Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia,Mbeya

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hasaan, ameipongeza Benki ya NMB kwa mchango uliotukuka kwenye Sekta ya Kilimo, Uvuvi, Ufugaji na Misitu, sambamba na kusapoti Program ya Kuandaa Vijana na Wanawake Kujenga Kesho Iliyo Bora (BBT), huku akiishauri kushusha kadri inavyoweza riba ya mikopo ya nyanja hizo muhimu kwa uchumi.

Rais Samia alitoa pongezi hizo na ushauri huo leo Jumatano Agosti 8, alipotembelea Banda la NMB wakati wa kufunga Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Tanzania (Nane Nane 2023), kwenye Viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya, ambayo yalifunguliwa na Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, Agosti 1 mwaka huu.

Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara wa NMB, Nsolo Mlozi, ndiye aliyempokea Dk. Samia na kumueleza kuwa katika Sekta ya Kilimo (inayojumuisha kilimo chenyewe, Uvuvi, mifugo na Misitu), benki yake imeshatoa mikopo ya zaidi ya Shilingi Bilioni 319 tangu Julai 2021 walipoanza kutoa mikopo kwa riba ya asilimia 9 kwa mwaka.

“Tumeshatoa mikopo ya zaidi ya Shilingi Trilioni 1.61 katika Sekta ya Kilimo katika kipindi cha miaka sita mfululizo, huku kwenye Programu ya BBT, tangu mwezi Machi tumetenga Sh Bi. 20.

“Pia, NMB tunatoa Elimu katika Vituo Atamizi kwa vijana na wanawake, ambao wamebeba kaulimbiu ya maonesho haya ambayo tumeyadhamini kwa Sh. Milioni 80, huku tukishirikiana na Wizara ya Kilimo kuwezesha awamu inayofuata wanapoenda kwenye uzalishaji,” alibainisha Mlozi.

Mlozi akamueleza Rais Samia kuwa, katika Mikopo ya Kimkakati, NMB imetenga Sh. Bilioni 20 za mikopo ya ujenzi maghala ili kupunguza changamoto ya uharibifu na upotevu wa mazao ama kuathiri thamani na ubora wake.

Aliongeza kuwa wana mashirikiano na taasisi mbalimbali zinazotoa matrekta ‘power tillers,’ zana za kilimo na pembejeo, ikiwemo Kampuni ya Agricom Africa.

Kutokana na maelezo hayo ya Mlozi, Dk. Samia aliipongeza NMB kwa namna inavyowajali na kuwathamini wadau wa mnyororo wa thamani wa kilimo, kisha akaiomba benki hiyo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali yake na iwapo itawezekana, basi ishushe zaidi riba.

“Kwanza nawashukuru sana, pia hongereni kwa jitihada zenu kwenye Sekta ya Kilimo. Endeleeni kuunga mkono jitihada za Serikali. Mkiweza kushusha zaidi ya riba kwa mikopo ya kilimo basi shusheni ili wakulima wa Kitanzania waendelee kunufaika zaidi,” alisema Rais Samia.

Dk. Samia ametoa ombi sawa na alilotoa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea Banda la NMB, Agosti 4 mwaka huu, siku moja kabla ya Waziri Mkuu Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mizengo Pinda, kutembelea banda hilo na kuipongeza kwa jitihada zake kwenye Sekta ya Kilimo, huku akiitaka kutunza kanzi data ya wakopaji ili kufuatilia maendeleo ama changamoto zao katika Kilimo au biashara zao.

,……………………………………..

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan akimsikiliza Mkuu wa Idara ya Kilimo Biashara wa Benki ya NMB, Nsolo Mlozi alipotembelea Banda la Benki hiyo katika maonesho ya Kilimo, uvuvi na Ufugaji ya Nane Nane katika viwanja vya John Mwakangale jijini Mbeya. Wapili kulia ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson na Watatu kulia ni Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe

By Jamhuri