*Atangaza kimbunga kwa wavamizi wa barabara
*Afumua mtandao wa ufisadi, gharama ujenzi zashuka
*Flyovers kuanza kujengwa kwa kasi jijini D’ Salaam

Waziri wa Ujenzi, Dk. John Magufuli, ametangaza kiama dhidi ya wavamizi wa hifadhi za barabara nchini, huku akifanikisha kushusha gharama za ujenzi kutoka Sh bilioni 1.8 kwa kilomita moja hadi Sh milioni 700.

Kwa msimamo huo, amesema wavamizi wote waliokuwamo na watakaokuwamo kwenye hifadhi, hawatalipwa fidia.

Amewaonya mameneja wote wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) mikoani kote kwamba watakaoshindwa kusimamia sheria kikamilifu, na hasa Sheria ya Hifadhi ya Barabara, wataondolewa katika nafasi zao mara moja.

Dk. Magufuli alitangaza msimamo huo bungeni alipokuwa akiwasilisha Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi ya Mwaka wa Fedha wa 2012/2013, jana.

Akinukuu vifungu kadhaa vya sheria, Dk. Magufuli alisema, “Wizara imeendelea kuzingatia sheria mbalimbali hususani Sheria ya Barabara Na. 13 ya Mwaka 2007. Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Ibara ya 26 (Kifungu cha 1 na 2), inatutaka wananchi wote kufuata na kutii Katiba na sheria za nchi.

“Kwa mantiki hii, inashangaza sana pale wizara inapoombwa kulipa fidia wananchi ambao kwa mujibu wa sheria wamo ndani ya hifadhi ya barabara. Baadhi ya maombi hayo yanatoka kwetu sisi viongozi ikiwa ni pamoja na kwenu waheshimiwa wabunge mliopitisha Sheria Na. 13 ya Mwaka 2007.

“Kufanya hivyo ni kukiuka sheria ambazo ndizo zinatuongoza. Wizara itaendelea kuzingatia sheria na wananchi wote walio ndani ya eneo la hifadhi ya barabara na wale waliokwisha ondolewa hawatalipwa fidia. Kwa wananchi ambao bado wapo ndani ya hifadhi ya barabara wanatakiwa waondoke wenyewe bila fidia.”

Ujenzi barabara za lami kuendelea kwa kasi

Dk. Magufuli alizungumzia kasi ya ujenzi wa barabara nchini kwa kusema Serikali ya Rais Jakaya Kikwete inaendelea na ujenzi wa barabara za lami zenye urefu wa kilomita 11,154.35 nchini kote. Orodha ya barabara hizo na gharama zake zimeainishwa katika hotuba ya Dk. Magufuli iliyopo ukurasa wa saba wa toleo hili.

Amesema Sh bilioni 6,005.63653 zitatumika katika ujenzi wa miradi mikubwa ya barabara, madaraja, vivuko, nyumba na majengo ya Serikali nchini kote katika mwaka huu wa fedha wa 2012/2013. Kiasi hicho cha fedha, kwa mujibu wa Dk. Magufuli, hakihusishi miradi mingine midogo inayoendelea.

Kwa miradi hiyo yote nchini, ameliambia Bunge kwamba ajira 650,000 zimepatikana chini ya Wizara ya Ujenzi pekee.

“Ukichukua miradi mikubwa ya ujenzi wa barabara na madaraja katika mikoa yote, ikajumuishwa na miradi ya nyumba na vivuko pamoja na miradi ya ukarabati na kazi za matengenezo maalumu na ya dharura katika mikoa yote ya Tanzania Bara, miradi iliyo chini ya Wizara ya Ujenzi kwa ujumla inatarajiwa kuajiri zaidi ya watu 650,000.

“Idadi hii ni mbali na mama/baba lishe, wachimba kokoto, wafyatua matofali, watengeneza mbao za ujenzi, wachimba mchanga na kadhalika. Wafanyakazi hawa wote watafanya kazi katika miradi niliyoitaja katika mwaka wa fedha wa 2012/2013,” amelithibitishia Bunge.

Usajili wa makandarasi kufuatiliwa

Dk. Magufuli amesema Wizara ya Ujenzi inaendelea kufutilia usajili wa makandarasi, wahandisi na wahandisi washauri wasiotekeleza wajibu wao ipasavyo.

“Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Bodi za CRB, ERB na AQSRB, Bodi ya CRB imekwishasajili makandarasi wa madaraja yote 9,041 na imewafutia usajili makandarasi 2,576; ERB imesajili wahandisi 11,264 na imewafutia usajili wahandisi washauri sita na kampuni tano za ushauri wa kihandisi kwa makosa mbalimbali yakiwamo ya ukiukwaji wa maadili. AQSRB imesajili wataalamu wa fani za wabunifu majenzi na wakadiriaji majenzi 548 na kusajili kampuni 269 za ushauri katika fani hizi,” amesema.

Gharama ujenzi wa barabara zashuka

Umakini wa Waziri Magufuli umefanikisha kushusha gharama za ujenzi wa barabara kutoka Sh bilioni 1.8 kwa kilomita moja mwaka 2010 hadi kati ya Sh milioni 680 na Sh milioni 780 kwa kilomita kwa mwaka 2011/2012.

Amesema, “Mfano ni gharama za ujenzi kwa barabara ya Dodoma – Iringa na Same – Mkumbara. Aidha, jitihada za kutumia makandarasi wa ndani nazo zimeanza kuzaa matunda kwa makandarasi hao kuanza kuchukua miradi mikubwa ya ujenzi kama ambavyo imetokea katika daraja la Mbutu katika Mkoa wa Tabora wilayani Igunga linalojengwa na muungano wa makandarasi 13 wazalendo kwa gharama ya Sh bilioni 12.34.”

Katika hatua nyingine, Dk. Magufuli ameliambia Bunge kwamba Sh bilioni 300 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya kulipa madeni ya makandarasi.

Dar kuanza kuziona ‘flyover’

Ujenzi wa madaraja ya Kigamboni, Kilombero na Kikwete (Malagarasi) umeshaanza. Wakati ikipigwa hatua hiyo, tayari mpango wa kuanza ujenzi wa ‘flyover’ katika eneo la Tazara jijini Dar es Salaam, nao umetengewa fedha.

Barabara ya Dar es Salaam – Chalinze – Mororgoro itapanuliwa; huku Mradi wa Mabasi Yaendayo Kasi nao ukiwa umepangwa kukamilika kwa wakati.

Barabara ya Makutano – Natta – Mugumu/ Loliondo – Mto wa Mbu nayo imeshapatiwa ufumbuzi, na tayari mipango ya kuanza kuijenga kwa kiwango cha lami imeshaanza.

Mkoa wa Dar es Salaam umetengewa mabilioni yha shilingi kwa ajili ya upanuzi wa barabara. Aidha, TANROADS imechukua baadhi ya zilizokuwa barabara za manispaa na Jiji la Dar es Salaam.

Mchanganuo wa barabara hizo na gharama zake upo kwenye hotuba ya Waziri wa Ujenzi ndani ya gazeti hili zuri la Jamhuri.

Katika kukabiliana na foleni mkoani Dar es Salaam, Dk. Magufuli amelithibitishia Bunge kwamba usafiri wa boti kwa ajili ya abiria na mizigo kati ya Dar es Salaam na Bagamoyo, utaanza.

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) naye amepanga kujenga nyumba 2,500 nchi nzima. Viwanja 2,253 katika mikoa yote, ikiwamo mikoa mipya, vimeshapatikana.

1318 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!