Balozi Umoja wa Ulaya amtembelea Jaji Mkuu

Na Mary Gwera,JamhuriMedia

BALOZI wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) Tanzania, Manfredo Fanti amemtembelea Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma kwa lengo la kujifunza mambo mbalimbali ya utoaji haki nchini.

Akizungumza na Jaji Mkuu ofisini kwake katika jengo la Mahakama ya Rufani jijini Dar es Salaam, Balozi Fanti amesema kuwa dhumuni mojawapo la kuonana na Mkuu huyo wa Mhimili ni pamoja na kuangalia maeneo mbalimbali ya kushirikiana katika suala zima la kuboresha utoaji haki.

Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Mustapher Siyani (kushoto) akiwa na Balozi wa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) Tanzania, Mhe. Manfredo Fanti walipokutana ofisini kwa Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma

“Moja ya sababu ya kukutana na wewe leo ni pamoja na kufanya mazungumzo ili kufahamu malengo yenu kama Taasisi, changamoto mlizonazo pamoja na kujenga ushirikiano baina yetu,” amesema.

Ameongeza kuwa Umoja wa Nchi za Ulaya (EU) upo tayari kushirikiana na Mahakama ya Tanzania katika maeneo mbalimbali kwa lengo la kuboresha huduma za utoaji haki, hivyo ujio wake umelenga katika kubaini maeneo yenye changamoto yanayowakabili.

Kwa upande wake,Jaji Mkuu amemueleza Balozi huyo kuwa Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika uboreshaji wa huduma mbalimbali ikiwemo matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), miundombinu ya majengo ya Mahakama na uondoshaji wa mashauri.

“Mahakama ya Tanzania tumekuwa tukitekeleza Mpango Mkakati (2015/2016-2019/2020 na 2020/2021-2024/2025) pamoja na Mradi wa Maboresho wa Huduma za Mahakama unaofadhiliwa na Benki ya Dunia, yote ikiwa inalenga kuboresha zaidi huduma za Mahakama kwa wananchi,” amesema Prof. Juma.

Jaji Mkuu amesema kuwa matumizi ya TEHAMA yamesaidia katika kurahisisha shughuli mbalimbali za Mahakama, huku akitoa mfano kuwa wakati janga la Korona lilipoanza Mahakama haikusimamisha shughuli zake, bali iliendelea kusikiliza mashauri kwa njia ya Mkutano Mtandao ‘Video Conference’.

Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Prof. Elisante Ole Gabriel (kulia), pamoja na Makatibu wa viongozi wakuu wa Mahakama, Katibu wa Jaji Mkuu, Mhe. Venance Mlingi (kushoto) na Katibu wa Jaji Kiongozi, Mhe. Obadia Bwegoge (katikati) wakifuatilia mazungumzo kati ya Mhe. Prof. Juma na Balozi Fanti (hawapo kwenye picha)

Aidha, Mhe. Prof. Juma amemweleza Balozi huyo kuwa katika kushughulikia masuala ya familia na hususani haki za wanawake, wameamua kuanzisha Mahakama maalum iliyopo katika Wilaya ya Temeke kwa lengo la kushughulikia kwa karibu masuala hayo.

Ameongeza kuwa miongoni mwa vipaumbele ambavyo Mahakama inasisitiza katika kuangalia njia za haraka zaidi zitakazosaidia kupunguza mlundikano wa mashauri ni pamoja na kutumia Usuluhishi ‘mediation’, uanzishwaji wa Mahakama ndogo zitakazosaidia kusikiliza na kuamua mashauri ya kibiashara.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto) akimwonyesha Balozi  Fanti (kushoto) nakala moja ya jarida la Mahakama la Haki Bulletin, huku Siyani (wa pili kulia) na Prof. Ole Gabriel (kulia) wakishuhudia.

Hata hivyo, Jaji Mkuu amemueleza Balozi huyo kuwa ingawa Mahakama imepiga hatua katika uboreshaji wa huduma zake, bado kuna changamoto kadhaa ambazo inakabiliana nazo ikiwemo namna ya kufikisha huduma za utoaji haki kwa wananchi ambapo amefafanua kuwa baadhi ya maeneo kukosa majengo ya Mahakama au kuwa mbali na Mahakama.