zanzibar wenye pointi 3, Libya wenyewe wana pointi 2 wakati Rwanda wanaburuza mkia wakiwa hawana pointi wakifungwa kwenye michezo yake yote miwili iliyochezwa.

Timu hizo za Kundi A zinaingia Uwanjani hiyo kesho zikiwa kwenye nafasi tofauti wakati Kilimanjaro Stars ikikamata nafasi ya nne ikiwa na pointi moja iliyoipata kwa kutoka suluhu bila kufungana na Libya,Zanzibar Heroes wao wapo kwenye nafasi ya pili wakiwa na pointi tatu baada ya kushinda mechi yake ya kwanza dhidi ya Rwanda.

Timu nyingine kwenye Kundi hilo mbali ya Kilimanjaro Stars na Zanzibar Heroes ni Libya na Rwanda ni wenyeji Kenya “Harambee Stars”. Kundi B lenyewe linacheza mechi zake huko Kakamega likiwa na timu za Uganda, Burundi, Ethiopia na Sudan Kusini.

Please follow and like us:
Pin Share