Katika kipindi cha miaka miwili cha uongozi wa serikali ya awamu ya sita Wakala wa Usalama Mahala pa kazi (OSHA) umeongeza idadi ya maeneo ya Kazi yaliyosajiliwa kutoka 4,336 hadi 11,953 ikiwa ni ongezeko la asimilia 276.

Hayo ameyasema leo Machi 4,2023 jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA), Khadija Mwenda,wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali na utekelezaji wa majukumu ya Wakala hiyo katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Aidha amesema kuwa idadi ya kaguzi zilizofanyika zimeongezeka kutoka kaguzi 104,203 hadi kufikia Kaguzi 322,241 sawa na asilimia 132.

MTENDAJI Mkuu Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) Bi. Khadija Mwenda,akijibu maswali lmbalimbali yaliyoulizwa na waandishi wa habari (hawapo pichani)  leo Machi 4,2023 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya OSHA katika kusimamia Sheria ya Usalama na Afya katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita.

“Halikadhalika, kumekuwa na ongezeko la asilimia 175 ya Wafanyakazi waliopata mafunzo ya Usalama na afya mahali pa kazi kutoka wafanyakazi 32,670 hadi kufikia Wafanyakazi 43,318”amesema Mwenda.

Aidha amesema kuwa Mafunzo haya yanajumuisha mafunzo ya usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi na uundwaji wa kamati za Usalama na Afya ,mafunzo ya kufanya kazi za mazingira ya juu.

Pia, mafunzo ya huduma ya kwanza, mafunzo ya usimamizi na udhibiti wa kemikali katika maeneo ya kazi, mafunzo ya usalama na afya katika sekta ya mafuta na gesi na katika sekta ya ujenzi na majenzi, mafunzo ya usalama wa mitambo.

Aidha amesema kuwa katika kkipindi hicho kumekuwa na ongezeko la upimaji afya za wafanyakazi kwa asilimia 320.

“Upimaji afya kutoka Wafanyakazi 363,820 hadi kufikia Wafanyakazi 1,112,237 waliopimwa katika kipindi tajwa”amesisitiza

Amesema ongozeko hilo lilitokana na kupunguza ada mbalimbali na kuboresha mifumo ya usimamizi ambayo imewezesha maeneo mengi ya kazi kukaguliwa, wafanyakazi wengi kupimwa afya na mafunzo mbalimbali kufanyika, hali hiyo inamaanisha kuwa hali ya usalama na afya katika maeneo ya kazi inazidi kuimarika.

Kadhalika, amesema katika kusimamia Sheria ya Usalama na Afya kwa lengo la kuzuia ajali, magonjwa na vifo vitokanavyo na kazi, maeneo ya kazi ambayo hayakuzingatia Sheria na Kanuni za Usalama na Afya yalichukuliwa hatua mbali mbali za kisheria zikiwemo kupewa hati ya maboresho ambapo maeneo ya kazi 1,588 yalipewa hati hizo na maeneo ya kazi mengine105 yalitozwa faini.

Mwenda amsema miongoni mwa majukumu ya OSHA ni kuchunguza ajali mbali mbali zinazotokea katika sehemu za kazi kwa lengo la kubaini vyanzo vya ajali hizo ili kushauri namna bora ya kuzuia ajali kutokea tena.

Amesema kuwa katika kipindi cha miaka miwili, ajali zilizoripotiwa zilipungua kwa asilia 13.2 kutoka ajali 2,138 kupungua hadi kufika 1,855.

Vilevile, Magonjwa yanayotokana na kazi yalipungua kwa asilimia 22.1 kutoka wagonjwa 140 kufikia wagonjwa 109.

MTENDAJI Mkuu Wakala wa Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA) Bi. Khadija Mwenda,akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 4,2023 jijini Dodoma wakati akielezea mafanikio ya OSHA katika kusimamia Sheria ya Usalama na Afya katika kipindi cha miaka miwili ya Serikali ya Awamu ya Sita.

Amesema takwimu hizi zinaonesha kuimarika kwa mifumo ya usimamizi wa masuala ya usalama na afya mahali pa kazi, ambayo imepelekea ajali na magonjwa yatokanayo na kazi kupungua.

“Sambamba na kuimarika kwa mifumo hii ya usimamaizi wa usalama na afya, kunapelekea mifuko ya hifadhi ya jamii kuwa himilivu”amesisitiza

Hata hivyo, amesema OSHA imepata mafanikio makubwa ambayo yametokana na uongozi madhubuti wa Rais Samia Suluhu Hassan yanayoendana na utekelezaji wa Ilani ya Chama Tawala Ibara ya 130 (f) ambapo Chama kimewaahidi Watanzania kwamba kitajenga uwezo wa waajiri na wafanyakazi kuhusu afya na usalama mahali pa kazi.

By Jamhuri