Na Mwamvua Mwinyi, JamhuriMedia,Pwani

Halmashauri tisa ,mkoani Pwani zinatarajia kunufaika na awamu ya pili ya mradi unaofadhiliwa na Korea Foundation For Health Care (KOFIH ),mradi ambao unaolenga kupunguza vifo vya uzazi kwa mama na mtoto mchanga.

Mradi huu unatarajia kutekelezwa katika kipindi cha miaka mitano na kugharimu takriban Bilioni 12 baada ya kukamilisha utekelezaji wa miaka Saba (2016-2022) .

Akizungumza wakati wa tathmini ya Mradi huo awamu ya kwanza (2016-2022) , Mkurugenzi wa huduma za afya ya uzazi na mtoto Wizara ya Afya Dkt.Ahmad Makuwani alieleza, mradi huo umetekelezwa katika Halmashauri sita ,vituo 19 chini ya Wizara ya afya na mkoa wa Pwani na uligharimu dollar za Kimarekani 5 milioni (USD).

Makuwani alisema, mradi umeleta matokeo chanya kwa kupunguza changamoto ya vifo vya uzazi na mtoto
,kwani kabla ya Mradi kulikuwa na vifo vya watoto 800 hadi Mradi unakamilika vifo vimefikia 390.

Kwa Upande wa vifo vya Mama ilikuwa vifo 82 na hadi mradi unamalizika vifo vimefikia 35.

Awali Mratibu wa afya ya uzazi na mtoto Kanda ya Mashariki na Mkoa wa Pwani ,Joyce Gordon alifafanua ,KOFIH imeongeza majengo ya uzazi ,mama na mtoto, kununua vifaa mbalimbali vya uzazi,vitanda,majokofu ya kuhifadhia damu,kujenga vyumba vya kufulia na kusomesha wataalam wa kutoa dawa za usingizi.

Alieleza, suala la kukosa usafiri ni moja ya chanzo kinachosababisha mama kufariki njiani wakikimbizwa kujifungua ,hivyo KOFIH wametoa magari ya wagonjwa matano Kibaha Mjini, Kibiti, Kisarawe,Mafia, Rufiji huko Mbwera wamepatiwa boti .

Nae Mjumbe Mwakilishi kutoka KOFIH Tobias Kyuong Kyun Oh alielezea,wanaanza mradi mwingine utakaotekelezwa kwa miaka mitano ijayo na mradi huo utagharimu takriban Bilioni 12 za kitanzania.

Kyun Oh alieleza ,mradi huu utanufaisha akinamama wote watakaokwenda kujifungua katika Halmashauri zote Tisa Mkoani Pwani.

“Tunaunga mkono juhudi za Serikali chini ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ambae anaonyesha Nia kubwa ya kupunguza changamoto ya vifo vya uzazi kwa mama na mtoto, na sisi tunaendelea kushirikiana na Serikali kuboresha huduma katika sekta ya afya”

Kwa Upande wake,mganga mkuu wa mkoa wa Pwani Dkt.Gunini Kamba alieleza,mkoa unaendelea kupunguza changamoto za uzazi na kuboresha huduma za kiafya.

Gunini aliwashukuru KOFIH kwa kushirikiana na mkoa kuboresha huduma na kupambana na kero zinazochangia kusababisha vifo hivyo.

By Jamhuri