Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara Abdulrahaman Kinana, ameeleza kuwa Mwenyekiti wa Chama hicho na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia Suluhu Hassan ni msikivu,mtulivu na mwenye kupokea ushauri na kutoa uamuzi kwa kutanguliza maslahi ya Taifa.

Amesema chini ya uongozi wa Rais Samia Tanzania imepiga hatua kubwa ya maendeleo na kwa sasa hata ukusanyaji wa mapato umekuwa uko juu kuliko wakati wowote ule katika nchi yetu, hivyo amesema hata wanapompongeza na kumsifu ni kutokana na kazi kubwa na nzuri anayoendelea kuifanya.

Mzee Kinana ameyasema hayo leo Julai 23, mwaka 2023, wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma ulioandaliwa na Mbunge wa Kondoa Dk.Ashatu Kijaji kwa ajili ya kuelezea utekelezaji wa Ilani katika kipindi cha miaka miwili ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia.

“Katika kipindi cha miaka miwili Rais Samia amefanya mambo makubwa ya maendeleo na hiyo inatokana na uongozi wake mzuri unatokana utulivu, usikivu, kupokea ushauri na kufanya uamuzi wa busara kwa manufaa ya Watanzania. Kwa hali ilivyo na kwa hatua tuliyopiga tukienda hivi tunavyokwenda mpaka kufika 2025…

“Nina uhakika kila Mtanzania atakuwa na sababu ya kusema tuendelee na CCM, tuendelee na Rais Samia Suluhu Hassan. Hatutokuwa na sababu nyingine yoyote kwanza ni utamaduni wetu Chama Cha Mapinduzi hatubadilishi uongozi katikati ya safari, ukitaka kubadilisha sababu itakuwa nini, hakuna, ” amesema Mzee Kinana

Amesisitiza lazima wampe nafasi ili yale aliyokusudia chini ya uongozi wa Chama chetu yatimie.”Ikifika 2025 tunakwenda na Rais Samia.Hatusemi haya kwa kujivuna bali kwa utekelezaji wa Ilani ya CCM lakini tunaangalia na wenzetu wa nchi jirani wanakwendaje.

“Nchi yetu imetulia, inamaani, ina umoja, inamshikamano, nchi ina malengo, na ina mipango ambayo inatekelezwa na kila mtu ni shahidi, CCM itaendelea kuchaguliwa kwa sababu ina sera nzuri ina Ilani nzuri inayotekelezeka,” amesisitiza.

Aidha ametumia nafasi hiyo kuzungumzia umoja na mshikamano walionao watanzania ambao uko imara na ndio maana kuna watu wamejaribu kuwagawa wananchi kwa misingi ya udini wameshindwa, wamejaribu kuwagawa kwa misingi ya ukabila wameshindwa.

” Kuna watu wamejaribu kutugawa kwa misingi ya ubara na visiwani wameshindwa huku akifafanua katika Bara la Afrika ziko nchi nyingi zimeajaribu kuungana na wanazifahamu ikiwemo Afrika Magharibi na nchi za Uarabuni zote zimesambaratika umoja haupo, lakini Tanzania muungano wao umeendelea kuwa imara na mwakani muungano huo unafikisha miaka 60.

“Sababu ni misingi imara iliyojengwa na wasisi wa taifa letu hayati baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na marehemu Abeid Aman Karume, misingi yenyewe migumu na mnakumbuka katika kipindi mbalimbali muungano wetu umepitia kashikashi lakini tumeendelea kuwa imara,” amesema Kinana.

Ameeleza kwamba anaungana na viongozi wengine pamoja na wananchi kumpongeza Mwenyekiti wa Chama na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. Samia kwa uongozi wake madhubuti.

Pia amesema chini ya uongozi wa Rais Samia makusanyo ya fedha yameongezeka na yamekuwa juu kuliko wakati wowote.“Fedha hizo ni mapato ya ndani, mapato ya nje. Mapato ya ndani yaliyokusanywa na serikali katika miaka hii miwili kwa kila mwezi yako juu kuliko kipindi chochote, makusanyo yamefanikiwa bila mtu kusukumwa, bila kutishwa bila mtu kuwekwa mahabusu.

“Hivi karibuni kulikuwa na mashirika mawili duniani ambayo yanafanya tathimini ya hali ya uchumi na namna nchi inavyoweza kukopesheka.Mashirika yote mawili yametoa alama ya juu kwa serikali ya Chama Cha Mapinduzi inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

“Maana yake ni nini ukitaka kupewa msaada hawa wanaaminika, watatumia misaada vizuri hawataiba, hawatatumia vibaya, hatawapoteza mkitaka kwenda kutafuta mkopo kwa tathimini yao Tanzania tunakopesheka,”amefafanua Kinana.

Kwa upande wake Dk. Kijaji wakati anaelezea utekelezaji wa Ilani Kondoa amempongeza Rais Samia kwa kuitazama kwa karibu Kondoa ambapo katika kipindi cha miaka miwili na nusu miradi ya maendeleo imepelekwa katika sekta mbalimbali na hiyo ni kutekeleza ahadi ya Chama Cha Mapinduzi kupitia Ilani yake ya Uchaguzi.

Amesisitiza kwamba anatoa shukrani kwa Serikali chini ya uongozi thabiti wa Dk.Samia kwa kutekeleza kwa vitendo na kwa ufanisi mkubwa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 .

“Kwa wananchi wetu wa Jimbo la Kondoa kila mmoja wetu anaona kwa macho miradi mingi ya maendeleo inayotekelezwa.

By Jamhuri