Mamlaka ya Udhibiti wa usafiri Ardhini (LATRA), imetangaza nauli mpya za mabasi ya Mwendo kasi yanayofanya kazi zake jijini Dar es Salaam huku ikijiandaa kupanga nauli za treni ya mwendokasi (SGR)

Akitangaza nauli hizo mbele ya waandishi wa habari jana jijini Dodoma, Mkurugenzi Mkuu wa (LATRA) CPA. Habibu Suluo amesema nauli hizo zimeongezeka kwa Sh.100 kutoka nauli za zamani.

CPA Suluo amesema mabadiliko hayo ni kwa mujibu wa sheria na yamepitishwa na bodi ya Wakurugenzi baada ya kupokea maoni kuhusu nauli katika maeneo hayo.

Suluo amesema nauli ya mabasi ya mwendokasi kwa njia kuu (truck route) ni Sh.750 kutoka Sh.600, njia ya mlisho (feeder router) ni Sh.500 kutoka Sh.400, njia ya mlisho na njia kuu (feeder +truck route) ni Sh.900 kutoka 800 na njia ya kimara kwenda Kibaha ni Sh700 badala ya pendekezo la DART la Sh.1,200.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (LATRA) CPA.Habibu Suluo,akifafanua jambo wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma.

“Mapendekezo haya ni kwa mujibu wa sheria lakini kama kuna mdau yeyote ana malalamiko au hakubaliani na haya alete malalamiko yake ndani ya siku 14 kutoka leo,” amesema CPA Suluo.

Kwa upande wa nauli za teksi mtandao zinazobeba abiria wanne nauli itakuwa Sh.3,000 hadi 4,000 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama kuna safari nyingine toka hapo nauli itaongezeka kwa Sh.800 hadi 1,000 kwa kilomita moja na safari inapokutana na vikwazo kama foleni nauli ya ziada itaongezeka kwa Sh80 hadi Sh100 nauli kwa dakika.

Pia, kwa upande wa magari yanayobeba abiria sita nauli elekezi ni Sh.4,000 hadi Sh.5,000 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama kutakuwa na safari ya ziada toka ya awali nauli itaongezeka kwa Sh1,000 hadi Sh.1,200 kwa kilomita moja na vinapotokea vikwazo kama foleni nauli itaongezeka Sh80 hadi Sh150 kwa dakika.

Amesema kwa nauli za pikipiki ya kubeba abiria wawili nauli elekezi itakuwa Sh.1,000 hadi Sh.1,500 kwa safari isiyozidi kilomita moja na kama safari itaongezeka kutoka hapo nauli itaongezeka kwa Sh.300 hadi Sh400 kwa kilomita moja na kama kutakuwa na vikwazo kama foleni nauli itaongezeka Sh.50 hadi Sh.70 kwa dakika.

“Kwa upande wa nauli za pikipiki mtandao zinazobeba abiria wasiozidi watatu ni nauli Sh.2,000 hadi Sh.2,500 kwa safari isiyozidi kilomita moja na safari ya ziada itakayongezeka nauli itaongezeka kwa Sh.500 hadi Sh.600 kwa kilomita moja na kama kutakuwa na vikwazo njiani kama foleni nauli itaongezeka kwa Sh70 hadi Sh90 kwa dakika moja,” amesema CPA Suluo.

Aidha CPA Suluo kuhusu usafiri wa mabasi amesema kuwa mamlaka inawakumbusha mabasi yaendayo haraka kuzingatia kanuni ziliopangwa ili kufanya kazi kwa weledi.

CPA Suluo amesema bado wapo kwenye vikao vya masikilizano na wadau kuhusu nauli za treni ya mwendokasi (SGR) na bei kamili ya nauli hizo zitatangazwa mwezi ujao baada ya kuwasili kwa mabehewa nchini.

Kuhusu tiketi mtandao kuandika jina abiria CPA Suluo amewasisitiza wananchi kuhakikisha wanazingatia hilo ili ajali inapotokea waweze kutambulika kirahisi.

“Naomba jamii izingatie suala la majina kuandikwa kwenye tiketi zao,”amesema CPA Sulu.