ABUJA, NIGERIA

Katika hali isiyokuwa ya kawaida, ndege ya kivita ya jeshi la Nigeria imetunguliwa na kundi linalodaiwa kuwa la majambazi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Nigeria, rubani wa ndege hiyo, Luteni Anga Abayomi Dairo, alijikuta akishambuliwa na kundi hilo baada ya mwenyewe kufanya mashambulizi dhidi ya watekaji nyara.

“Amenusurika kifo na hata kutekwa nyara na majambazi hao baada ya kuruka kutoka kwenye ndege, akajificha, kisha kuungana na wenzake,” inasema taarifa hiyo.

Shambulio hilo limetokea kwenye mpaka wa majimbo ya Zamfara na Kaduna.

Kundi lenye silaha – linalofahamika na wakazi wa maeneo hayo kama ‘majambazi; – limekuwa likilaumiwa kuhusika na utekaji nyara wa hivi karibuni eneo la kaskazini magharibi mwa Nigeria.

Limekuwa likiwalenga zaidi wanafunzi na watoto wa shule ambapo zaidi ya watoto 1,000 wametekwa nyara kuanzia Desemba mwaka jana. 

Wengi wameachiwa huru, inasemekana, baada ya kulipa ‘kikombozi’ (fidia), lakini wengine wameuawa.

Hivi karibuni Rais Muhammadu Buhari amelielekeza jeshi kufanya kila kinachowezekana kumaliza uhalifu katika majimbo ya Katsina, Zamfara na Kaduna.

Jeshi la Anga la Nigeria linasema linafanya operesheni za usiku na mchana dhidi ya wahalifu kwa kushirikiana na majeshi ya ardhini. 

Ni katika moja ya operesheni hizo ndipo ndege hiyo ilipotunguliwa.

“Kutokana na operesheni hizi, mamia ya wahalifu wamezimishwa huku maficho yao kadhaa yakiharibiwa,” inasema taarifa ya Jeshi la Anga.

Pamoja na kwamba kumekuwa na ajali kadhaa za ndege za kijeshi kwa mwaka huu, hii ni mara ya kwanza kwa ndege ya kivita kutunguliwa na wahalifu wenye silaha.

Mei mwaka huu, Nigeria ilikumbwa na mshituko pale Luteni Jenerali Ibrahim Attahiru, alipofariki dunia katika ajali ya ndege pamoja na maofisa wengine 10.

Mwezi mmoja nyuma, Aprili, ndege nyingine ilianguka katika Jimbo la Borno – moja ya maeneo ambako Boko Haram wameshika hatamu. 

Jeshi likakanusha taarifa kwamba ilitunguliwa na waasi hao.

Kabla ya hapo, Februari mwaka huu, ndege ya jeshi ilianguka Abuja ikiwa inaelekea kuwatafuta wanafunzi waliotekwa katika Jimbo la Niger na kuua watu saba waliokuwamo. 

By Jamhuri