DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Katika kuboresha mazingira ya utoaji huduma za mawasiliano nchini, Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari imetangaza maboresho ya Kanuni za Miundombinu ya Utangazaji Dijiti na Kanuni za Leseni zinazosimamiwa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA). 

Maboresho ya kanuni hizi pamoja na mambo mengine yanakusudia kuboresha mazingira ya uwekezaji na utoaji huduma nchini, pia kupanua wigo wa upatikanaji wa huduma za mawasiliano ya kielektroniki nchini.

Makala hii inanuia kuainisha maboresho ya msingi yaliyofanywa katika kanuni mbili ambazo ni Kanuni za Leseni, 2018 na Kanuni za Miundombinu ya Utangazaji Dijiti, 2018. Lengo la mabadiliko haya ni kuendana na mabadiliko ya kasi ya ukuaji wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Maboresho katika Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Leseni), 2022 

Katika maboresho haya mambo yaliyofanyiwa uboreshwaji ni kama ifuatavyo: –

Mosi, kufuta ada ya masafa kwa wenye miundombinu ya utangazaji wa televisheni dijiti (MUX) ili kuleta nafuu kwa wawekezaji kwenye eneo hili na kuwawezesha kupanua wigo wa huduma za mawasiliano pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa huduma bora za mawasiliano. 

Pili, kuainisha aina mpya ya leseni maalumu kwa watoa huduma wanaotengeneza bando za maudhui, kurahisisha utoaji wa leseni, pia kuhimiza watengenezaji wa maudhui wa ndani kuandaa yanayohamasisha ukuaji wa utamaduni wa Kitanzania na jamii inayoizunguka. Vilevile, kuongeza ajira kwa vijana wanaovutiwa na uandaaji wa maudhui kwa kuzingatia kuwa hitaji la soko katika miaka ya hivi karibuni limeongezeka kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ongezeko la idadi ya watu. 

Tatu, kubadili leseni ya vituo vya utangazaji vya kijamii kuwa leseni ndogo. Lengo la maboresho haya ni kuchochea uanzishwaji wa vituo vya utangazaji vya kijamii katika maeneo ya nchi yasiyofikiwa au yanayopata huduma hafifu za utangazaji hasa wa redio. 

Hatua hii pia itawezesha wananchi kunufaika kwa kupata huduma za maudhui ya utangazaji yanayoakisi maisha na tamaduni zao katika maeneo husika. 

Aidha, upatikanaji wa leseni hizi utachukua muda mchache zaidi kwa kuwa mlolongo wa uchakataji wa leseni umefupishwa tofauti na leseni kubwa zinazohitaji mchakato wenye mlolongo zaidi hadi hatua ya mwisho ya ukamilishwaji. 

Nne, kupunguza ada za leseni ili kuwezesha utoaji huduma nafuu na wenye viwango utakaosaidia kukuza ajira na kuvutia watu wengi zaidi kuwekeza katika sekta ya mawasiliano nchini.

Tano, kuainisha aina mpya ya leseni ya utangazaji kwa maudhui maalumu ya elimu ili kutoa nafasi kwa taasisi au mashirika yanayonuia kutoa huduma ya elimu kutoa kwa kuzingatia kwamba mazingira ya utoaji elimu yamekuwa yakibadilika katika miaka ya karibuni kutokana na sababu mbalimbali, ikiwamo mlipuko wa maradhi kama vile UVIKO -19 uliochagiza kubadilika kwa modali ya uwasilishaji elimu maeneo mengi duniani, Tanzania ikiwamo. 

Maboresho katika Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Redio na Televisheni), 2021 

Maboresho yafuatayo yamefanyika kwenye kanuni zinazoongoza huduma za utangazaji wa televisheni na redio, kama ifuatavyo:-

Mosi, kuruhusu chaneli za televisheni za kulipia kuchukua matangazo ya kibiashara (yasizidi dakika tano kwa saa). Kabla ya maboresho haya ya kanuni, haikuruhusiwa chaneli za televisheni za kulipia kuweka matangazo ya kibiashara. 

Wizara pamoja na TCRA wanabainisha kwamba lengo la kuruhusu chaneli za televisheni za kulipia ziweze kuchukua matangazo ya kibiashara ni kuweka mazingira bora zaidi ya uwekezaji katika utengenezaji wa maudhui, pia kuendana na uhalisia wa biashara ya chaneli za maudhui ya kulipia. Kuhimiza (promote) maudhui ya ndani, pia kuwezesha wasanii wa ndani kutengeneza maudhui ya kulipia.

Nne, kuruhusu chaneli za televisheni za kutazamwa bila kulipia (Free to Air) zionyeshwe bila kulipia katika visimbuzi vyote nchini pasipo kujali ni vya kulipia au la. Kabla ya maboresho haya ya kanuni, chaneli za kutazamwa bila kulipia (Free to Air) hazikuruhusiwa kuonyeshwa katika ving’amuzi vya kulipia nchini. 

Lengo la maboresho katika eneo hili ni kuongeza wigo wa mapato kwa watoa huduma wa chaneli za kutazamwa bila kulipia; kuongeza wigo wa ufikiwaji wa habari kwa wananchi, kwa sababu kwa maboresho haya kila king’amuzi kitaweza kuonyesha chaneli zote za kulipia na zisizo za kulipia.

Aidha, hatua hiyo ya kuruhusu visimbuzi vyote kubeba chaneli za bila kulipia kunaongeza na kuwezesha uhuru wa watazamaji kuchagua chaneli watakazo kirahisi. Pia itawezesha kutatatua changamoto ya mtumiaji kulazimika kumiliki kisimbuzi zaidi ya kimoja.

Mabadiliko mengine kwenye kanuni hizi ni yanayoruhusu chaneli za televisheni za kulipia kurusha matukio mbashara (live events) yakiwamo matukio ya kitaifa kama vile hotuba za viongozi waandamizi wa taifa. Kabla ya marekebisho haya chaneli za kulipia hazikuruhusiwa kurusha matukio mbashara. 

Maboresho katika Kanuni za Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (Simu na Intaneti), 2021 

Katika kanuni hizi, mambo kadhaa yamefanyiwa maboresho na marekebisho kama ifuatavyo:-

Mosi, kuboresha mfumo wa leseni kwa kuainisha leseni ya Vituo vya Kuhifadhi Taarifa (Public Data Centre Licence). Maboresho haya yanalenga kuongeza wigo wa uwekezaji katika huduma za mawasiliano hasa katika masuala ya kuhifadhi taarifa kutokana na ongezeko la huduma mtandao kama vile ‘cloud computing services’.

Pili, kuainisha leseni kwa ajili ya vituo vya maingiliano ya mtandao (Internet exchange Points). Maboresho haya yatawezesha kuainisha vigezo vya kiufundi vya miundombinu ya vituo vya maingiliano ya mtandao (Internet Exchange Points).

Tatu, kupunguza ada za masafa ya mawasiliano ya redio ili kuhimiza upelekaji wa mtandao (network expansion) katika maeneo mengi zaidi nchini. Mabadiliko haya yanaendana na Dira ya Maendeleo ya 2025 inayolenga kuhakikisha ufikishwaji wa huduma za TEHAMA kwa wananchi wote. 

Nne, maboresho ya nne yanahusisha kupunguza ada ya vituo vya mawasiliano ya redio kutoka dola 3,000 za Marekani hadi kuwa dola 100 za Marekani kwa kituo, ili kuongeza kasi ya usambazaji wa intaneti yenye kasi nchini, hasa maeneo yasiyofikiwa kirahisi na miundombinu iliyopo.

Tano, kuainisha ada kwa ajili ya mawasiliano ya simu kwa njia ya satelaiti ili kuongeza udhibiti wa huduma za mawasiliano ya simu kwa njia hiyo.

Sita, kuondoa ada ya usajili kwa madishi ya mawasiliano ya redio ili kuongeza usambaaji wa huduma. Saba, kupunguza ada za madishi ya mawasiliano ya redio (VSAT) kutoka dola 3,000 za Marekani na kuwa dola 60 za Marekani ili kuhimiza matumizi ya VSAT, pia kuchochea uwekezaji katika eneo hili.

Saba, kutofautisha kati ya leseni ya kutengeneza vifaa vya mawasiliano ya kielektroniki kwa mafundi wakubwa na wadogo. Mabadiliko ya nane yanahusu kupunguza ada mbalimbali za leseni ili kupunguza mzigo wa ada kwa watoa huduma na kuhimiza uwekezaji zaidi. 

Mwisho, kuongeza aina mpya ya leseni ndogo kwa ajili ya huduma mtandao kwa ajili ya kutambua huduma mpya za mtandao na kuweka mazingira wezeshi kiudhibiti.

Maboresho ya kanuni ni suala muhimu katika kuhakikisha utoaji wa huduma za mawasiliano unaendana na mabadiliko ya teknolojia na uhalisia wa mazingira yaliyopo na dhamira ya serikali ni kuendelea kufanya maboresho ya Kanuni kila itakapohitajika kwa kuzingatia kuwa teknolojia inabadilika kila mara kama mkondo wa maji unavyobadili njia zake kila mtiririko unavyosonga. 

Wizara pamoja na TCRA wanatarajia kuona wadau wa sekta ya mawasiliano wakiendeleza ushirikiano madhubuti ili kuendelea kuijenga Tanzania yenye huduma bora za mawasiliano ambazo ni chachu ya maendeleo ya nchi yetu katika kujenga uchumi wa kidijitali.

Makala hii imetayarishwa na Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano kwa Umma cha TCRA 

By Jamhuri