Wanaoishi kinyemela nchini sasa ni wakati wa kuwabaini

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Uhamiaji anasema jeshi hilo linaendelea na operesheni ya kuwabaini wahamiaji haramu nchini.

Anasema tayari kazi hiyo imeonyesha mafanikio makubwa kwani watu wengi walio nchini kinyume cha sheria wameshatiwa mbaroni na kufikishwa mahakamani na wengine kurejeshwa makwao.

Tunampongeza Kamishna Jenerali kwa hatua hiyo muhimu katika kulinda ustawi wa nchi yetu, lakini tunakiri kusema kuwa bado kuna kazi kubwa ya kufanya, kwa sababu watu wanaoishi kinyemela hapa nchini ni wengi mno.

Kijiografia na kirasilimali Tanzania ni kivutio kikubwa kwa wageni wengi kutoka Afrika na nje ya bara hili. Tabia ya kiungwana ya Watanzania ya kutotaka kuulizana makabila na asili zetu imekuwa mwanya mkubwa sana kwa wageni kuja kuishi nchini kihuni au bila kufuata sheria.

Wapo wanaoamini kuwa kasi ya ongezeko la watu nchini mwetu inachangiwa na kuiacha wazi mipaka yetu kiasi kwamba wageni ni rahisi kuingia na kujichanganya na wenyeji. 

Hali hiyo imeiliumiza taifa kwa sababu wakati mwingine mipango yetu ya maendeleo imekwazwa na ongezeko la watu lisilowiana na uhalisia wa kuzaliana kwetu.

Mwaka huu tunatarajia kuwa na sensa kubwa ya watu na makazi. Ni wajibu wa vyombo vya dola na raia wema kuhakikisha Watanzania halisi wanatambulika, pia wageni nao wanajulikana.

Tunasema hivyo kwa sababu tayari upo ushahidi usiotiliwa shaka kuwa maeneo kama ya mipakani kuna wahamiaji kutoka nchi jirani wanaoingia Tanzania kufaidi huduma za elimu bure, na ardhi ya kilimo na malisho. Kuna wageni wameingia hadi katika misitu na kuua wanyamapori na kuchoma mkaa ambao huusafirisha nje ya nchi.

Pamoja na kuamini kuwa binadamu wote ni ndugu zetu, na kwamba Afrika ni moja, bado hatuna sababu ya kuachia nchi yetu iwe shamba la bibi ambalo kila anayejisikia anaingia kufaidi kilichomo. Tunao wajibu wa msingi wa kuhakikisha Tanzania inakuwa ya Watanzania kwanza ili wafaidi rasilimali walizopewa na Mwenyezi Mungu.

Kauli hii hailengi kuleta ubaguzi, bali ni ukweli ulio wazi kwamba ni wajibu wetu kuhakikisha mipaka yetu inakuwa thabiti, kwa kuwachuja hasa wale wanaokuja kuishi nchini kinyemela na kuwa kichocheo cha uhamishaji rasilimali na uhalifu.

Tuitumie sensa ya mwaka huu kuhakikisha tunakuwa na idadi halisi ya watu ambao ni raia halali wa nchi hii ili isaidie kupanga mipango ya maendeleo.

Kwa ufupi idadi ya watu wanaoishi kinyemela humu nchini ni kubwa mno. Sasa ni wakati sahihi wa kuwabaini.