Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Philip Mpango amesema katika kuelekea mwaka 2030, mataifa yanapaswa kujitoa upya na kuazimia kuongeza uwekezaji  zaidi katika sekta ya elimu kwa nia ya kuhakikisha Watoto wanapata elimu iliyo bora na ya uhakika.

Makamu wa Rais amesema hayo wakati akitoa hotuba katika Mkutano wa Umoja wa Mataifa uliobeba ajenda ya Mageuzi katika sekta ya elimu ulioshirikisha wakuu wa nchi na serikali kutoka mataifa mbalimbali, wakuu wa taasisi na mashirika pamoja na wadau wa elimu. Amesema kwa kuwa elimu ni sehemu muhimu ya ajenda ya maendeleo 2030 hivyo hakuna budi kuchukua hatua na masuluhisho katika kuleta mabadiliko kwenye sekta hiyo.

Makamu wa Rais amesema kupatikana kwa elimu bora kutapunguza matabaka katika ajira pamoja na kipato baina ya wananchi.

Amesema tayari Tanzania imechukua hatua mbalimbali katika kuboresha sekta ya elimu ikiwemo kuanza mchakato wa kuboresha mitaala kwa kuwashirikisha wadau wa elimu, kuwekeza katika vyuo vya ufundi stadi na mafunzo , kutoa elimu bila malipo kwa shule za msingi na sekondari pamoja na kuongeza bajeti ya wizara husika kufikia asilimia 18 ya bajeti yote ya serikali.

Aidha Makamu wa Rais amesema serikali ya Tanzania inahakikisha upatikanaji wa elimu jumuishi kwa wote bila kujali Jinsia , Ulemavu na hali ya uchumi. Ameongeza kwamba kwa kuzingatia maendeleo ya sayansi na teknolojia,serikali  pia imedhamiria kuboresha usimamizi wa nguvu kazi ya walimu ili kuboresha ufundishaji na ujifunzaji bora kwa kuwajengea uwezo walimu na maofisa elimu kuhusu uunganishaji wa teknolojia katika ufundishaji na ujifunzaji pamoja na uandaaji  wa masomo ya kidijitali.

Makamu wa Rais yupo nchini Marekani kumwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Baraza Kuu la 77 la Umoja wa Mataifa (UNGA

By Jamhuri