Rais wa Ujerumani, Frank- Walter Steinmeir, amehitimisha ziara yake katika bara la Afrika kwa kuhimiza masuala ya demokrasia na maendeleo ya kiuchumi.

 Katika ziara yake hiyo, Rais Steinmeir  amehimiza uimarishwaji vita dhidi ya ufisadi  na  mapambano imara juu ya  uhamiaji unaoendelea kuwa tishio kwa maisha ya binadamu hasa katika kipindi hiki.

Mataifa yote yanapaswa kuungana ili kukabiliana na janga hili linaloendelea kuangamiza maisha ya wanadamu wengi hasa wale wanaojaribu kuvuka bahari kuingia Ulaya,” amesema Rais Steinmeir.

Amesema Afrika inahitaji uwepo wa taasisi imara na siyo viongozi imara kama watu wengi wanavyodhani, na kuongeza kuwa kamwe Afrika haiwezi kupitia mafanikio kwa kuwa na kiongozi imara.

Amesema tatizo kubwa kwa baadhi ya nchi za Kiafrika ni kutilia maanani ujenzi wa viongozi imara, badala ya kuandaa taasisi imara zinazoweza kutoa mwongozo hata baada ya miaka 100.

Rais Steinmeir amesema wakati masuala ya uhamiaji yakiendelea kuwa tishio hasa katika nchi ya Gambia na nchi nyingine za Magharibi, wahusika kutoka upande wa Ulaya wanapaswa kukaa pamoja kutafuta suluhu ya matatizo hayo.

Kuendelea kuyafumbia macho masuala haya ya uhamiaji huku watu wengi wakiendelea kupoteza Maisha, ni sawa na uhaini unaopaswa kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa manufaa ya pande zote,” amesema Rais Steinmeir.

 Kwa upande wa Rais wa Gambia, Adama Barrow, akiwa na mgeni wake amesema tukio la uhamiaji haramu limeendelea kuwa tishio katika nchi nyingi za Kiafrika kutokana na vita ya wenyewe kwa wenyewe na majanga mengine.

Mimi mwenyewe ni mhanga wa uhamiaji haramu, nilipokuwa na  umri wa miaka 22, mwaka 1988, kwa kuvutiwa na hadithi za mafanikio kutoka kwa marafiki zangu pamoja na ndugu wengine; nilivutiwa kwenda Ulaya,” amesema Barrow.

Amesema kama vijana wengine alivutiwa yeye pia aliamini kwamba nchini Ujerumani kuna fedha na baada ya kurejeshwa nyumbani, amesema kuwa anaiona Gambia kama Ujerumani yake, Marekani yake na  Ulaya yake.

Kiongozi huyo alisema hayo  wakati alipowahutubia vijana katika chuo cha mafunzo katika ya Mji Mkuu wa Banjul na kuhadithia juu ya  madhila yaliyomkuta ya kurudishwa nchini mwake kutoka Ujerumani.

Please follow and like us:
Pin Share