Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia,Kigoma

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahman Kinana ameishauri Kampuni ya huduma za meli nchini (MSCL) kujiendesha na kuanza kufikiri kibiashara ikiwemo kuomba dhamana za serikali Ili kukopa fedha na kununua meli mpya ili kukidhi mahitaji ya huduma za usafiri na usafirishaji katika ziwa Tanganyika.

Amesema hayo wakati alipotembelea na kukagua ukarabati wa meli ya MV. Sangara mjini inagharimu shilingi bilioni 8.4 ameshauri ni muhimu kampuni hiyo ifikirie kibiashara zaidi.

Aidha Kinana ameipongeza Serikali ya CCM Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea na kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ikiwa ni utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya CCM 2020-2025.

Hiyo ni baada ya kuambiwa kuwa kama meli hiyo ambayo ni ya mafuta ikikamilika bado mahitaji ya huduma za meli kwenye ziwa Tanganyika ni makubwa na kwamba zinahitajika meli nyingine tatu.

“Sikilizeni ndugu zangu msisubiri hela kutoka bajeti ya serikali, ombeni dhamana ya serikali mkakope mnunue meli mpya.. pesa za namna hiyo ziko nyingi duniani.” amesema Kinana.

Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Ndg Abdulrahman Kinana akikagua meli ya mafuta  MT.Sangara ya Kampuni ya huduma za meli nchini (MSCL)  iliyokuwa inafanya kazi Katika ziwa Tanganyika mkoani Kigoma  kabla ya kusimama Kwa ukarabati

Kinana pia alipata nafasi ya kutembelea meli kongwe kabisa duniani ya MV Liemba ambayo nayo ipo kwenye mpango wa kukarabatiwa kwa kiwango kikubwa na serikali katika mwaka huu wa fedha 2022/2023. Meli hiyo ya mv Liemba ina umri wa zaidi ya miaka 100 na imeingia kwenye orodha ya urithi wa dunia chini ya UNESCO.

Kinana ambaye ameambatana na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Itikadi na Uenezi Ndg Shaka Hamdu Shaka ameanza ziara yake ya siku tano katika mikoa ya Kigoma, Kagera, Geita na Mwanza.

By Jamhuri