kingunge-ngombale-mwiru-2-1Wakati Tanzania na dunia nzima inaadhimisha miaka 16 bila ya kuwa mwasisi wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, mwanasiasa mkongwe nchini, Kingunge Ngombale-Mwiru, ametoa siri za hisia za siasa za Baba wa Taifa.

Kingunge, ambaye amehudumu nchini kuanzia chama TANU na baadaye CCM na kwa jumla yake ametumikia vyama hivyo kwa miaka 61, anasema kama Mwalimu Nyerere angekuwa hai, basi angejitoa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kama alivyofanya yeye wiki iliyopita.

Akizungumza na JAMHURI katika mahojiano maalum, Kingunge, ambaye wiki iliyopita alijitoa CCM, anasema kwa hali ilivyo kwa sasa ndani ya CCM anashangazwa na baadhi ya wanachama wenye nia ya mabadiliko kuendelea kubaki huko.

“Tena nadhani Nyerere angeenda mbali zaidi, yeye angetangaza kujitoa na moja kwa moja anajiunga na chama gani… ila mimi nimesema sitajiunga na chama chochote, lakini ni mtu ambaye nataka mabadiliko,” anasema Kingunge.

Kingunge anasema kuwa wakati wa uhai wake, Mwalimu Nyerere alijua kuwa ingetokea siku angejitoa CCM kwa sababu ya dalili za kukiuka misingi yake ya kutetea wanyonge hasa wakulima na wafanyakazi.

Badala yake, CCM ilianza kukumbatia na bado inakumbatia wafanyabiashara, hivyo aliona wazi kuwa kulikuwa na uwezekano wa kujitoa na ndiyo msingi wa kutamka “Naweza kujitoa.”

“Madhara ya kukumbatia wafanyabiashara ni kushamiri wa rushwa, hivyo wale mliopanga kuwatetea hamuezi tena kuwatetea, ndiyo maana unaona wakulima wanalia, walimu wanalia, madaktari wanalia. 

“Sasa nchi inahitaji mabadiliko. Turudi kwenye misingi yetu, lakini CCM haina sera. Ndiyo maana nikasema CCM imechoka na ipishe wengine,” anasema Kingunge na kuongeza kwa kukiuka taratibu na Katiba ya CCM kukiukwa, na hivyo ingekuwa vigumu kwa mwasisi huyo kubaki.

“Tulipotoka vitani, ile Vita ya Kagera, hali ya uchumi haikuwa nzuri. Wazungu wakaanza kumnyanyasa na kumtoa kwenye siasa alizoamini za Ujamaa na Kujitegemea.

“Ilipofika mwaka 1985, akaona haiwezekani. Mambo yamekuwa magumu. Ujamaa unaondoka na watu wanataka mambo ya utandawazi. Walikuwa na Azimio lao, akaona hapana. Akang’atuka.

“Sasa hivi kwenye chama ambacho mimi nimejitoa, Nyerere aliona haya mapema kuwa chama kimepoteza dira na mwelekeo. Katiba haifuatwi, taratibu na kanuni zinakiukwa, angesema hapana. Naamini angejitoa,” anasema Kingunge.

Mwanasiasa huyo ambaye tayari ameanza kupanda jukwaa la Ukawa kumnadi Edward Lowassa – akisisitiza mabadiliko kwa sasa hayaepukiki na kwamba huu ndiyo mwisho wa CCM anayoijua yeye.

Anasema kujitoa kwake ni kumuenzi Mwalimu kwa matendo badala ya kauli huku umejifungia CCM.

Kingunge anasema Mwalimu Nyerere angekuwa wa kwanza kutoka kabla hata ya Lowassa aliyejitoa sambamba na Frederick Sumaye, mbali ya makada wengine wa CCM ambao wamekwenda Ukawa.

Anasema kwamba wanaoifahamu vyema CCM, hawawezi kubaki kwenye chama hicho, hivyo ni sahihi wale waliotangulia kutoka akiwamo aliyekuwa Mwenyekiti wa Singida, Mgana Msindai, akitumikia wadhifa huo sambamba na cheo cha mwenyekiti wa wenyeviti.

Makada wengine ambao Kingunge aliwataja kuwa wanamuenzi Mwalimu ni pamoja na aliyekuwa Mwenyekiti wa Shinyanga, Khamis Mgeja, na Mwenyekiti wa zamani wa Dar es Salaam, John Guninita, na mawaziri wa zamani, Dk. Makongoro Mahanga (Segerea), na Goodluck ole Medeye (Arumeru).

Anasema, tena hata juhudi za kumkata Lowassa kinyume cha taratibu Julai mwaka huu huko Dodoma, ni mbinu za Mwenyekiti wa sasa wa CCM, Jakaya Kikwete, kuogopa chama kumfia mikononi.

“Safari hii chama kinamfia,” anasema Kingunge na kuongeza akisema Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa walijitahidi kwa kiasi chao kuendeleza umoja, lakini kwa mgawanyiko ulioko CCM kwa sasa “chama hiki hakina maisha marefu. Hii ni kwa sababu kimechoka.”

Katika mahojiano hayo, Kingunge alikumbusha mambo mawili ambayo Mwalimu Nyerere alionesha kuichoka CCM kuwa ni wakati wa hafla ya kumuaga Rashidi Mfaume Kawawa, aliyekuwa anastaafu siasa za majukwaani.

Anasema kwamba siku hiyo, Mwalimu Nyerere alishangazwa na hotuba ya rafiki yake – Kawawa, aliyesema: “Naahidi nitakufa nikiwa mwanachama mwaminifu wa CCM.”

Kingunge akinukuu maneno hayo anasema, “Sasa Mwalimu akamwangalia Kawawa na alipopanda kwenye ile podium (meza ya kutolea hotoba) naye ili azungumze, akasema:

“Rashidi una roho ngumu. Utakufa mwanachama mwaminifu wa CCM? Mimi siwezi kuyasema haya. CCM inaweza kubadilika. Siku ikiacha misingi, nami naachana nayo, kwa sababu CCM si mama yangu. Ninaye mama mmoja na siwezi kupata mwingine…”

Kutokana na hoja hiyo, Kingunge akasema, “Sasa mimi nibaki kufanya nini kwenye chama kilichoishiwa pumzi. Kama nilivyosema inafika mahala pumzi inakwisha. Huwezi kuendelea mbele na ukitaka kuendelea wananchi watabaki palepale walipo,” anasema.

Kwa kuwa CCM imekiuka taratibu zake, imekuwa ni shida kwa Watanzania ambao kwa sasa wanakabiliwa na changamoto za uchumi, ajira, umaskini usiomithilika.

Kadhalika, Kingunge alifuta maneno, miguno na hisia hasi kuhusu kauli ya Mwalimu Nyerere dhidi ya Lowassa, akisema ni upotoshaji kwamba mwasisi wa Taifa alimkataa mgombea huyo wa Ukawa.

“Si kweli kwamba Mwalimu alimkataa Lowassa. Hajawahi kutamka mahali popote pale kuhusu hilo.”

Kingunge anasema anakumbuka kuwa Mwalimu aliulizwa swali na waandishi kuhusu mtu anayefaa kuwa rais mwaka 1995, ambako pamoja na mambo mengine, aliwataja makada kadhaa akiwamo Lowassa.

Waliotajwa wakati huo ni Jaji Joseph Warioba, David Cleopa Msuya na Mark Bomani kwa upande wa wazee, na vijana aliwataja Mkapa, Rais wa sasa, Jakaya Kikwete, na Lowassa.

Anasema kwamba Nyerere alikiri kwamba Lowassa anao uwezo wa kujieleza na kugusa hisia za watu, na kwa asili yake ni mwanaharakati wa kweli kama yeye Kingunge anavyoamini.

Anasema kwamba hatua ya Chadema na Ukawa kwa ujumla kumpitisha Lowassa ni dhahiri kumeamsha siasa mpya na kwamba atamdhibiti na kumshinda mgombea wa CCM, John Pombe Magufuli.

Anasema kwamba ndani ya CCM kumejaa ukiritimba na ulevi mkubwa wa madaraka kiasi kwamba imefika hatua imebadili vionjo vyake vya salamu bila kujali demokrasia iliyoiasisi.

Na kutokana na uongozi wa sasa wa CCM, kuamua kukibinafsisha chama hicho na kufanya yale wanayotaka wao kwa maslahi ambayo Mzee Kingunge amedai hana hakika ni kwa maslahi ya nani na mambo yanafanyika ya ajabu, ameamua kujitoa.

Mzee Paul Ngwani

Gazeti hili lilizungumza pia na baadhi ya wazee na wasomi juu ya uwezo wa Mwalimu Nyerere kukemea wanasiasa na kama kuna mtu anayeweza kuwa kama yeye.

Kwa upande wake, Mzee Paul Ngwani wa Shinyanga, akizungumza na gazeti hili anasema: “Hakuna kama Nyerere. Kwa upande wangu niliona kwamba labda Warioba angeweza kufuata nyayo, lakini hawezi kuvaa viatu vya Mwalimu Nyerere.”

Mwandishi wa habari na kwa sasa mchambuzi huku akiwa anaandika vitabu, Yussuf Halimoja, anasema: “Sijaona kama Nyerere. Na sidhani kama atatokea mtu kama huyo ambaye ni rais pekee aliyekuwa ameshuka kwa watu.”

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia (Centre for Foreign Relations-CFR) kilichopo Kurasini, Dar es Salaam, Israel Sosthenes, anasema kwamba Mwalimu Nyerere atabaki kuwa alama ya uongozi bora katika historia ya Tanzania.

Sosthenes, aliyepata kuwa mtumishi katika Tume ya Usuluhishi na Uamuzi Tanzania, anasema kwamba Mwalimu Nyerere alikuwa kiongozi wa maridhiano yaliyomsukuma kutafuta si tu uhuru wa Tanzania, bali pia nchi nyingi za Afrika.

By Jamhuri