Dar-es-Salaam copyHayawi, hayawi hatimaye yamekuwa. Wiki hii ndiyo ya mwisho kwa tambo, vijembe na kila aina ya mbwembwe za wagombea na vyama vya siasa vinavyoshindana kushika mamlaka ya kuongoza dola.

Wakati hii ikiwa ni lala salama, nafasi kubwa ya ushindani ipo kwa miamba miwili-Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia (Chadema) kinachowakilisha Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Kampeni zinatarajiwa kufikia tamati Jumamosi wiki hii, Oktoba 24. Upigaji kura utafanyika kwa siku moja, Jumapili Oktoba 25.

Kila upande umekuwa ukitamba kuibuka na ushindi wa kishindo katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu, lakini duru za kiasiasa tangu kampeni zianze rasmi Agosti 2, mwaka huu zinaonyesha kuwa mchuano kati ya CCM na Chadema (Ukawa) ni hautoi nafasi kwa mshindi kuibuka na kura za kishindo.

Hayo yakiwa kwa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa upande wa nafasi kama hiyo kwa Zanzibar, nako mchuano mkali ni kati ya mgombea wa CCM, Dk. Ali Mohamed Shein, na mwenzake wa Chama cha Wananchi (CUF), anayeungwa mkono na Ukawa, Maalim Seif Sharif Hamad.

Mikoa tisa ndiyo inayoweza kuamua mshindi wa urais. Ukiacha Mkoa wa Dar es Salaam wenye wapigakura zaidi ya milioni 2, mikoa mingine minane ina wapigakura zaidi ya milioni moja kila mkoa. Mikoa hiyo ni Arusha, Dodoma, Kagera, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Tabora na Tanga. Orodha ya idadi ya wapigakura kama ilivyotolewa na Tume ya Uchaguzi ya Taifa (NEC) imeambatanishwa kwenye habari hii.

Mgombea urais kupitia CCM, Dk. John Magufuli, amenukuliwa akisema ushindi kwa chama chake ni jambo lililo wazi, kwani amefanya mikutano nchini kote na kuwavutia wapigakura kwa sera na ahadi kama zilivyoainishwa kwenye Ilani ya Uchaguzi ya chama hicho kwa mwaka 2015-2020.

Dk. Magufuli, amekuwa akiwataka wananchi wamchague kwa ahadi kuwa amenuia kuifanya Tanzania iwe na mabadiliko ya kweli yenye tija kwa Watanzania wote.

Hadi Oktoba 10, 2015, Dk. Magufuli, alikuwa amekwishatembelea mikoa 22 na majimbo 203 na kufanya mikutano mikubwa rasmi 240 na mikutano 865 ya kusimamishwa na wananchi njiani, hasa wananchi wa vijijini.

Dk. Magufuli amekuwa akitumia usafiri wa barabarani, ambako hadi tarehe hiyo alikuwa ametembea kilometa 31,467 kwa barabara kuu, barabara za mikoa, barabara za wilaya, barabara za mlisho na barabara za mijini na vijijini.

“Watu wengi wamekuwa wanajitokeza kwenye mikutano yetu. Lakini la muhimu zaidi ni hamasa na matumaini wanayopata baada ya kumuona jukwaani na kumsikiliza Dk. Magufuli. Wananchi wanapoondoka kwenye mikutano yetu ya kampeni wanakuwa wamepata fursa ya kumsikia mgombea wetu kwa kitambo kinachotosheleza, wamemwelewa, wameelewa sera za CCM na wameshawishika kukipigia kura Chama Cha Mapinduzi,” wametamba CCM.

CCM wanasema tangu kampeni zianze hadi sasa, ushindi wa chama hicho unajidhihirisha. Hata hivyo, katika kujihakikishia ushindi na kuongeza kiwango cha ushindi, katika ngwe ya mwisho, CCM wameanza kampeni nzito kwa kuwahusisha Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, aliyeanza ziara ya kampeni katika majimbo 64.

Rais na Mwenyekiti wa CCM Mstaafu, Mzee Benjamin William Mkapa, naye ameanza safari za kuzunguka nchi nzima kumwongezea kura Dk. Magufuli na wagombea wetu wa Ubunge na Udiwani.

Kwenye mkakati huu wa lala salama CCM wameamua kutumia helikopta nne, lakini mgombea na mgombea mwenza wao wataendelea kutumia magari hadi mwisho wa kampeni ambao ni Jumapili ya wiki hii.

Kwa kuona ushindi uko dhahiri, CCM na mgombea wake wa urais wameshaanza maandalizi ya kile wanachokiita “Kuleta Mabadiliko ya Haraka na ya Kweli.”

Dk. John Magufuli, ameshaunda jopo la wana taaluma na wataalamu huru magwiji wazalendo wa uchumi, biashara, utawala na sheria, kutoka kwenye taasisi za elimu ya juu, asasi zisizo za kiraia, na sekta binafsi, kwa ajili ya maandalizi ya kufanya mabadiliko makubwa serikalini.

Jopo hilo lina kazi zifuatazo:

1: Kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo Serikali itabana matumizi, ikiwamo ununuzi wa umma, posho za vikao na matumizi ya magari, ili atoe uamuzi kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa.

2: Kuchunguza na kupendekeza maeneo ambayo Serikali itaongeza mapato mara moja bila hatua za kibajeti kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa.

3: Kuchunguza na kupendekeza maboresho makubwa katika mfumo wa utendaji na utumishi na ufanisi katika Serikali.

4: Kupitia kodi na ushuru wenye usumbufu kwa wafanyabiashara wa ngazi zote, wakulima, wafugaji na wavuvi iwapo unaweza kurekebishwa bila kuathiri bajeti ya Serikali inayotekelezwa sasa.

5: Kupitia sheria zote za nchi na kuorodhesha sheria ambazo zinapaswa kubadilishwa haraka ili kuharakisha mabadiliko ya kweli na ya haraka ambayo ameyaahidi kwa Watanzania.

6: Kupitia na kuorodhesha masuala yote na kero zote zinazosubiri maamuzi ya Serikali ili atoe maamuzi kuanzia siku ya kwanza atakapoapishwa.

7: Kupendekeza miundo na idadi ya Wizara na kutengeneza rasimu za mikataba ya kazi kwa Mawaziri, Makatibu Wakuu na watendaji wengine wakuu atakaowateua mara baada ya kuapishwa.

8: Kupendekeza njia za haraka za kumaliza kero za watumishi wa umma, hasa walimu, askari, madaktari na wauguzi, ili aanze nao kazi wakiwa na ari na morali ya kusukuma mabadiliko ya kweli.

9: Kutengeneza rasimu ya mpango-kazi wa utekelezaji wa Ilani ya CCM na ahadi alizozitoa kwenye kampeni, hasa upatikanaji wa ajira kwa haraka na umeme wa uhakika.

10. Kupendekeza muundo wa kitaasisi na utaratibu muafaka wa kutekeleza ahadi ya kutoa Sh milioni 50 kwa kila kijiji na mtaa nchini.

“Dk. Magufuli ameazimia kuanza kazi mara moja kwa bidii kubwa na maarifa mapya,” wametamba CCM.

Dk. Magufuli, amewekea mkazo kwenye suala la ujenzi na kufufua viwanda ili kuongeza ajira kwa maelfu ya vijana wa Tanzania.

Ilani ya CCM kwa upande huo inasema katika kipindi cha 2015 -2020, Serikali ya CCM itajenga viwanda mama na kuimarisha viwanda vilivyopo kwa kuhakikisha kwamba:

1: Ifikapo 2020, mchango wa sekta ya viwanda katika Pato la Taifa unaongezeka toka asilimia 9.9 za sasa hadi asilimia 15, na sekta hiyo inachangia asilimia 40 ya ajirza zote nchini.

2: Tutatekeleza mpango thabiti wa kuhamasisha sekta binafsi kuanzisha viwanda vikubwa na vya kati na kuweka utaratibu wa kuvilinda dhidi ya bidhaa zisizo na ubora zinazoingizwa nchini kinyume na utaratibu.

3: Tutajenga mazingira rafiki yatakayowezesha kupunguza gharama za uwekezaji na uendeshaji wa viwanda.

4: Tutaanzisha viwanda vya msingi vinavyotumia malighafi ya chuma na makaa katika maeneo ya Liganga na Mchumchuma.

“Tutaendeleza kasi ya ujenzi wa viwanda vidogo na vya kati hasa vinavyosindika mazao na kuhakikisha Benki ya Rasilimali (TIB) inapanua wigo wake ili kutoa huduma katika maeneo yote nchini ikiwemo Zanzibar,” inasema Ilani hiyo.

Kwa upande wake, mgombea wa Chadema, Edward Lowassa, amekuwa akiwahakikishia wananchi kuwa huu ni wakati wa mabadiliko, na kwamba kumchagua yeye na wagombea wengine wanaotokana na Ukawa kutawafanya Watanzania waondokane na jinamizi la kukosa maendeleo kwa muda mrefu.

 Chadema/Ukawa wanasema historia inaonyesha kuwa vyama vikongwe barani Afrika vimeanguka kutokana na sababu mbalimbali hasa kukithiri kwa umasikini na ukosefu wa ajira; ajira za upendeleo; kukua kwa matabaka hasimu kwenye jamii; rushwa, ufisadi,

ubadhirifu na matumizi ya anasa serikalini.

“CHADEMA inatambua sababu kuu nne zilizosabisha nchi yetu ifike katika umaskini uliokithiri wakati inazo rasilimali za kutosha. Sababu hizo ni:

1: Ukosefu wa katiba ya wananchi ambayo ingewapa

mamlaka ya kuwadhibiti watawala.

2: Ukosefu wa uongozi wenye uzalendo, uadilifu na utawala bora ambao umepelekea uzembe na kutowajibika; na kukithiri kwa ufisadi na ubadhirifu wa mali ya umma.

3: Kufanya uchumi utumikie siasa badala ya siasa kutumikia uchumi – kupuuza ushauri wa kitaalamu katika sera, mipango na utekelezaji.

4: Ukiritimba wa madaraka wa chama kimoja.

 “Viashiria vinaonyesha kwa kiasi kikubwa kuwa tayari serikali ya CCM ni dola inayoanguka. CHADEMA na UKAWA wanadhamiria kuunda serikali itakayoondoa mambo yote hayo ili kujenga upya Taifa imara kwa manufaa ya Watanzania wote.

“Lengo kuu kwa ujumla katika ilani hii, ni kuhuisha uzalendo, uadilifu na uwajibikaji katika uongozi wa nchi ambao ndio msingi mama wa kuleta maendeleo ya jamii ya Watanzania. Ili tuweze kutoka hapa tulipo tunahitaji uongozi utakaozingatia yafuatayo ambayo ndiyo msingi wa Ilani ya Chadema:

1: Kuimarisha amani, umoja na mshikamano wa Taifa

2: Kuleta Katiba ya Wananchi inayosimamia haki na

usawa

3: Kujenga Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa

misingi ya usawa

4: Kuleta fikra ya Watanzania kujiamini na kujitegemea

kama Taifa huru

5: Kuimarisha Uzalendo na Uadilifu

6: Kujenga Uchumi shirikishi unaolenga kuondoa umaskini

7: Kuimarisha Huduma za Jamii

8:  Kuwajengea mazingira mazuri na kuwapa kipaumbele walemavu katika sekta zote

9: Kujenga Utendaji bora na Uwajibikaji katika sekta ya

Umma

10: Kujenga Ushirikiano wa karibu baina ya Serikali na sekta binafsi

11: Kudumisha na kuendeleza uhuru wa mawazo, uhuru wa kutoa na kupata habari na kujumuika na watu

wengine

12: Ulinzi thabiti na usalama wa raia.

13:  Ushirikiano wa Kimataifa wenye tija na Ujirani mwema.

“Ni dhamira ya CHADEMA na UKAWA kuunda serikali makini, adilifu na inayowajibika kwa umma, katika kuendeleza falsafa ya CHADEMA msingi wa juhudi zote za maendeleo za uchumi na kijamii zitalenga kwenye kuondoa umaskini na kuelekea

kwenye taifa la uchumi wa kati na hatimaye lililoendelea,” wanasema Chadema.

1477 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!