Home Kimataifa Marekani Kufufua Mazungumzo Kati ya Israel na Palestina

Marekani Kufufua Mazungumzo Kati ya Israel na Palestina

by Jamhuri

Ikulu ya Marekani inatarajia kuanzisha upya juhudi za kufikiwa  kwa makubaliano ya amani kati ya Israel na Palestina, licha ya uamuzi wa Rais Donald Trump kuitambua Jerusalem kuwa Mji Mkuu wa Israel.

Mpango huo wa Marekani unatarajiwa kuja baada ya awali kuliudhi taifa la  Palestina, mataifa ya Kiislamu na jumuiya ya kimataifa.

Maafisa utawala wa Marekani wamesema juhudi hizo huenda zikafufuliwa wiki ijayo kukiwa na matumaini kuwa ghadhabu dhidi ya hatua aliyoichukua Rais Trump itakuwa imepungua.

Wakati Serikali ya Marekani ikifikiria kufufua mpango huo, Rais wa Palestina, Mahamoud Abbas, amesema kuwa nchi yake haitakubali Marekani kuwa na jukumu lolote katika mchakato wa kutafuta amani katika mzozo wa Mashariki ya Kati.

Amesema tangu mwanzo, Serikali ya Marekani na washirika wake imeonekana kuwa upande tofauti na Wapalestina na kuongeza kuwa Palestina iko makini na haiwezi kuyumbishwa.

Rais Abbas amesema hii yote ni kwa sababu Marekani inaipendelea Israel na kuwa viongozi wa Palestina hawana mpango wa  kukutana na  Makamu wa Rais wa Marekani, Mike Pence, anayetarajiwa kwende Jerusalem wiki ijayo.

Pamoja na msimamo huo, bado Ikulu ya Marekani imesema ina matumaini ya ziara hiyo ya  Pence itakuwa sehemu ya kile ilichokitaja kama “kufungwa kwa ukurasa mmoja na kufunguliwa mwingine”.

You may also like