Wiki iliyopita kwenye maandiko ya mwalimu katika kitabu cha “Maendeleo ni kazi” tuliona agizo la mwalimu la kutaka chama tawala kushughuka na mambo ambayo tayawafanya wananchi kujitawala  wenyewe katika maisha yao ya kila siku. Sehemu inayofuata ni mwendelezo wa tulipoishia wiki iliyopita .. Endelea….

 Kazi za mkutano Mkuu:

Kutokana na kukua kwa chama na umuhimu wa kuwa na njia zilizo wazi za uwakilishi wa fikra za wanachama, kutoka vikao vya chini mpaka mkutano mkuu na vikao vya juu mpaka kumfikia mwanachama, Mkutano Mkuu unaiona haja ya kufafanua zaidi mwenendo wa mikutano ya Taifa, Mkoa na Wilaya.

Kwa hiyo Mkutano Mkuu unaiagiza Halmashauri Kuu ya Taifa kuchukua hatua za kuhakikisha kwamba kwenye mikutano mikuu hiyo wajumbe wanawasikiliza mawazo ya wanaowawakilisha.

Uchumi:

Katika kuzingatia msimamo wetu kwamba msingi na shabaha ya maendeleo ya Tanzania ni watu, Mkutano Mkuu unaazimia kwamba juhudi ya kuwashirikisha watu katika shughuli zote za maendeleo iongezwe, mkutano umeagiza pia kuwa tangu sasa mahitaji muhimu ya maji, shule na afya yafikiriwe kwanza katika matumizi yetu isipokuwa ya ulinzi na usalama.

Na ili kutekeleza agizo hilo mpango wa pili wa maendeleo urekebishwe . mkutano mkuu ukaagiza tena kwamba hatua zichukuliwe za kuwakilisha watu kikamilifu katika utayarishaji wa mipango ya maendeleo.

Mkutano umeagiza kuwa katika utekelezaji wa mipango na katika utendaji kazi mbali mbali za umma kila jitihada ifanywe ya kukomesha matumizi ya kifahari na anasa ili fedha tuliyo nayo iweze kuhudumia watu wengi zaidi.

Ili mipango ya maendeleo iweze kutekelezwa haraka na kwa ukamilifu zaidi, hatua zichukuliwe zitakazoipa Mikoa na wilaya mamlaka na uwezo wa kutekeleza mipango ya maendeleo ya sehemu zao.

Mkutano mkuu unatambua utajiri mkubwa na mali ya asili kama vile madini, maji, samaki, misitu, n.k. tulio nao katika nchi yetu na kwa hiyo unasisistiza  umuhimu wa kutumia rasilimali hizo ili kupanua uchumi wa Taifa letu.

Hali kadhalika mkutano mkuu unatoa wito kwa wana-TANU na vyombo vyote vinavyohusika  kuchukua hatua za kusitawisha uchumi wa ndani ya nchi,

 

Elimu:

Mkutano mkuu unazingatia umuhimu wa Elimu kwa maendeleo ya watu, ujenzi wa ujamaa  na demokrasia. Kwa hiyo unaipongeza serikali na wananchi  wote walioshiriki na mafanikio  makubwa yaliyopatikana katika kuendeleza Elimu ya watu wazima tangu Rais wa chama atoe wito kwa Taifa kuhusu wuala hilo.

Mkutano umevutiwa sana na juhudi iliyofanywa na wananchi wa mafia, chini ya uongozi wa chama, ambayo imewezesha kutekelezwa kikamilifu kwa wito wa Rais kutojua kusoma na kuandika kabla ya mwisho wa mwaka huu.

Mkutano unatoa pongezi maalum kwa viongozi na wananchi wote wa Mafia kwa mafanikio hayo na unatoa wito kwa viongozi na wananchi nchini pote kujifunza njia zilizotumika Aidha Mkutano unatoa wito kwa wananchi wote waliojaliwa kusoma hasa wafanyakazi, kushiriki katika mipango ya Elimu ya watu wazima .

Vile vile mkutano mkuu unaagiza kuwa tangu sasa elimu iwe sehemu ya kazi mahali pote na mipango itayarishwe ya kutekeleza wito huu. Mkutano mkuu unaagiza kwamba mipango ifanywe ili kutojua kusoma na kuandika vifutwe kabisa katika miaka minne ijayo.

Mkutano mkuu unatambua kwamba mafanikio ya kusisimua yaliyopatikana katika elimu ya watu wazima hivi karibuni, yametokana njia  za kimapinduzi zilizotumiwa; hivyo unahimiza  serikali kuchukua hatua za kubadili mtindo unaofuatwa hivi sasa katika elimu ya msingi na kutafuta njia zitakazotuwezesha kulifikia kwa haraka lengo letu la elimu kwa watoto wote.

Reli ya Tanzania na Zambia;

Mkutano unachukua nafasi hii kuusifu uamuzi wa kijasiri uliochukuliwa na serikali ya Zambia na Tanzania wa kujenga reli inayowaunganisha nchi hizo mbili. Mkutano unaipongeza pia serikali ya Jamhuri ya watu wa China kwa kukubali kuzisaidia nchi zetu mbili.

Mkutano unatambua kwamba kujengwa kwa reli hii mema ya kazi hiyo na unawapongeza wafanyakazi wote wa Jamhuri ya watu wa China kwa kazi njema hiyo.

Mkutano mkuu  umetiwa moyo na taarifa ya maendeleo mema ya kazi hayo na unawapongeza wafanyakazi wote wa Zambia na Tanzinia na wa Jamhuri ya watu wa China kwa kazi yao njema hiyo.

Mkutano unatambua kwamba kwamba kujengwa kwa reli hii kunaleta matumaini makubwa ya kusaidia maendeleo katika Mikoa inakopitia, na kwamba ili kuhakikisha maendeleo hayo yanawanufaisha watu, unatoa wito kwa wananchi kuanzisha vijiji vya Ujamaa kando kando ya reli hiyo.

Vijiji vya Ujamaa:

Mkutano mkuu unatambua maendeleo makubwa yaliyofanyika nchini katika uanzishaji wa vijiji vya Ujamaa; na unawapongeza wananchi wote walioitikia wito huo hasa wananchi wa Dodoma ambao kwa maelfu wamejiunga katika vijiji vya ujamaa mwaka huu.

Mkutano unampongeza Rais wa chama kwa kushiriki kwa vitendo  katika shughuli za ujenzi wa ujamaa kama alivyofanya kwa kuishi vijiji Dodoma na unatoa wito maalum kwa viongozi wote wa chama na vyombo vyake  vya utekelezaji kuongozwa na mfano huo katika shughuli zao za kila siku. Vile vile utaratibu ufanywe utakaowawezesha wafanyakazi kwenda vijijini kushirikiana na wanavijiji  kazi katika kazi.

Ili kuimairisha uongozi wa kijamaa vijijini na kuwawezesha wana-vijiji kujifunza kutoka kwa wenziwao, mkutano unahimiza mipango ya semina za siasa vijijini na kuwepo kwa utaratibu utakaowezesha wajamaa wa vijiji mbali mbali kutembeleana.

Mkutano Mkuu unasisitiza umuhimu kwa vijiji vya Ujamaa kuwa na mipango kuhusu shughuli zote za vijiji, na hasa shughuli za maendeleo ya uchumi; na unatambua juhudi kubwa iliyokwisha kufanywa katika jambo hili.

Mkutano  unatilia mkazo haja ya kuzidisha bidii katika kuwasaidia wanavijiji kutayarisha mipango yao; na unasisitiza kwamba ili ifanikiwe, mipango hiyo sharti izingatie matakwa ya wanavijiji mazingira ya mahali walipo na mahitaji ya nchi nzima.

Kadhalika utekelezaji wa mipango hauna budi usimamiwe barabara; na kila jitihada ifanywe ili kuwafundisha wavijiji wenyewe aina mbali mbali za ufundi na maarifa kwa madhumuni ya kuwazidishia uwezo wa kujitegemea.

Ulinzi na Usalama.

Mkutano Mkuu unaipongeza Hlmashauri Kuu kwa hatua ilizochukua kuimarisha ulinzi na usalama wa Taifa; na unapongeza majeshi na wananchi kwa kazi yao nzuri wanayofanya mkutano unatoa pongezi maalum kwa wanajeshi wa Tanzania walioko mpakani kwa ujasiri waliouonyesha katika kulinda uhuru na siasa ya nchi yetu.

Mkutano mkuu huo umetumia nafasi hii kusisitiza kwamba majeshi yetu ni majeshi ya ulinzi; ni majeshi ya kuilinda nchi yetu kutokana na masdhambulizi na uchokozi wa adui; si majeshi ya kushambulia nchi nyingine yoyote.

Lakini mkutano unasisitiza pia kwamba wanajeshi wetu, au raia wetu wakifanyiwa uchokozi, basi mchokozi huyo hana budi apewe adhabu anayostahili.

By Jamhuri