Na Mwandishi Wetu, JamhuriMedia

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere, amezidi kuripoti madudu yaleyale yanayotokea katika mashirika ya umma.

Kupitia Ripoti Kuu ya Ukaguzi wa Mashirika ya Umma kwa Mwaka wa Fedha wa 2022/2023, Kichere, amesema katika ukaguzi alioufanya katika usimamizi wa matumizi kwa mwaka ulioishia Juni 30, 2023, amebaini mashirika ya umma 17 yenye matumizi ya Sh bilioni 72.36 yasiyo na tija.

“Hii inamaanisha kuwapo kwa ongezeko la asilimia 13 ikilinganishwa na mwaka uliopita kulipokuwa na mashirika ya umma 12 yenye jumla ya Sh bilioni 63.77,” amesema.

Akifafanua zaidi amesema matumizi yasiyokuwa na tija ni tozo za  adhabu na riba kutokana na kucheleweshwa kwa malipo ya wazabuni na makandarasi, kuchelewa kujaza, kutuma michango na makato ya watumishi yaliyoainishwa kisheria, kununua bidhaa zilizokwisha muda na zisizohitajika. 

Katika ukaguzi wake, amesema mashirika manne yamejirudia tena mwaka huu kufanya matumizi yasiyokuwa na tija licha ya kuripotiwa mwaka jana, huku 13 yamebainika kwa mara ya kwanza mwaka huu.

“Mashirika hayo ni Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA, Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza, na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO).

“Hii inasababisha upotevu wa fedha za umma na kutofikiwa kwa ufanisi wa matumizi sahihi ya rasilimali fedha zilizokabidhiwa kwa mashirika husika,” amesema.

Pia amesema amebaini mashirika 11 yenye matumizi yasiyostahili ya jumla ya Sh bilioni 4.64 ikiwa ni pungufu kwa asilimia 94 ikilinganishwa na Sh bilioni 77.75 kwa mashirika 21 kwa mwaka uliopita.

“Matumizi yasiyostahili ni malipo ambayo hayakidhi vigezo na matakwa ya kisheria na udhibiti, makubaliano ya kimkataba, na viwango vya uhasibu.

“Ukaguzi wangu unaonyesha mashirika matatu yamejirudia kati ya yale niliyoyaripoti mwaka jana huku manane yakiwa yametokea mwaka huu pekee. Mashirika ambayo yamejirudia ni: Mfuko wa Maendeleo ya Zao la Pamba, Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), TBS na TANESCO,” amesema.

Akikazia hoja hiyo, amesema baadhi ya matumizi yasiyostahili yalitokana na malipo kwa makandarasi kwa kazi wasizofanya au yaliyo kinyume cha masharti ya mkataba, malipo ya posho yasiyoidhinishwa, malipo yaliyolipwa kwa makosa mara mbili kwa wazabuni na malipo kwa wapokeaji wasiostahili.

Amesema upungufu huo unaonyesha uwapo wa matumizi mabaya ya fedha za umma na kuongeza wasiwasi wa kuwapo kwa udanganyifu na kuhatarisha ufanisi na usimamizi bora wa matumizi ya rasilimali fedha katika mashirika tajwa.

Vilevile amesema kuna uwezekano wa kutopata tija kwa malipo ya Sh bilioni 3.09 kwa ajili ya vifaa vya kukagulia magari katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

“Huenda vifaa hivyo visitumike kama ilivyokusudiwa kutokana na agizo la serikali la kusitisha ukaguzi wa magari ndani ya nchi kama ilivyokusudiwa awali,” amesema.

Hatua hiyo amesema ni baada ya Julai 9, 2020, serikali kuiagiza TBS kusitisha ukaguzi wa magari kupitia mawakala wa nje ya nchi uliohusisha uhakiki wa awali wa ubora wa magari yanayoingizwa nchini kufikia Februari, 2021 huku mikataba yao ilikuwa inamalizika.

“Ukaguzi maalumu TBS uliohusisha kipindi cha kuanzia Julai, 2020 hadi Desemba, 2022, ulibaini kuwa Desemba 9, 2020 ilisaini mkataba Na. PA/044/2020-2021/HQ/G/24 kwa ajili ya ugavi, usimikaji, upimaji wa  ufanisi, mafunzo na uzinduzi wa vifaa vya kukagulia magari kwa Euro milioni 1.24 sawa na Sh bilioni 3.39,” amesema na kuongeza:

“Pia nilibaini ucheleweshwaji wa kukamilika kwa mchakato wa ununuzi katika mkataba huo. Kutokana na ucheleweshwaji huo na katika jitihada za kupata vifaa vya kukagulia magari kabla ya ukomo wa mikataba na mawakala wa nje ya nchi, TBS iliingia mkataba mwingine wa ununuzi wa vifaa vya kukagulia magari vinavyohamishika Januari 29, 2021.

“Vifaa hivyo viliwasilishwa na mzabuni Machi, 2021 kwa bei ya Euro 143,853.42 sawa na Sh milioni 402.79. Vilevile nilibaini kuwa mkataba wa awali Na. PA/044/2020-2021/HQ/G/24 uliongezwa muda hadi Septemba, 2022 ili kuiruhusu TBS kuandaa na kujenga mahali vifaa hivyo vitakapofungwa.”

Vifaa katika mkataba huo, amesema viliwasilishwa Septemba 12, mwaka juzi na mzabuni alilipwa Euro milioni 1.18 sawa na Sh bilioni 3.09, ikiwa ni asilimia 95 ya bei ya mkataba huo lakini hadi mwisho wa ukaguzi mwezi Novemba, mwaka juzi vifaa hivyo havijafungwa bado na vilikuwa ofisi za TBS.

“Hii ilitokana na maagizo mengine ya serikali Julai, mwaka juzi ya kusitisha ukaguzi wa magari ndani ya nchi na TBS imerudi tena kutumia mawakala wa nje ya nchi,” amesema.

Katika hatua nyingine, amesema vifaa vya kukagulia magari vinavyohamishika vilivyotokana na mkataba wa pili vilifungwa na vilikuwa vinatumika kukagua yanayoingizwa nchini kutoka kwenye nchi ambazo TBS haina mawakala kwa kuwa kiwango cha uagizaji ni kidogo.

Amesema uamuzi kinzani uliofanywa unaweza kusababisha hasara ya Sh bilioni 3.09 zilizolipwa katika mkataba wa awali zikiwa ni gharama za ugavi, usimikaji, upimaji wa ufanisi, mafunzo na uzinduzi wa vifaa hivyo.

“Kwa sababu vifaa hivyo bado havijafungwa wala kuhakikiwa ufanisi wake hadi sasa na vinaweza visitumike tena,” amesema.

Kuhusu kasoro katika usimamizi wa sekta ya nishati, amesema TBS haitekelezi kwa ukamilifu hadidu za rejea za uwekaji wa vinasaba kwenye mafuta zilizo katika makubaliano kati yake na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA).

Amezitaja hadidu hizo zisizotekelezwa kuwa ni nne kati ya tisa, sawa na asilimia 44, na hali hiyo inaathiri juhudi za kuzuia uingizaji wa mafuta yaliyochepushwa na kuingiza katika soko la ndani bidhaa za mafuta za magendo zinazosafirishwa nje ya nchi.

Aidha, amesema amebaini kutokuwapo kwa uhakika juu ya urejeshwaji wa Sh bilioni 14.7 za kodi na tozo za uingizaji wa mafuta nchini.

Amesema fedha hizo zililipwa na Kampuni Tanzu ya Mafuta (TANOIL) ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) katika shehena za mafuta zilizokuwa na zuio kwa kushindwa kulipa gharama kwa mzabuni na baadaye kuuzwa kwa kampuni zingine za uuzaji wa mafuta.

Kuhusu kukusanya fedha, amesema amebaini mashirika 66 hayakukusanya Sh bilioni 284.71 kutoka katika bajeti ya vyanzo vya ndani katika mwaka wa fedha wa 2022/2023.

Pia amesema amebaini manane yalitumia zaidi ya bajeti kwa kiasi cha Sh bilioni 21.14 bila idhini ya ofisa masuuli au bodi ya wakurugenzi.

Ufanisi mdogo

Katika kipindi cha muda mfupi, amesema  ukaguzi wake wa ripoti ya kubadilisha mita katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 umebaini jumla ya mita 108,088 kati ya 602,269 zilibadilishwa kabla ya kipindi cha uhai wa matumizi yake kwisha.

Amesema ukaguzi huo umebaini mita 13,493 zilibadilishwa ndani ya kipindi cha mwaka mmoja baada ya kufungwa, wakati 94,595 zilikuwa na muda mfupi wa matumizi kati ya mwaka mmoja hadi miaka 15, ikilinganishwa na unaotarajiwa wa miaka 20 ndipo zibadilishwe.

Hatua hiyo amesema imesababishwa na uduni wa mita zilizowekwa na mabadiliko ya haraka ya teknolojia yaliyosababisha kushindwa kufikia muda wake uliotarajiwa.

“Kubadilisha mita mapema husababisha gharama zaidi inayoathiri utendaji wa kifedha wa shirika,” amesema.

Katika mwaka wa fedha wa 2022/2023, amesema TANESCO ilifanya malipo ya dola milioni 10.16 za Marekani kwa mzabuni katika mkataba Na. PA/001/2018-2019/HQ/W/31 kwa ajili ya kubuni, kusimika, kutekeleza, kutoa mafunzo na kuzindua mfumo wa usimamizi wa biashara, kusaidia miundombinu ya mfumo huo na kutoa ushauri elekezi.

Hata hivyo, amesema amebaini malipo hayo yalifanywa bila kuthibitishwa kwa ubora wa kazi husika na mshauri elekezi.

“Hii ni kinyume na Kifungu cha 4.4 cha Mwongozo wa Uendeshaji wa Kitengo cha Uwekezaji cha TANESCO cha mwaka 2020 na Kifungu 3.3 cha Maelekezo ya Uhasibu C12 ya Mwongozo wa Uhasibu ya TANESCO ya mwaka 2022.

“Hali hii imetokana na mratibu wa mradi aliyeteuliwa kutekeleza majukumu mawili kwa wakati mmoja, kama meneja wa mradi na kama mthibitishaji wa malipo, ikiwa mshauri elekezi hayupo. Kwa maoni yangu katika hali kama hii kuna hatari ya mzabuni kulipwa kwa kazi ambazo hazijatekelezwa kama inavyotakiwa kwenye mkataba,” amesema.

Kuhusu ukaguzi wake wa gharama za safari za nje katika TANESCO, amesema amebaini watumishi watano walilipwa dola 34,623 za Marekani sawa na Sh milioni 89 kusafiri nje ya nchi bila kupata kibali cha kusafiri.

Ktendo hicho amesema ni kinyume cha Aya Na. 1 ya Mwongozo wa Utumiaji wa Mfumo wa Vibali vya Kusafiri Toleo Na. 1 la mwaka 2016, na hali hii ilisababishwa na upungufu wa udhibiti wa ndani unaoruhusu malipo ya posho ya kujikimu kwa safari za nje bila kibali kutoka kwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Kwa upande wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), amesema ukaguzi wake umebaini kiwango kidogo cha ongezeko la safari za ndege za kimataifa.

Amesema mpango mkakati wa ATCL kwa mwaka wa fedha wa 2022/23 hadi 2026/27 ulikuwa ni kuongeza safari za kimataifa ifikapo Juni 30, mwaka juzi.

Safari hizo amesema zilijumuisha Dzaoudzi-Mayotte, Ufaransa na Johannesburg ifikapo 30 Juni 2023.

“Wakati wa ukaguzi nilibaini safari za kimataifa zilizopangwa kuanzishwa mwaka 2023 hazikutekelezwa. Hii inasababisha kutokuwa na matumizi bora ya ndege kwa ajili ya safari za nje.

“Hii ilichangiwa na mikakati duni ya kampuni katika kuongeza safari za kimataifa kwa ndege zilizopo. Kushindwa kuongeza safari za ndege za kimataifa kutasababisha kampuni kupoteza mapato kutokana na matumizi yasiyotosheleza ya uwezo wa ndege,” amesema.

Kuhusu Kiwanda cha Dawa Keko kufanya ununuzi wa dola milioni 4.97 za Marekani bila kufuata sheria, amesema alibaini hakikuanzisha bodi ya zabuni kwa ajili ya kuwezesha ununuzi wa bidhaa, huduma, kazi za ujenzi na uondoaji wa mali za umma kupitia mchakato wa zabuni kinyume cha matakwa ya Kifungu cha 31 (1)-(2) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura 410.

“Kutokana na hali hiyo, nilikuta ununuzi wenye thamani hiyo ambao mchakato wake na kuidhinishwa ulifanywa na mkurugenzi wa fedha na ofisa masuuli pekee. Hii ni kinyume cha Kifungu cha 33 (1)(c) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma Sura 410.

“Pia nilibaini ofisa masuuli hakuteua kamati ya kutathmini zabuni kama inavyotakiwa na Kanuni ya 202 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma ya mwaka 2013 iliyofanyiwa marekebisho na Kanuni ya 69 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma (Kama zilivyorekebishwa) za mwaka 2016. Hii ilisababisha kutokuzingatiwa kwa taratibu za tathmini katika zabuni za ununuzi,” amesema.

Katika ukaguzi wake pia amebaini kuna mikataba yenye thamani ya Sh bilioni 9.89 na dola milioni 2.95 za Marekani hazijawasilishwa kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) au maofisa sheria kwa uhakiki.

“Ripoti yangu ya mwaka 2021/2022 ilionyesha mikataba yenye thamani ya Sh bilioni 45.71 na dola milioni 7.46 za Marekani katika mashirika ya umma manane kutokuhakikiwa na AG, hali hiyo imejirudia katika ukaguzi niliofanya mwaka huu wa 2022/2023.

“Ukaguzi wangu ulibaini katika mashirika manne ambayo hayakufanya uhakiki wa mikataba kwa AG wala ofisa sheria wa shirika husika kabla ya kusaini mikataba hiyo kinyume na Kanuni ya 59 na 60 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma za mwaka 2013 kama zilivyorekebishwa na kanuni ya 2 na 3 ya Kanuni za Ununuzi wa Umma (Marekebisho) za mwaka 2016,” amesema.

Kutokuhakikiwa kwa mikataba na AG kabla ya utekelezaji, amesema kunaweza kusababisha uwapo wa vifungu visivyo na tija kwa taasisi husika na kusababisha hasara wakati wa utekelezaji.

Hasara ya Sh bilioni 1.99 amesema imepatikana katika Bohari Kuu ya Dawa MSD baada ya ununuzi wa vitendanishi visivyokidhi viwango vya Uviko-19 vijulikanavyo kama Next Generation Sequencing (NGS).

Julai 15, 2021, amesema amebaini Mkurugenzi Mkuu wa MSD alimwandikia barua mzabuni kwa ajili ya ununuzi wa vitendanishi hivyo vyenye gharama ya Sh bilioni 2.08 kwa mahitaji ya haraka.

Ununuzi huo amesema ulijumuisha vitendanishi vya NGS vinavyoendana na kifaa cha ‘Ion Torrent Next Generation Sequencing Platform’ vyenye thamani ya Sh bilioni 1.99 pamoja na ‘Nasal Pharyngeal Swabs’ yenye thamani ya Sh milioni 86.91 kwa madhumuni ya kutumika katika Maabara ya Taifa ya Afya ya Jamii (NPHL).

“Agosti 24, 2021 MSD ililipa Sh milioni 997.82 kwa mzabuni. Desemba 11, 2021 mzabuni aliwasilisha kifurushi kimoja. Baada ya kuchunguzwa na kuthibitishwa na mtaalamu wa NPHL, ilibainika bidhaa zilizowasilishwa hazikukidhi viwango na haziendani na mahitaji ya mashine ya NPHL.

“Licha ya taarifa ya Januari 19, 2022 ya kutokukidhi viwango na kutoendana na mashine kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Maabara ya Taifa ya Afya kwenda MSD, mzabuni huyo aliwasilisha vifurushi vinne vilivyobaki Februari 11, 2022,” amesema.

Pia amesema alibaini Februari 25, 2022 MSD ilifanya malipo ya mwisho ya Sh milioni 997.82 kwa ajili ya bidhaa zilizowasilishwa licha ya kutoendana na viwango bila kuzingatia maelezo ya awali yaliyotolewa na Mkurugenzi Mkuu wa NPHL.

Ununuzi wa vitendanishi visivyofaa, amesema ulichangiwa na kutoa zabuni kwa mzabuni asiye mtengenezaji. Pia kamati ya tathmini ya zabuni ilikosa mjumbe mwenye utaalamu wa vitendanishi vinavyotakiwa kulingana na Kifungu cha 40 (4) cha Sheria ya Ununuzi wa Umma.

Pia amesema kuna bidhaa au vifaa visivyotumika, vilivyopitwa na wakati na vinavyotumika polepole vyenye thamani ya Sh bilioni 6.57 katika ghala la MSD.

“Mwongozo wa usimamizi wa mali ghalani wa MSD wa mwaka 2018 unaeleza kuwa vifaa visivyotumika vinahitaji kutolewa au kuuzwa na vifaa vinavyotumika polepole vinahitaji kugawiwa kwenye hospitali zingine.

“Vifaa hivyo ni matokeo ya mabadiliko katika teknolojia kama vile mashine za X-ray ambazo kwa sasa zipo za kidijitali na makadirio duni ya mahitaji yasiyotumika na magonjwa yanayotangazwa kuwa si janga tena kama Uviko-19,” amesema.

Kuhusu kasoro katika usimamizi wa sekta ya nishati, amesema bidhaa za mafuta na gesi za 72,533.56 MMscf zilizalishwa na Sh bilioni 1,042 zilitozwa na watoa huduma kama tozo za uunganishaji wa gesi asilia lakini hazikuidhinishwa na EWURA, ikiwa ni kinyume cha Kanuni ya 20 ya Kanuni za Upangaji Bei ya Petroli na Gesi Asilia za mwaka 2020.

Vilevile amesema hakukuwa na hatua zilizochukuliwa na EWURA dhidi ya watoa huduma hao na hali hiyo inaweza kuathiri haki na uwazi katika upangaji wa bei wa soko katika sekta ya gesi asilia.

Amesema EWURA haikuwachukulia hatua wazalishaji wadogo 11 kati ya 15 waliopewa leseni na haikuchukua hatua kwa wengine zaidi 10 waliosajiliwa na hawakuwasilisha taarifa zao za mwaka kinyume cha kanuni za uzalishaji wa umeme za mwaka 2020 zinazowataka wazalishaji hao kuwasilisha taarifa zao za mwaka ndani ya siku 120 baada ya mwaka wa fedha kwisha.

“Hii inaweza kuathiri uwezo wa EWURA katika kupanga na kukadiria mahitaji ya nishati ya umeme,” amesema.

Pia amesema hakuna viwango vya ujenzi wa uuzaji wa rejareja wa mafuta kwa wafanyabiashara wenye angalau vituo vinne kwenye majiji, manispaa au miji ya wilaya kinyume cha kanuni ya 7(1)(2)(3) 7(1)(2)(3) ya Kanuni za Petroli za Mwaka 2022.

“Nilibaini kwa sasa EWURA haifuatilii  uzingatiwaji wa kanuni hii na inaweza kusababisha kutokuwapo kwa usawa wa mgawanyo wa nishati ya mafuta kati ya jamii za mijini na vijijini, kuathiri sekta zingine na kuzuia usawa katika kukuza uchumi wa kikanda,” amesema.

Jumla ya wauzaji wakubwa wa mafuta na gesi asilia 12, amesema wamepewa leseni za biashara hiyo na walikuwa wakiendelea hadi Juni 30, mwaka jana.

Baada ya kufanya mahojiano na menejimenti ya EWURA na mapitio ya rejista ya leseni, amesema amebaini EWURA haivisajili wala kuvifuatilia vituo vya uuzaji rejareja wa mafuta  na gesi. Pia haikukagua wala kufanya udhibiti wa vituo hivyo kinyume cha kanuni ya 46(1) ya kanuni za petroli za mwaka 2020.

Hali hiyo amesema inaweza kusababisha udhaifu katika usimamizi, utunzaji na usafirishaji wa petroli na gesi asilia na hasa kusababisha majanga kama vile kuvuja kwa mafuta na gesi, moto au milipuko na kuhatarisha usalama wa jamii.

Amesema hakuna mkakati ulioanzishwa na kuidhinishwa wa kusimamia na kuhakikisha kiwango cha chini cha bidhaa za mafuta kinahifadhiwa na wauzaji wa jumla na wadogo wadogo kinyume cha kanuni ya 25(2)(b)(iii) ya Kanuni za Petroli za Mwaka 2022.

“Hali hii inaweza kusababisha baadhi ya wauzaji wenye leseni kutohifadhi kiwango cha kutosha cha mafuta na kusababisha uwezekano wa kuwapo kwa upungufu wa mafuta na kuathiri watumiaji,” amesema.

Kwa upande wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), amesema baada ya kufanya ukaguzi wa muda uliotumika katika maabara ya kuchukua vipimo na kutoa majibu amebaini ucheleweshaji mkubwa wa baadhi ya vipimo.

Amesema alifanya ukaguzi wa sampuli za vipimo 50 kutoka vitengo mbalimbali katika kipindi kilichoishia Juni 30, mwaka jana.

Kati ya hivyo, amesema vipimo 26 vilichukua muda mrefu zaidi ya uliopangwa, kuanzia saa nne hadi saa 260 na hatua hiyo ni kinyume cha muda uliobainishwa kwenye mpango mkakati wa mwaka 2022 hadi 2027.

“Sababu kuu za kuchelewa zilikuwa kuharibika kwa mashine za vipimo bila kuwa na mashine mbadala na upungufu wa vitendanishi. Hali hii inasababisha kuchelewa kwa matokeo ya vipimo; hivyo kuathiri ufanisi wa maabara.

“Muda mrefu unaotumiwa na Muhimbili kuchukua vipimo na kutoa majibu unazorotesha huduma za afya kwa njia mbalimbali. Wagonjwa wanasubiri muda mrefu, ufanisi wa hospitali unapungua na wateja hawaridhiki,” amesema.

Katika ukaguzi wake mwingine MNH-Mloganzila, amesema amebaini kuwa vifaa tiba 406 kati ya 2,565 sawa na asilimia 16 vina hitalafu, havifanyi kazi. Pia hakukuwa na mpango wa kuvitengeneza.

Amesema ukaguzi huo ulionyesha dosari katika kutekeleza mpango wa matengenezo ya kuzuia vifaa tiba kuharibika.

“Vifaa 60 sawa na asilimia 31 kati ya 192 ndivyo vilivyofanyiwa matengenezo yanayotakiwa, kutokana na ukosefu wa fedha za kufanya matengenezo. Hii inaweza kuharibu vifaa mapema na kuongeza gharama za ukarabati au uagizwaji,” amesema na kuongeza:

“Vifaa tiba visivyofanya kazi vinaathiri utoaji wa huduma kwa wagonjwa kwa kuchelewa kutoa huduma, hivyo kuhatarisha afya za wagonjwa. Kuendelea kukarabati au kubadilisha vifaa visivyofanya kazi kunaweza kuwa na gharama kubwa.

“Vifaa vyenye kasoro vinaweza kupunguza kasi ya utendaji kazi wa kitabibu, kuongeza muda wa kusubiri kwa mgonjwa na kupunguza ufanisi wa utoaji wa huduma ya afya ndani ya hospitali.”

Wakataa kutoa majibu

Wiki iliyopita baada ya ripoti hiyo kutolewa, JAMHURI imemtafuta Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Profesa Mohamed Janabi, atoe ufafanuzi wa hoja alizoziibua CAG kuhusu taasisi anayoiongoza lakini kwa ufupi akasema: “Wizara ya Afya itakuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kutoa ufafanuzi katika hili.”

Kwa upande wake, Meneja Uhusiano na Masoko wa TBS, Gladness Kaseka, ameiambia JAMHURI: “Katika ripoti ya CAG hatuwezi kusema chochote kutokana na kile kilichoibuliwa.”

Maoni mbadala

Hivi karibuni, Msajili wa Hazina, Nehemia Mchechu, amesema watafanya uchambuzi wa kina wa hoja zilizoibuliwa katika Ripoti ya CAG kuhusu mashirika ya umma na pale itakapohitajika watachukua hatua.

“Pale itakapohitajika kulisaidia shirika tutafanya hivyo kuwapa mtaji au kile kilichokwama,” amesema.

Pia amesema wataangalia mwenendo wa mashirika yaliyopata hasara kama yanaweza kuboreshwa.

Amesema kwa mwaka huu mashirika mengi yamejitahidi tofauti na mwaka uliopita na ameahidi watafanya uchambuzi kubaini kama kuna yanayotakiwa kuunganishwa au kufutwa.

“Tutakuwa tunafanya uchambuzi na utatupa majibu ama kuyafuta au kuyaunganisha mashirika baada ya kutambua tatizo liko wapi na ukilitatua litafanya vizuri,” amesema.

Kwa upande wake, Ludovick Utouh, amesema kuna maeneo yanayohitaji nguvu zaidi katika ripoti zinazotolewa na CAG.

Utouh ambaye ni CAG mstaafu ametoa kauli hiyo kupitia andiko lake alilolitoa hivi karibuni likiwa linafanana na kile alichowahi kusema siku za nyuma alipozungumza na JAMHURI.

Amesema ili kuongeza utekelezaji wa mapendekezo ya CAG, ameshauri Katibu Mkuu Kiongozi kuwataka watumishi wote wanaopaswa kuchukua hatua wajieleze ni hatua gani wamechukua na ikibainika hawajachukua wachukuliwe hatua kwa kushindwa kuchukua hatua.

“Ni bora Katibu Mkuu Kiongozi akafuata mtiririko wa kiutumishi wa kuwawajibisha wahusika ili kuimarisha mfumo,” amesema. 

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), Naghenjwa Kaboyoka, ameiambia JAMHURI wiki iliyopita kwamba bado hawajaanza kuichambua ripoti hiyo.

“Nilikuwa safarini, kwa hiyo bado hatujaichambua. Nipe muda kidogo hadi wiki ijayo (wiki hii) tutakuwa tumeshaanza kuisoma na kuifanyia uchambuzi,” amesema.

Please follow and like us:
Pin Share