Na Mwandishi Wetu,JamhuriMedia

IMEELEZWA kuwa kosa la mwanahabari limekuwa likichukuliwa kama kosa la taasisi ya habari na kusababisha madhara makubwa ya kufungwa kituo ama gazeti tofauti na ilivyo kwenye tasnia nyingine nchini.

Hayo yamesemwa na Deodatus Balile, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), wakati akizungumza kwenye Kipindi cha 360 cha Clouds Televisheni leo.

Balile amesema, kufanya kosa la mwandishi kuwa kosa la taasisi ya habari, kumesababisha madhara makubwa mpaka wengine kukosa ajira.

Amesema kosa atakalofanya mwandishi wa habari, linapaswa kuwa kosa la mwanahabari mwenyewe na sio taasisi anayoifanyia kazi

“Kosa la mwandishi mmoja, unafungia kituo ama gazeti? Kuna watu wengi wanaumia hapo. Yupo dereva ambaye wala hahusiki na habari iliyochapishwa,” amesema Balile.

Ametoa mfano wa daktari aliyemfumua nyuzi mgonjwa baada ya kushindwa kulipa Sh. 10,000 gharama za matibabu “huyu daktari, waziri hakumfukuza kazi, alimpeleka kwenye bodi ya madaktari na wao wakachukua hatua stahili.”

Amesema, iwapo Bodi ya Ithibati ya Habari itakuwa huru na kujumuisha wadau mbalimbali wa tasnia hiyo, itakuwa na ufanisi mkubwa na kujengea heshima Tashia hiyo.

Pia amesema, mchakato wa mabadiliko ya sheria kandamizi za habari nchini, haulengi upendeleo kwa wanahabari bali haki, wajibu na mazingira mazuri ya tasia hiyo.

“Mchakato wa mabadiliko haya, unalenga kuweka mipaka lakini pia uhuru wa habari bila kuumiza mtu yeyote. Tunalenga kupata uhuru zaidi wa habari na wajibu kwa mwanahabari.

“Tunapozungumzia uhuru wa vyombo vya habari, sio kwamba tunataka upendeleo kutoka serikalini, la! Tunacholenga hapo kila mmoja apate haki na awajibike,” amesema Balile.

Balile amesema ingawa wadau wa habari wanasimamia mabadiliko hayo, uhuru wa habari unawahusu hata wale wasio wanahabari.

Kwamba, nchi ambayo uhuru wa habari haupo, wananchi hukosa fursa ya kupata taarifa sahihi na hivyo kunyima haki yao ya msingi ya kuhabarika.

“Tufahamu kuwa uhuru wa habari ni haki ya msingi ambayo wengine wanaitaka. Vyombo vya habari visipokuwa huru, wananchi nao pia wanakosa uhuru ikiwa ni pamoja na kutoa maoni yao pia kupata taarifa zinazowahusu moja kwa moja,” amesema.

Ametoa mfano wa ajali iliyotokea Mtwara na kusababisha vifo vya wanafunzi wanane amesema, watu wamefahamu nini kimeendelea kutokana na ajali hiyo, lakini uhuru wa kutoa habari bado haujalindwa kisheria. Ndio maana tunataka haya ulindwe na sheria.

Amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kupitia sheria za habari na kuagiza zifanyiwe maboreshio ili kuendana na mazingira yaliyopo.

“Tulikutana na rais (Rais Samia) Ikulu na kwa kuanza, tulimuomba kuhamisha tasnia ya habari na kuipeleka kwenye Wizara ya Mawasiliano, tunashukuru amefanya hivyo.

“Tukasema sasa tutengeneze muingiliano mzuri wa sheria, na jambo zuri ni mchakato umeanza lakini siku za karibuni hapa umepoa, ” amesema.

Ametumia nafasi hiyo kumkumbusha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye kuongeza kasi ili kufikia matamanio ya wadau wa tasnia ya Habari.

By Jamhuri