Na Jumanne Magazi, JamhuriMedia, Dar es Salaam

Waziri wa Uchukuzi Makame Mbarawa amepokea seti ya kwanza ya vichwa vitano vya treni ya umeme EMU,maarufu mchongoko na mabehewa matatu ya abiria vyenye thamani ya Dola za Marekani mil 190.

Ameyasema hayo wakati wa kupokea shehena hiyo ambapo amesema hadi sasa Serikali kupitia Shirika la Reli nchi limeshapokea jumla ya mabehewa 65, huku seti nyingine za EMU zitaendelea kuwasili,kila mwezi hadi mwezi Oktoba mwaka huu.

Aidha Mbarawa amesema kuwasili kwa vitendea kazi hivyo kunaifanya TRC, kuwa tayari kuanza kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria na mizigo kupitia reli ya kisasa na ya kimataifa.

Mbarawa amesema kichwa kimoja cha umeme kina uwezo wa kuvuta mabehewa nane huku ikiwa na uwezo wa kubeba abiria 589 kwa safari moja.

Waziri huyo ameendelea kusema kuwa tayari Serikali kupitia Shirika la TRC, lilifanya manunuzi ya seti kumi (10) treni ya kisasa ijulikanayao kama ELetric Multiple Unit,kutoka kwa watengenezaji wa kampuni ya Hyundai Rotem ya nchini Korea kusini.

Aidha Mbarawa amesema leo Tanzania imeandika historia nyingine kwa kuingia vichwa hivyo vya EMU kwa jina la utani vichwa “mchongoko”, nakuzima maneno ya watu wasioitakia mema nchi hii kuhusu Treni hii ya kisasa.

Kwa upande waka Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa TRC, Amina Lumuli ameseme seti moja ya EMU,inauwezo wa kubeba abiria 589 ambao ni idadi kubwa ukilinganisha na usafiri mwingine.

Aidha Lumuli amemshukuru Rais Dkt, Samia Suluhu Hasan, kufuatia juhudi zake za kuwaletea wananchi maendeleo hususani katika sekta ya uchukuzi hapa nchini.

Naye Meneja Manunuzi na mitambo wa TRC, Mhandisi Kelvin Kimario amesema EMU ni Treni iliyoundwa kwa teknolojia ya kisasa, inayomuwezesha abiria kupata huduma muhimu ikiwemo Mtandao (Wi-Fi) sehemu ya kukaa watu wenye mahitaji maalum,mifumo ya ubaridi, kamera maalum za usalama (CCTV camera ).

Katika huta nyingine Mkuu wa Mawasiliano wa TRC, Bi Jamila Mabrouk ameviomba vyombo vya habari kusaidia kulitangaza Shirika Reli nchini hususani mradi huu wa Reli ya kisasa ya SGR iliwaweze kuitumia kwa manufaa yao.

Katika hatua nyingine Waziri Mbarawa ameeleezea maendeleo ya ujenzi wa Mradi wa SGR, awamu ya kwanza yamefikia asilimia 98.90 kwa kipande Cha kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro chenye urefu wa km
300, huku asilimia 96.51 kipande Cha kutoka Morogoro hadi Makutupora.

Aidha amevitaja vipande vya kutoka Makutupora hadi Tabora kuwa ujenzi umefikia asilimia 13.98 ambapo asilimia 5.44 ni kipande Cha kutoka Tabora hadi Isaka, huku asilimia 54.01 ni kipande Cha kutoka Isaka hadi Mwanza alimalizia kusema Waziri Mbarawa.

By Jamhuri