Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Dar es Salaam

MAMLAKA ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya ya Tanzania (DCEA) imekatama kilogramu 3,182 za dawa za kulevya aina ya heroin na methamphetamine ambazo zilikuwa zimefungashwa kwenye vifungashio vya bidhaa zenye chapa za kahawa na majani ya chai.

Pia imewakamata watu saba, wawili kati yao wana asili ya Asia wanaodaiwa kuwa ni miongoni mwa mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya inayofuatiliwa duniani.

Hayo yamebainishwa leo Desemba 27, 2023 jijini Dar es Salaam na Kamishina Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu operesheni maalumu iliyofanyika jijini humor na mkoani Iringa kati ya Desemba 5 hadi 23 mwaka huu.

Amesema kiasi hicho cha dawa za kulevya kinajumuisha kilogramu 2,180.29 za dawa aina ya Methamphetamine na Kilogramu 10001.71 aina ya heroin zilizokamatwa katika wilaya ya Kigamboni, Ubungo na kinondoni jijini Dar es salaam mkoani na Iringa.

“Ukamataji huu umehusisha kiasi kikubwa cha dawa za kulevya ambacho hakijawahi kukamatwa katika historia ya Tanzania tangu kuanza kwa shughuli za udhibiti wa dawa za kulevya”.amesema Kamishna Jenerali Lyimo.

Nakuongeza kuwa
“Watuhumiwa hawa waliokamatwa ni miongoni mwa mitandao mikubwa ya wauzaji wa dawa za kulevya inayofuatiliwa nchini na duniani”alisisitiza Kamishna Jenerali Lyimo

Amesema kuwa mbinu waliyotumia ya kuweka dawa za kulevya kwenye vifungashio vya bidhaa zenye chapa mbalimbali za kahawa na majani ya chai ni mbinu inayotumika kwa lengo la kurahisisha usafirishaji wake na kukwepa kubainika.

“Ukiacha dawa ya heroin inayotengenezwa kwa mchanganyiko wa kemikali kutoka kwenye mimea ya afyuni (opium popy) inayolimwa katika nchi za Asia na baadhi ya kutoka Amerika.

Alifafanua kuwa dawa aina ya Methamphetamine ni dawa mpya ya kulevya iliyopo katika kundi la vichangamshi sawa na cocaine.

Kamishna Jenerali Lyimo amesema dawa hiyo uwa kwenye mfumo wa vidonge, unga au chembechembe mithili ya chumvi ang’avu yenye rangi mbalimbali ambayo huzalishwa kwenye maabara bubu kwa kuchanganya aina mbalimbali za kemikali bashirifu.

“Dawa hii ni hatari kwa afya ya mtumiaji, madhara yake ni makubwa na hayatibiki kirahisi kwani mtumiaji hupata madhara ya kudumu kwenye ubongo na hivyo hupunguza uwezo wa kutunza kumbukumbu, kusababisha uraibu na kuathiri mfumo mzima wa ufahamu”amesema.

Aidha amesema kiasi cha dawa za kulevya zilizokamatwa , endapo zingefanikiwa kuingia mtaani zingeweza kuathiri zaidi ya watu 76,368,000 kwa siku.

“Ukamataji huu umeokoa nguvu kazi ambayo ingeangamizwa kutokana na madhara yatokanayo na matumizi ya dawa za kulevya ndani na nje ya nchi”amesema

Kamishna Jenerali Lyimo alitoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na DCEA kwani mafanikio hayo yametokana na ushirikiano unaotokana na wananchi wanaotoa taarifa kuhusu watu wanaojihusisha na biashara ya dawa za kulevya ikiwa ni pamoja na weledi na uzalendo mkubwa na maafisa DCEA katika kudhibiti biashara ya dawa za kulevya.

Pia alitoa onyo kwa watu wote wanaoendelea kujiusisha na biashara ya dawa za kulevya hapa nchini kuacha badala yake wajikite kwenye biashara nyingine halali kwani DCEA imejizatiti kukomesha biashara ya dawa za kulevya kwa kufanya operesheni katika maeneo mbalimbali nchini.

Katika hatua nyingine Kamishna Jenerali Lyimo aliishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuiwezesha DCEA katika kutekeleza kazi zake ufanisi mkubwa.

By Jamhuri