Na Zulfa Mfinanga, JamhuriMedia ,Arusha

Ili kuhakikisha kodi ya Serikali inatozwa pasipokuacha mianya ya ukwepaji, Mamlaka ya Mapato nchini (TRA), imekuja na sheria ya kutoa kamisheni ya asilimia tatu kwa mtu atakayefanikisha kupatikana kwa kodi iliyokwepwa.

Akizungumza kwenye semina ya siku moja kwa waandishi wa habari Mkoa wa Arusha Afisa Uhusiano Mwandamizi wa TRA Rachel Mkundai alisema utaratibu huo upo kisheria hivyo kuwataka waandishi wa habari kutoa elimu hiyo kwa Umma ili waweze kushirikiana na TRA katika kuwabaini wakwepa kodi na wakati huo huo mtoa taarifa atajizolea asilimia tatu ya Kodi iliyokwepwa.

“Tunajua ninyi waandishi wa habari mna uwezo wa kuwafikia watu wengi na ndiyo maana tunawatumia katika shughuli zetu, hivyo naomba muwaambie wananchi kuhusu hili suala la kupata asimilia tatu ya kodi inayokwepwa, na asilimia hiyo isiwe imezidi shillingi milioni 20” alisema Mkundai.

Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha Eva Raphael

Awali akifungua semina hiyo Meneja wa TRA Mkoa wa Arusha Eva Raphael alisema licha ya mamlaka hiyo kuwa na jukumu la kukusanya kodi lakini pia ina wajibu wa kutoa elimu kwa walipa kodi na wadau wao kuhusu haki na wajibu wao pamoja na kuweka mifumo mizuri ya ulipaji wa kodi.

Katika hatua nyingine alisema kwa sasa sheria inamtaka kila mtanzania mwenye umri wa kuanzia miaka 18 kuwa na namba ya utambulisho ya mlipa kodi (TIN) hata kama siyo mfanyabiashara.

“Lengo la semina hii kukumbushana kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu kodi Ili kila mtanzania ajione anao wajibu wa kulipa Kodi kwa maendeleo ya Taifa lake, lakini pia nisisitize kuwa sheria ya kumtaka kila mtanzania aliyefikisha miaka 18 na kuendelea ni lazima awe na TIN na kutokuwa nayo ni kuvunja sheria” alisema Eva.

Naye Afisa Elimu na Mawasiliano Mwandamizi wa Mamlaka hiyo Mkoa wa Arusha Eugenia Mkumbo amesema kila mfanyabiashara ana wajibu wa kulipa kodi isipokuwa kwa wafanyabiashara ndogo ndogo wenye mauzo yasiyozidi kiasi cha shillingi milioni nne kwa mwaka.