Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia, Lindi

Mbunge wa Jimbo la Ruangwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amekiomba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kutoa fomu moja tu ya mgombea urais 2025.

Majaliwa ameyasema hayo wakati akizungumzia utekekezaji wa Ilani ya CCM ambapo amesema ni vema Halmashauri Kuu ya CCM 2025 ikatoka fomu moja tu ya Rais Samia Suluhu Hassan.

“Nisikosee mbele ya wajumbe wenzangu ila kusema kwa vyovyote itakavyokuwa Makamu Mwenyekiti Abdulrahman Kinana tunaomba mkashauri kule Kamati Kuu na Halmashauri Kuu watoe fomu moja tu ya Dk Samia Suluhu Hassan mwaka 2025 kama mgombea pekee wa CCM,” amesema.

Akizungumzia hilo Kinana amesema hakuna dhambi kwa kiongozi aliyeko madarakani anapomaliza awamu ya kwanza kupewa awamu ya pili aendelee kuongoza.

Amesema, Rais Samia ameonyesha njia kwa kupanga, kuweka mikakati na vipaumbele na sasa Watanzania wanajivunia mafanikio na hata wana CCM wanaposema mgombea tuliyenaye anatosha kugombea mwaka 2025 nadhani kama wanasababu yoyote zaidi ya kutambua mchango wake mkubwa katika taifa hili.

“Na Wana-CCM si dhambi kusema fomu ya mgombea urais ni moja kama wanaridhika na kiongozi aliyeko madarakani. Pia CCM tuna utaratibu wetu kiongozi akichukua awamu ya kwanza anapewa kuongoza na awamu ya pili, “amesema na kuongeza

“Rais Samia Suluhu Hassan yuko awamu ya kwanza, kwa nini asipewe awamu ya pili? Hakuna sababu ya kusema hapana. Kwa CCM tumezingatia utaratibu wa chama chetu Rais anapomaliza kuongoza awamu ya kwanza anaingia ya pili.

By Jamhuri