MOMBASA

Na Dukule Injeni

Wagombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa Kenya unaotarajiwa kufanyika Agosti 9, mwaka huu wamepewa hadi Jumatatu ya Mei 16 wawe wameshawasilisha majina ya wagombea wenza Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC). 

Licha ya msururu wa watu kujitokeza kuwania urais wakisubiri kupitishwa na IEBC, ni wawili tu ambao wanatajwa kuwa na mvuto; Naibu Rais William Ruto na aliyekuwa Waziri Mkuu, Raila Odinga. 

Ruto atawania urais kupitia Chama cha United Democratic Alliance (UDA) ambacho kipo ndani ya muungano wa Kenya Kwanza wakati Raila ambaye ni kinara wa Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) atapeperusha bendera ya muungano wa Azimio la Umoja One Kenya. 

Wanasiasa hawa wawili wanasubiriwa kwa hamu kuwataja wagombea wenza, jambo ambalo linaweza kubadili upepo katika mbio za kumrithi Rais Uhuru Kenyatta atakayekuwa anamaliza muda wake wa uongozi. 

Tayari Rais Kenyatta aliyeingia madarakani kupitia Chama cha Jubilee amekwisha kutangaza kumuunga mkono Raila na kwa siku za hivi karibuni cheche za maneno zimetawala kati ya Rais Kenyatta na Naibu Rais Ruto. 

Tofauti kati ya hao wawili ilianza kuibuka baada ya tukio la Machi 9, 2018 maarufu kama ‘handshake’ baina ya Kenyatta na Raila huku Ruto akidai kutengwa japo Rais Kenyatta mara kadhaa amekuwa akisisitiza kumhusisha katika kila hatua ya mazungumzo yake na Raila, lengo likiwa ni kuleta amani ili kuepuka machafuko ya kisiasa kufuatia marudio ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2017. 

Ukaribu wa Kenyatta na Raila ulimfanya Ruto ahisi kukosa sapoti ya bosi wake kuelekea Uchaguzi Mkuu, hivyo kusaka njia atakayotumia kuingia Ikulu kwa kubuni Chama cha UDA. 

Naibu Rais Ruto anatafuta mgombea mwenza kama tu ilivyo kwa Raila, na wanasiasa hawa wawili ni kama vile wanategeana kwa hofu ya kuibua manung’uniko ndani ya kambi zao kutokana na uamuzi utakaofanywa. 

Wanachoangalia zaidi katika uteuzi wa mgombea mwenza ni utashi wa mtu mwenye tajiriba ya hali ya juu anayekubaliwa kwa urahisi na kundi kubwa la watu. 

Aidha, wanasaka mgombea mwenza mwenye mvuto na aina fulani ya watu wanaomkubali mfano kama watahitaji kura za kina mama na wanawake kwa ujumla itabidi darubini ielekezwe kwa mgombea mwenza mwanamke. 

Mgombea urais wa Azimio la Umoja One Kenya, Raila, ameteua jopo la kuwapiga msasa wanaowania kuwa wagombea wenza linaloongozwa na waziri wa zamani, Dk. Noah Wekesa, ambapo imepitisha watu saba kati ya 20 waliopendekezwa na vyama tanzu ndani ya muungano huo. 

Saba hao ni Kalonzo Musyoka aliyependekezwa na chama chake cha Wiper, Chama cha Jubilee cha Rais Kenyatta kimewapendekeza Sabina Chege na Peter Kenneth, huku kinara wa Narc Kenya, Martha Karua, akipendekezwa na chama chake.

Wengine waliopitishwa kuwania ugombea wenza ni Mwenyekiti wa KANU, Gideon Moi, aliyependekezwa na chama chake, Hassan Joho akipendekezwa na ODM huku National Liberal Party ikimpendekeza Stephen Tarus. 

Nao Kenya Kwanza kupitia mkuu wa kampeni, Josephat Nanok, amesema kinara wa UDA – Naibu Rais Ruto, tayari anaye mgombea mwenza atakayemtaja kabla ya Mei 16 na hawahitaji kubuni jopo la kusaka mwenye sifa ya nafasi hiyo. 

Hata hivyo wanaotajwa ni Spika wa Bunge la Taifa, Justin Muturi; Seneta wa Tharaka Nithi, Profesa Kithure Kindiki; Mbunge wa Mathira, Rigathi Gachagua; kiongozi wa Chama cha ANC, Musalia Mudavadi; Senata wa Bungoma, Moses Wetangula; Mbunge wa Kiharu, Ndindi Nyoro na Gavana wa Kirinyaga, Ann Waiguru. 

By Jamhuri