NA BASHIR YAKUB 

Si siri, wengi waliowekeza kwenye biashara ya Bajaj, Bodaboda, teksi na hata daladala wamejuta kufanya hivyo. Wengi wameingia hasara na mambo hayakuwa kama walivyotarajia. 

Na niamini, waliomo leo kwenye hiyo biashara si wale walioanza, bali ni wageni, kwani walioanza walikwishaacha siku nyingi kuepuka kichwa kuuma.

Sasa yafaa tuzingatie mambo kadhaa ya kisheria ili kuona namna gani unaweza kudhibiti biashara hii na hata ikikushinda isikushinde ukiwa mwenye kupoteza (loser). Katika kufanya hivyo tutazame mambo mawili; kwanza, mkataba. Pili, udhamini.

  1. 1. Mkataba

Eneo la mkataba au makubaliano ni eneo muhimu sana tangu unapowaza biashara hii. Mkataba ndiyo tafsiri ya uhusiano wako na huyo unayemkabidhi chombo. 

Popote na wakati wowote mtakapotofautiana rejea yenu ya kwanza ni mkataba. Mkataba ndio biashara yenyewe, na hivyo uimara wa mkataba utatambulisha uimara wa biashara. Halikadhalika udhaifu wa mkataba huenda ukawa ndio udhaifu wa biashara.

Uimara wa mkataba ni sehemu kuu mbili. Kwanza, mfumo. Pili, maudhui/vipengele. Mfumo ni lazima mkataba uwe katika muundo mzuri wa sheria. Kifungu cha 10 cha Sheria ya Mikataba, Sura ya 345 kinasema mkataba  mzuri ni ule ambao umefanywa na watu stahili kufanya mkataba (parties’ competence), wenye hiari huru (free consent), wakibadilishana vitu halali (lawful object and consideration), na kile wanachokubaliana kiwe hakijakatazwa na sheria nyingine yoyote. Kwa hiyo mfumo mzuri wa mkataba utategemea haya.

Upande wa pili tumesema ni upande wa maudhui/vipengele. Hapa tunazungumzia masharti (conditions/terms). Haya ni yale ambayo mnataka yatekelezwe. 

Hapa napo ni sehemu muhimu sana kwa sababu panabeba lipi litakuwa likifanyika na lipi hapana. Hapa ndipo patakaposema hesabu ni kiasi gani, italetwa kila baada ya muda gani, nani atakabidhiwa, endapo isipoletwa kabisa au ikaletwa nje ya muda nini kitokee, chombo kitatunzwa vipi, nani atabeba uharibifu ndani ya chombo, kesi ya kuibiwa au kupotea inakubalika kwa misingi ipi, nani atabeba hasara hiyo, endapo dereva akipotea nani atafutwe kwa niaba yake nk.

Hii ni sehemu huru ambayo  mipaka yake ni pale litakapoingizwa sharti lolote la kuvunja sheria nyingine ya Tanzania. Kama halipo, mtaweka sharti lolote na mbingu ndiyo itakuwa mpaka (sky is the limit).

2.   Udhamini 

Kwa dhati kabisa kama mtu anahitaji ajira/kazi kwenye chombo chako hakikisha anayemdhamini.  Alete mdhamini na kama hana atafute kazi kwingine asikutie kwenye majaribu. Sehemu ya VIII ya Sheria ya Mikataba, Sura ya 345 imeeleza habari ya udhamini na kufidia hasara (indemnity). Mdhamini ni mtu wa lazima kwenye makubaliano ya aina hii, hasa kwa namna biashara hii inavyoumiza kichwa. 

Kutakuwa na mikataba miwili, mmoja kati yako mwenye chombo na dereva. Wa pili ni kati yako mwenye chombo na mdhamini. Dereva ataleta mdhamini wake na wewe kazi yako itakuwa ni kumtathmini (asses) kama anafaa au hapana.

Aidha, mkataba wako  na mdhamini utaeleza wazi kuwa mdhamini atabeba hatia yote (full liability)  ya dereva pale ambapo kutatokea hasara, na/au dereva akapotea, na/au akapatikana lakini akawa hana uwezo  wa kufidia hasara nk.

Mdhamini awe ni mtu wa kuaminika, mwenye makazi yanayotambulika, na awe mtu ambaye kweli anaweza kubanwa akafidia endapo litatokea la kutokea.

Aidha, mdhamini si lazima awe mtu wa tatu (third party). Hata dereva mwenyewe anaweza kujidhamini ikiwa atakubali kuweka rehani mali yake yoyote isiyohamishika au inayohamishika ambayo utakuwa na uhakika kuwa italinda chombo chako. Huu ni utaratibu ambao umekuwa ukitumiwa na taasisi za fedha kuhakikisha kwamba haziingii hasara.  Na sisi wajasiriamali  wa hii biashara tukiuasili (adopt) utaratibu huu, tukautumia, hakika utasaidia na hatutaingia hasara. Utapata usingizi, na utaepuka kurudishwa nyuma na watu ambao bado wako kwenye mchezo mchezo, ambao bado hawako makini (serious) na maisha.    

Kwa machache haya niseme kuwa kuna umuhimu wa kuyatilia maanani yaliyosemwa humu ili tukomeshe tabia ya kurudishana nyuma. 

Wale ambao tayari wameingia makubaliano lakini hawakufanya hivi bado hawajachelewa, wanaweza kuitisha makubaliano mapya. Na wale ambao wanatarajia kuingia kwenye hii biashara, itakuwa vema kwao walau wakifuata utaratibu huu.

Niseme tu kuwa biashara hii ni nzuri, yenye faida, ila taswira yake imeharibiwa na madereva walio wengi.

By Jamhuri