Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa ameiagiza Benki kuu ya Tanzania (BOT) kuzisimamia Taasisi za kifedha kwa upande wa mabenki kuboresha riba katika mikopo wanayoitoa.

Akizungumza Leo,Agosti 3, 2023, katika banda la BoT mara baada ya  kutembelea mabanda ya Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane  yanayofanyika Kitaifa kwenye viwanja vya John Mwakangale, jijini Mbeya amesema Serikali inaendelea kuwaasa na kuwataka wafanye maboresho zaidi kwenye riba.

“Mabenki yote yapo katika maonesho haya ambayo wanaeleza namna yatakavyokupa mkopo wa kuanzisha shughuli zako za Kilimo,Mifugo na Uvuvi, ni kama bahati imekuja Leo Iko hapa na wewe upo hapa kwa nini urudi ukiwa huna majibu ambayo yote yatapatikana hapa na kila nilipopita niliuliza riba zao zikoje.

“Wengi walikuwa na riba ya asilimia 20, tukawaambia wakashusha ikafika asilimia 18,wakashusha ikawa asilimia 17,na baadae ikawa asilimia 15,wakaja kukwama kwenye asilimia 12,hivyo basi nimefurahi sana kukuta wameshuka wapo kwenye 9,na Matumaini yangu watashuka zaidi,amesema Mh.Majaliwa.

Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka mpango kabambe  wa kuwawezesha vijana kulima kibiashara (BBT), fanyieni kazi   hasa suala la kufanya kazi kwenye eneo kijana analolitaka.

“Vijana waliojiunga na mpango wa BBT, walioanza mafuzo mwaka huu, wamekaribia kuhitimu. Eneo la BBT liko pia kwenye mifugo. Unaweza kupewa eneo, ukaweka mifugo na kuwanenepesha. Kubwa zaidi ni upatikanaji wa mitaji,” amesema.

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa akimsikiliza Spika wa Bunge na Mbunge wa jimbo la Mbeya mjini Dkt. Tulia Ackson wakati  akizungumza katika maonesho ya Kimataifa ya Kilimo ya Nane Nane kwenye viwanja vya John Mwakangale  jijini Mbeya mara baada ya kutembelea mabanda mbalimbali katika maonesho hayo.

Naibu Gavana Utawala na Udhibiti wa ndani Benki kuu ya Tanzania (BoT) Bw. Julian Banzi katikati akiwa ameketi pamoja na Waziri wa Ulinzi Innocent Bashungwa kulia na Mkurugenzi wa BoT tawi la Mbeya Dkt. James Machemba wakigfuatilia hotuba wakati  Waziri Mkuu  akizungumza katika maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nane Nane yanayofanyika viwanja vya John Mwakangale  jijini Mbeya.

Naibu Gavana Utawala na Udhibiti wa ndani Benki kuu ya Tanzania (BoT) Bw. Julian Banzi akiwa na Mkurugenzi wa BoT tawi la Mbeya Dkt. James Machemba wakikirejea katika banda la BoT mara baada ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kumaliza kutembelea mabanda na kuzungumza na washiriki wa maonesho hayo.

Wananchi wakipata elimu ya Fedha na uelewa kuhusu majukumu ya Benki Kuu ya Tanzania wakati walipotembelea banda hilo kwenye maonesho ya Kimataifa ya Kilimo NaneNane yanayofanyika kwenye viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya

By Jamhuri