Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Ugumu wa maisha, kuporomoka kwa bei ya tanzanite, kupanda bei kwa bidhaa na huduma mbalimbali, simanzi wilayani Hanang na matukio ya kupotea kwa watu mkoani Geita ni baadhi ya mambo yaliyoigubika Sikukuu ya Krismasi mwaka 2023.

Wakati hayo yakiendelea nchini Tanzania, Kanisa Katoliki linaloaminika kuwa ‘kanisa mama’ limesherehekea Krismasi ya mwaka huu huku likiwa limetikisika.

Waraka tata uliotolewa na Vatican Desemba 18, mwaka huu, ‘Fiducia Supplicans’, ukielekeza utaratibu mpya kwa mapadri kuwabariki hata wapenzi wa jinsia moja na wenza ambao hawapo kwenye ndoa, umezua mtafaruku wa aina yake duniani ukipokewa kwa hisia tofauti.

“Huenda waamini wa kawaida wasiwe na tatizo na waraka wa Vatican, lakini kwa namna unavyopingwa na mabaraza ya maaskofu katika mataifa mbalimbali, ni wazi kuwa kanisa limetikisika,” anasema padri mmoja wa Jimbo Katoliki Mpanda.

Mabaraza ya maaskofu ya Poland, Ghana, Nigeria, Cameroon na Malawi ni miongoni mwa mabaraza yaliyopingana waziwazi na msimamo mpya wa Vatican; kuthibitisha kwamba sherehe za Krismasi mwaka huu hazikuwa kama zilivyozoeleka.

LATRA lawamani gharama za huduma

Kwa upande mwingine, uamuzi wa Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (LATRA) unalaumiwa kwa kuongeza gharama za maisha baada ya kupandisha nauli ya mabasi ya masafa marefu na mafupi siku chache kabla ya Sikukuu ya Krismasi.

Akizungumza na JAMHURI, abiria aliyekuwa akielekea Moshi kwa usafiri wa Coaster, Frederick Urassa, anasema haikuwa sahihi kupandisha nauli Desemba.

“Kwa kwaida nauli huwa zinapanda zenyewe kila mwaka nyakati kama hizi. Sasa kwa nini LATRA wamepandisha? Si wangesubiri hadi Januari mwakani?” analalamika Urassa ambaye amelazimika kulipa Sh 60,000 kwenda Moshi.

Hali kama hiyo ipo pia katika maeneo mengine nchini ambapo wasafiri wanaokwenda Bukoba mkoani Kagera nao wamelazimika kuingiza mkono mfukoni baada ya nauli kupanda maradufu huku ‘booking’ za ndege zikiwa zimejaa hadi Januari mwakani.

Yote haya yanadhihirisha namna ambavyo Krismasi ya mwaka huu imekuwa tofauti na miaka mingine.

Katesh bado

Wakati hofu ya kuwapo kwa idadi kubwa ya watu waliofariki dunia kwa kufukiwa na matope huko Katesh, Hanang mkoani Manyara ikiwajaa wakazi wa huko wakati wa Sikukuu ya Krismasi, taratibu maisha yameanza kurudi katika hali ya kawaida.

JAMHURI limeelezwa kwamba zipo familia ambazo bado hazijui ndugu zao walipo na zimekuwa zikiiomba serikali kufanya tathmini yakinifu kufahamu idadi kamili ya waathirika wa mafuriko yaliyotokea Desemba 3, mwaka huu.

“Kuna bibi mmoja jirani yangu amepoteza ndugu zake wote Kata ya Gendabi. Siku ya tukio yaya alikuwa Katesh mjini ndiyo maana akanusurika. Lakini watoto wake na familia zao wamepotea,” anasema mkazi mmoja wa Katesh.

Kwa bibi huyo hakuna Krismasi na huenda isiwepo tena maishani mwake kwa kuwa sasa anaonekana kurukwa akili kutokana na tukio hilo.

Hata hivyo, waathirika waliokuwa wamewekwa kwenye kambi maalumu sasa wameruhusiwa kurejea kwa ndugu zao wakati mipango ya serikali kuwaandalia makazi mapya ikiendelea.

Bei ya tanzanite yaporomoka

Wadau: Tunguu kugumu kuingilika tofauti na Msoga, Chato

Hali ikiwa hivyo huku na kule wakati huu wa Sikuku ya Krismasi, wafanyabiashara wa vito wamedai kuwa kuporomoka kwa bei ya tanzanite kumeifanya Krismasi ya mwaka huu kuwa chungu.
JAMHURI limeelezwa kwamba bei ya tanzanite, vito vinavyopatikana Tanzania pekee, imeporomoka kutoka kati ya dola za Marekani 1,500 hadi 2,000 kwa karati hadi kufikia dola za Marekani 400 hadi 500 kwa karati.

“Hii ni hatari sana kwa mustakabali wa vito hivi na taifa letu kwa ujumla. Tumekuwa tukitafuta nafasi ya kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan tuzungumze naye kuona namna ya kunusuru soko la tanzanite duniani, lakini imekuwa vigumu kumpata,” anasema mmoja wa wafanyabiashara wa vito, Adolph Mpenza.

Inadaiwa kuwa kumekuwa na vizingiti vingi katika jitihada za wadau kumfikia Rais Samia tofauti na ilivyokuwa kwa watangulizi wake; Jakaya Kikwete na Dk. John Magufuli.

Miongoni mwa juhudi zilizofanywa na wadau hao ni kukutana na kufanya vikao na viongozi mbalimbali, akiwamo Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Doto Biteko.

Wadau wa biashara ya vito wanaamini kuna uwezekano wa kurejesha hadhi ya tanzanite kimataifa iwapo serikali itaamua, wakimwomba Rais kufuta agizo la serikali.

Sababu ya anguko la tanzanite

Agizo la serikali lililotolewa Januari 6, 2022 kwamba si ruhusa tanzanite kuuzwa sehemu nyingine yoyote nchini zaidi ya kule inakochimbwa, Mererani, Simanjiro mkoani Manyara, linatajwa kuwa sababu ya kudorora kwake.

“Ninaamini serikali haikupewa taarifa sahihi kuhusu biashara ya madini inavyofanyika. Thamani ya madini hutokana na upatikanaji wake.

“Ni falsafa potofu kuwa madini yakipotea sokoni ndiyo yanapanda bei. Hiyo ipo kwenye mazao tu, si madini hasa haya ya vito. Yakipotea sokoni, hushuka thamani,” anasema Mpenza.

Anasema utaratibu uliopo kwamba tanzanite iuzwe Mererani pekee unasababisha kuingizwa sokoni vito vingine mbadala kama ‘ruby’, ‘sapphire’ na ‘spinel spacetite’.

“Thamani ya tanzanite hutokana na uwepo wake kwenye soko la ndani ambapo wanunuzi wake wengi ni wageni (watalii). Wapo wanaonunua hapa hapa na wengine wanaagiza wapelekewe nje ya nchi,” anasema.

Awali Royal Tour iliibeba tanzanite

Wadau wengi wanakubaliana na ukweli kwamba juhudi za Rais Samia kutangaza utalii wa Tanzania kupitia filamu ya the Royal Tour zililibeba pia soko la tanzanite.

Katika mahojiano na JAMHURI, Mjumbe wa Chama cha Wauza Madini nchini (TAMIDA), Morris Hamad, amesema juhudi zilizoonyeshwa na Rais ni kama zinakwamishwa na serikali yake mwenyewe.
“Utalii umekua, kampuni zilizokufa zimefufuka na hoteli zinajaa wageni. Yote hii ni pamoja na Royal Tour. Lakini kwa tanzanite, hali ni tofauti. Ndiyo maana tunamwomba mama afute agizo la serikali ili kuiokoa sekta hii,” amesema Hamad.

Anasema agizo hilo limeua ajira kwa Watanzania wengi, kwa kuwa kibiashara tanzanite ikitoka nje ya ukuta wa Mererani baada ya kukatwa kodi, hutoa ajira kwa watu watano hadi 10.

“Mzunguko wa fedha umekuwa mdogo sana sasa na ndiyo maana utaona watu wanasema mwaka huu hakuna Krismasi. Ajira zimepotea. Sidhani kama serikali inapata mapato kama ilivyokuwa awali,” anasema.

Katibu Mkuu wa Chama cha Wenye Kampuni za Utalii (TATO), Cyril Ako, anaungana na Hamad akisema kuwa sekta ya utalii Krismasi imekwenda vizuri tofauti na upande wa tanzanite.
“Kwa miaka miwili mfululizo watalii wamemiminika na kuweka historia tangu tupate uhuru,” anasema Ako akikiri kwamba hana uzoefu na biashara ya vito.

Hali halisi Mererani

Wadau wa tanzanite wanaamini kuwa nia ya kuifanya Mererani kuwa ‘mji maalumu’ wa biashara ya tanzanite si mbaya, lakini ukweli ni kwamba miundombinu yake si rafiki kwa wanunuzi, hasa wageni na wafanyabiashara wa kimataifa.

Wanunuzi wa kimataifa ambao hufika Arusha, Dar es Salaam na Mwanza huomba wapelekewe madini huko huko waliko wakitambua kwamba Mererani bado haina miundombinu wezeshi ya hadhi ya hoteli za nyota tatu; huku barabara pia ikiwa ni tatizo jingine, achilia mbali usalama.

Mwenyekiti mstaafu wa TAMIDA, Sammy Mollel, anasema utaratibu wa uuzaji wa tanzanite unapaswa kuwa huru kama ilivyokuwa awali.

“Kitu cha msingi ni serikali kuhakikisha madini yote yanayotoka nje ya ukuta yawe yamelipiwa kodi, kisha mtu awe huru kuyapeleka kokote ndani ya Tanzania, na anapopeleka nje ya nchi, alipie ushuru stahiki. Hapo tutapandisha thamani ya madini yetu badala ya kuyafungia sehemu moja,” anasema Mollel.

Anashauri siasa isiingizwe kwenye biashara ya madini ili sekta hiyo iongeze mchango wake katika pato la taifa.

India, Rwanda, Kenya zanufaika na tanzanite

Mdau mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe, anadai kuwa tanzanite imeadimika nchini ilhali inapatikana kwa wingi katika maduka ya vito yaliyopo Kenya, Rwanda na India.

“Aina zote. Zilizonakshiwa na ambazo hazijanakshiwa ziko huko. Wafanyabiashara wa tanzanite Arusha wanakimbilia Kenya ambako wanafanyabiashara nzuri zaidi wakati sisi tumezuia,” anasema.

Anasema kuondoka nchini kwa wafanyabiashara wakubwa waliokuwa wanaingiza hadi Sh bilioni 10 kwa siku kwenye mzunguko wa soko la tanzanite ni hasara kwa taifa.

By Jamhuri